Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya kila uchao Gaza- OCHA

Joyce Msuya, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Dharura wa Misaada, akitoa taarifa kwa Baraza la Usalama kuhusu hali ilivyo Mashariki ya Kati.
UN /Evan Schneider Joyce Msuya, Kaimu Mkuu wa OCHA akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Hali ya Mashariki ya Kati, hususan Suala la Palestina

Hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya kila uchao Gaza- OCHA

Amani na Usalama

Hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na kikao kuhusu Hali Mashariki ya  Kati hususan Suala la Palestina wakati huu ambapo tangu Oktoba 5, jeshi la Israeli limekuwa likiendesha operesheni za kijeshi katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza ambako Israeli inadai wanamgambo wa Hamas wanajaribu kuimarisha tena  uwezo wao.

Akihutubia Baraza, Kaimu Mkuu wa Ofisi ya  Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA, Joyce Msuya amesema tangu ahutubie Baraza wiki moja iliyopita, yaani tarehe 9 Oktoba, raia huko Gaza wamekumbwa na madhila lukuki kutokana na mashambulizi yanayoendeshwa na Israeli.

Hamas na Israeli waendelea kurushiana makombora 

“Katika wiki moja pekee, takribani wapalestina 400 wameuawa huko Gaza na wengine 1,500 wamejeruhiwa,” amesema Bi. Msuya.

Vihoro vimekumba raia baada ya eneo karibu na hospitali ya Al-Aqsa kuteketezwa kwa moto wa makombora, wanawake na watoto wakikumbwa na machungu yatokanayo na majeraha ya moto.

“Mapigano makali ndani na kuzingira kambi ya Jabaliya ambayo imezingirwa, yanaendelea kuripotiwa wakati ambapo makombora yanayorushwa kiholela na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas yakiendelea kuelekezwa Israeli,” amesema Kaimu Mkuu  huyo wa OCHA.

Katika eneo la Jabaliya, watu zaidi ya 55,000 yaripotiwa wamefurushwa kwenye makazi yao tangu mwanzo wa mwezi huu na wengine wamenasa kwenye makazi yao, chakula na maji vikikaribia kuisha.

“Jana watu 13 wa familia moja waliuawa baada ya wafanyakazi wa uokoaji kuzuiwa kufikia majeruhi walionasa kwenye vifusi, watu hao walikuwa wanaita wapatiwe msaada bila mafanikio,”

Mtoto wa Kipalestina ameketi kwenye kitanda cha hospitali katika Hospitali ya Nasser, Khan Yunis, Gaza, huku mwanamke aliyevaa kitambaa kichwani akiwa amemshika mkono.
© UNICEF/Abed Zaqout Mvulana mwenye umri wa miaka 3, ambaye nyumba yake ilishambuliwa kwa bomu, anapata nafuu katika hospitali ya Nasser baada ya kukatwa sehemu ya mguu wake wa kulia.

Wajawazito wanahaha pa kujifungulia

Ikiwa hospitali tatu zimesalia kaskazini mwa Gaza ndio zinazofanya kazi, tena katika kiwango cha chini huduma za damu, tiba ziko mashakani. Kwa wajawazito na akina mama 155,000 wanaonyonyesha huko Gaza hali ni tete.

“Wanawake wanajifungua huku makombora yakiendelea kurindima. Hawana uhakika wa wao au watoto wao kuishi. Huduma baada ya kujifungua hakuna,” amesema Bi. Msuya.

Chanjo imethibitisha umuhimu wa UNRWA

Licha ya makombora, awamu ya pili ya chanjo ilianza Gaza Kati Oktoba 14 na itamalizika Oktoba 17.

Takribani watoto 157,000 wameshapatiwa chanjo, ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 10.

“Kampeni ya chanjo imethibitisha jukumu muhimu la shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA, ambalo watendaji wake walifanikisha utoaji chanjo kwa asilimia 43 ya watoto siku ya kwanza,” amesema Bi. Msuya.

Nini kifanyike sasa

Amekumbusha kuwa kiwango cha machungu Gaza kinashinda uwezo wa maelezo hata kiwango cha kusema.

Kila siku hali inazidi kuwa mbaya Gaza, amesema Bi. Msuya hivyo amesema ukatili Gaza ukome na hili haliwezi kufanyika kwa maneno; lazima kwa vitendo – tena haraka. Tunarejelea wito wa hatua za kidiplomasia miongoni mwa jamii ya kimataifa kuchagiza kumaliza uhasama, kuhakikisha sheria za kimataifa zinaheshimiwa, kufanikisha sitisho la mapigano Gaza na kukubaliana njia sahihi ya kuwa na amani endelevu.

