Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zote na mashirika ya kimataifa ikiwemo UN wanawajibika kukomesha ukaliwaji wa Palestina

Kizuizi cha kutenganisha zege chenye mnara uliounganishwa mbele, na mji wa kilima wenye paa zenye vigae vyekundu nyuma.
Ryan Rodrick Beiler Ukuta wa kutenga eneo la ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Nchi zote na mashirika ya kimataifa ikiwemo UN wanawajibika kukomesha ukaliwaji wa Palestina

Amani na Usalama

Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu eneo linalokaliwa la Palestina leo imesema mataifa yote na mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa, wana wajibu chini ya sheria za kimataifa wa kukomesha uwepo haramu wa Israel katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, wakati mashambulizi dhidi ya Gaza yakishika kazi na kuongeza madhila kwa raia.

Tume hiyo huru imeyasema hayo katika taarifa mpya ya msimamo wa kisheriia iliyotolewa mjini Geneva Uswis kuhusu eneo linalokaliwa la Palestina ikiwemo Jerusalem Mashariki ambayo imeweka wazi maoni ya tume kuhusiana na wajibu wa serikali na jinsi Baraza Kuu na Baraza la Usalama linavyoweza kutambua na kutekeleza mbinu na hatua sahihi zinazohitajika kwa kazi hiyo hadi mwisho wa ukaliwaji huo, na kwa haraka iwezekanavyo.

Tume ihiyo imebaini kwamba maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu matokeo ya Kisheria yanayotokana na sera na desturi za Israel katika eneo linalokaliwa la Palestina ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki ni wenye mamlaka na usio na utata kwa kusema kwamba kuendelea kuwepo kwa Israel katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu ni kinyume cha sheria na sheria ya kimataifa.

Taarifa hiyo ikitolewa Geneva Gaza kwenyenyewe hali inaendelea kuwa tete  , kwa mujibu wa Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestinna UNRWA  Phillipe Lazzarini, kwani shule nyingine ya UNRWA imeshambuliwa leo Jabalia Kaskazini mwa Gaza, watu kadhaa wameripotiwa kuuawa na miongoni mwao Watoto wengi waliokuwa wakipata hifadhi katika jengo hilo.

Lazzarini amesema hili ni shambulio la tatu dhidi ya majengo ya UNRWA kwa wiki moja. Na pia wafanyakazi wa shirika hilo wanaendelea kuuawa sasa wameffikia 231 tangu kuanza kwa vita hii Oktoba mwaka jana.

Msahirika ya UN

Naye msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF James Elder akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo amesema “Gaza ni mfano halisi wa ulimwengu wa kuzimu duniani kwa watoto milioni moja wa eneo hilo. Na hali inazidi kuwa mbaya, siku baada ya siku, tunapoona athari za kutisha za mashambulizi ya anga ya kila siku na operesheni za kijeshi za Israek kwa watoto wa Kipalestina.”

Nalo shirika la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA likiangazia Ukingo wa Magharibi limesema “Vikosi vya Israel vimekuwa vikitumia mbinu mbaya za vita katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na kuibua wasiwasi mkubwa juu ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na kuongeza mahitaji ya kibinadamu ya watu.” Ameelezea wasiwasi kuhusu mashambulizi ya walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina na miti yao ya mizeituni wakati huu wa mavuno ya kila mwaka.

Kifo cha Yahya Sinwar uwe mlango wa kufunga vita Gaza: Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kifo cha kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar kinapaswa kuwa chachu ya kumalizika kwa haraka kwa vita iliyodumu mwaka mzima huko Gaza, kuachiliwa kwa mateka wote na utoaji wa misaada ya kibindamu bila vikwazo, kwa mujibu wa naibu msemaji wake. Farhan Haq akizungumza na waandishi wa habari leo mjini New York Marekani Katibu Mkuu "Ingawa hazungumzi juu ya matukio ya aina hii, Katibu Mkuu ana nia kwamba hii sasa itasababisha usitishaji wa mapigano mara moja, kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote na ufikishaji wa misaada ya kibinadamu usio na kikomo kwa watu Gaza."