Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OHCHR yaelezea hofu yake juu ya mashambulizi ya Israel kaskazini mwa Gaza

Wafanyakazi wa uokoaji na raia wamekusanyika karibu na moto katika kambi ya mahema ya watu waliokimbia makazi yao karibu na Hospitali ya Al-Aqsa huko Gaza usiku.
UN Vikosi vya Israel vililenga na mikombora mahema ya kuwahifadhi raia waliokimbia makazi yao karibu na Hospitali ya Al-Aqsa, katika eneo ambalo watu kutoka kaskazini mwa Gaza waliambiwa kuhama.

OHCHR yaelezea hofu yake juu ya mashambulizi ya Israel kaskazini mwa Gaza

Amani na Usalama

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, leo imeelezea wasiwasi wake juu ya operesheni za kijeshi za Israel kaskazini mwa Gaza, na kuonya kwamba mchanganyiko wa mashambulizi yasiyo na kikomo, watu kulazimika kukimbia makwao na vikwazo vikali vya misaada ya kibinadamu inaweza kuwa ni "maangamizi ya jumla ya wakazi wa Palestina katika eneo la Ukanda huo”

Maisha "hayawezekani tena kwa raia walionaswa kaskazini huku kukiwa na maagizo ya mara kwa mara ya ya jeshi la Israel ya kuwataka kuhama na kupunguzwa kwa ufikiaji wa mahitaji muhimu ya kibinadamu, na hivyo kuwaacha watu wengi kwenye ukingo wa njaa,”  imesema ofisi hiyo jana Jumapili.

Taarifa ya OHCHR imeendelea kusema kuwa "Wakati jeshi la Israel limetaka raia wote kuondoka kaskazini mwa Gaza, limeendelea pia kulipua na kushambulia eneo hilo bila kuchoka, hasa ndani na karibu na Kambi ya Jabalya. Mashambulizi haya yamefanya kuwa hatari sana kwa raia kukimbia."

Pia ofisi hiyo imeripoti hofu miongoni mwa Wapalestina kwamba kuondoka kunaweza kumaanisha kuwa hawataruhusiwa kurejea makwao.

Vikosi vya Israel vimeharibu nyumba na shule zinazotumika kama makazi, na kuwaacha raia wengi bila kimbilio wakati msimu wa baridi unakaribia.

Shambulio baya la anga la Jumamosi lilipiga kizuizi cha makazi huko Beit Lahiya, na kuua takriban watu 87, kulingana na wizara ya afya ya Gaza.

Mashambulizi hospitali

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA mateso hayo yameongezeka zaidi huku hospitali zikipambana na uhaba mkubwa wa mafuta na vifaa vya matibabu, na timu za uokoaji zinaripoti kuzuiwa au kushambuliwa wakati wa kujaribu shughuli za kuokoa maisha ya watu.

"Hospitali zimepigwa na kuachwa bila nguvu huku watu waliojeruhiwa wakiachwa bila huduma," amesema Philippe Lazzarini, mkuu wa UNRWA kwenye mtandao wake wa kijamii wa X.

Ameongeza kuwa "Kukataa na kutumia msaada wa kibinadamu kama silaha ili kufikia malengo ya kijeshi ni ishara ya jinsi dira ya maadili ilivyo chini, hakuna mtu anayepaswa kuomba kusaidia au kusaidiwa".

Kila dakika ni muhimu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, imeitaka mamlaka ya Israel kuruhusu upatikanaji wa haraka wa fursa ya kuwaokoa watu kadhaa ambao bado wamekwama kwenye vifusi.

"Kila dakika inahesabika, hapo awali, idhini zilizocheleweshwa zilisababisha timu za uokoaji kurejesha maiti," limesema chapisho la OCHA kwenye kwenye ukurasa wake wa X.

Limeongeza kuwa upatikanaji wa mtandao umetatizwa na takriban waandishi wa habari watatu wa Kipalestina wameuawa, na hivyo kuzuia mtiririko wa habari kutoka eneo hilo.

Vita lazima ikome sasa

Naye Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati pia amelaani kuendelea kwa mashambulizi hayo.

Katika taarifa yake Tor Wennesland amesema “Hali inazidi kuwa mbaya Gaza. Matukio ya kuogofya yanajitokeza katika Ukanda wa kaskazini huku kukiwa na vita, mashambulizi ya Israel na janga la kibinadamu linaozidi kuwa baya,"

Ametoa wito wa kumalizika mara moja kwa vita, kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas, na kukomeshwa kwa hali ya watu kulazimishwa kuhama makazi yao.

Amesisitiza haja ya kuwalinda raia na kuruhusu misaada ya kibinadamu bila kuzuiliwa.

Amehitimisha taarifa yake kwa kusisitiza kwamba "Safari iliyo mbele itahitaji ujasiri, utashi wa kisiasa na mazungumzo mapya. Tuna deni kwa familia zinazoteseka huko Gaza na Israeli. Vita lazima ikome sasa."