GAZA: Zaidi ya watu milioni 1.8 wakabiliwa na njaa kali
GAZA: Zaidi ya watu milioni 1.8 wakabiliwa na njaa kali
Zaidi ya wapalestina milioni 1.8 huko Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na hali mbayá ya njaa, wakati huu ambapo asilimia 70 ya mashamba ya mazao yameharibiwa na mbinu za kujipatia kipato zimevurugwa na mashambulio yanayoendelea kufanywa na Israeli.
Hii ni kwa mujibu wa tathmini ya kiwango cha hali ya chakula, IPC iliyotolewa leo Alhamisi na jopo linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa, jopo ambalo limefanya tathmini ya hali ya chakula kwenye ukanda huo.
Takwimu kutoka ripoti hiyo zinaonesha kuwa watu 133,000 sawa na asilimia 6 ya wakazi wa eneo hilo lililozingirwa tayari wanakabiliwa na kiwango cha juu zaidi cha ukosefu wa chakula Awamu ya 5 au baa la ukosefu wa uhakika wa chakula.
Hofu ni kwamba idadi hiyo inaweza kufikia 345,000 sawa na asilimia 16 kati ya miezi ya majira ya baridi kali ambayo ni Novemba hadi Aprili mwakani.
“Hatari ya baa la njaa kuendelea Gaza ni kubwa. Kwa kuzingatia ongezeko la hivi karibuni la uhasama, kuna wasiwasi kwamba hali hii mbayá inaweza kutokea,” imesema tathmini hiyo.
Hali haivumiliki
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametiwa hofu na ripoti hiyo wakati huu ambapo pia kuna viwango vya juu vya watu kufurushwa na vile vile vizuizi vya kupeleka misaada ya kibinadamu, amesema Nabu Msemaji wa UN Farhan Haq akizungumza na waandishi wa habari leo New York, Marekani.
“Mwakammoja wa mzozo baa la njaa linanyemelea. Hii haiwezi kuvumilika.” Amesema Haq.
Katibu Mkuu anatoa wito kwa Israeli kufungua mara moja vivuko vyote vya kupitishia misaada.
Halikadhalika, urasimu na vikwazo vingine lazima viondolewe, na sheria na utaratibu urejeshwe Gaza ili mashirika ya Umoja wa Mataifa yaweze kusambaza misaada ya kiutu.
Mapendekezo makuu
Tathmini hiyo pia inasisitiza kuwa kasi ya kutumbukia kwenye baa la njaa inaweza kudhibitiwa tu pale ambapo watu watapa chakula cha kutosha, vifaa vya matibabu, na huduma za msingi katika Ukanda wote wa Gaza.
Inatoa wito wa kupitishwa mara moja kwa sitisho la mapigano na bila masharti yoyote, kurejeshwa kwa mifumo ya uzalishaji chakula, na kuzuia kwa ubora zaidi na udhibiti wa unyafuzi au utapiamlo uliokithiri.
Halikadhalika miradi ya kupatia watoto wachanga na watoto vyakula vya virutubisho irejeshwe ikiwemo pia huduma za unyonyeshaji watoto n ahata wale wasionyonyeshwa.
Hatua ya UN
Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa upande wao yameendelea kusaidia raia wa Gaza licha ya changamoto kali ikiwemo ukosefu wa usalama, vikwazo vya kufikisha huduma au kufikia wahitaji, amri zinazoendelea kutolewa za kuhama pamoja na mapigano.
Mathalani FAO ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, limepatia kipaumbele kuanzisha tena uzalishaji wa mazao na upatikanaji wa vyakula vyenye viwango vya juu vya lishe hasa wakati huu ambapo msimu wa baridi kali unakaribia. Hata kabla ya vita, majira ya baridi kali Gaza yaliambatana na viwango vya juu vya njaa na utapiamlo.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Beth Bechdol, amesema “misaada ya kibinadamu pekee haitoshi. Watu wanahitaji chakula kutoka shambani na chenye lishe. Ili kuleta tofauti, tunahitaij pia kusaidia wakulima kuendelea kuanzisha tena uzalishaji wa chakula, vile vile kuwezesha kuingizwa kwa vyakula na bidhaa zisizo vyakula kutoka nje ya Gaza.”