Balozi Amar Bendjama wa Algeria akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama UN kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwemo suala la Palestina.
UN /Eskinder Debebe Mwakilishi wa Kudumu wa Algeria kwenye UN Balozi Bendjama akihutubia Baraza Kuu la UN

Hali Gaza ni maangamizi - Algeria

Mkutano huu uliitishwa na Algeria, ikiungwa mkono na Ufaransa na Uingereza. Akihutubia Baraza Mwakilishi wa Kudumu wa Algeria kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Amar Benjama amesisitiza kuwa hali huko Gaza imefikia kiwango cha maangamizi akitoa wito kwa Israeli kutimiza wajibu wake wa kulinda maisha ya raia kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.

“Inawezekana vipi tunaweza kupatia chanjo hawa watoto, lakini tusiweze kuwapatia chakula?” amehoji wakati huu ambapo awamu ya pili ya chanjo inaendelea, akiongeza kuwa kuwaacha raia na njaa kama mbinu ya vita ni jambo linalopingwa waziwazi – akirelejea “sera iliyopangwa ya Israeli ya kuacha watu na njaa.

Balozi Benjama ametoa pia onyo juu ya rasimu ya sheria iliyoko kwenye Bunge la Israeli, Knesset inayolenga kufuta operesheni za UNRWA.

Balozi wa Ufaransa Nicolas de Rivière akizungumza katika Baraza la Usalama UN jijini New York.
UN /Eskinder Debebe Balozi Nicolas de Rivière, Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa kwenye UN akihutubia Baraza la Usalama la UN

Ufaransa yalenga idadi ya vifo kaskazini mwa Gaza

Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nicolas de Rivière, amelaani mashambulizi ya anga yanayofanywa na Israeli dhidi ya miundombinu ya kiraia Gaza, akisema raia lazima walindwe kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu. Akinukuu vyanzo vya Gaza, amesema tayari kuna takribani vifo 300 na watu 100 wamejeruhiwa katika wiki moja.

“Natoa wito kwa Israeli kuachana na miradi inayolenga kuharamisha shughuli za UNRWA. Hii itafanya hali ya kibinadamu ambayo tayari ni zahma, iwe mbaya zaidi.”

Sera ya kushindisha watu na njaa ni ukatili na haikubaliki- Marekani

Mwakilishi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Linda Thomas-Greenfield akamulika sera ya kushindisha watu na njaa huku akielezea wasiwasi wake kuhusu taswira ya kutisha ya vifo na majeruhi miongoni mwa raia huko katikati mwa Gaza kufuatia shambulio la angani lililofanywa na Israeli.

Balozi Linda Thomas-Greenfield wa Marekani akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwemo suala la Palestina.
UN /Eskinder Debebe Balozi Linda Thomas-Greenfield, Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye UN akihutubia Baraza la Usalama la UN New York, Markekani

Ametoa wito wa sitisho la mapigano Gaza akiongeza kuwa será ya kushindisha njaa haitakubalika. “Israeli imesisitiza kuwa vyakula na vifaa vingine muhimu vitaingia Gaza. Lakini tutafuatilia kuona vitendo vya Israeli ili viendane na kauli yake.”

Ameangazia juhudi za kidiplomasia za Marekani zilizofanikisha kufunguliwa kwa kivuko cha Erez na kwamba Israeli imeahidi kufunguliwa kwa kivuko kingine ili kupitisha misaada.

“Hata hivyo kiwango cha ufikishaji wa chakula hakitoshelezi. Vyakula na vifaa vingine lazima vifikishwe kwa haraka Gaza.”

‘Hakuna kanuni ambayo Israeli haijavunja’: Palestina

Balozi Riyad Mansour anayewakilisha Palestina akihutubia Baraza amelaani vitendo vya Israeli akisema ni mifumo ya ukiukaji wa sheria ya kimataifa.

Riyad Mansour, Mchunguzi wa Kudumu wa Nchi ya Palestina kwa UMOJA WA MATAIFA, akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama mjini New York.
UN /Eskinder Debebe

Wapaletsina 400,000 huko kaskazini mwa Gaza wamekumbwa na mabomu, njaa na ukosefu wa misaada ya kibinadamu na wanalazimishwa kuchagua kati ya kubakia na kufa au kuondoka na kukabiliwa na kifo kwingineko.

“Hiyo si vita,” ameongeza. “Huu ni uhalifu. Lazima vikomeshwe. Na lazima vikomeshwe sasa.”

Balozi Mansour ameangazia mashambulizi ya Israeli dhidi ya UNRWA na kwamba ni mpango wa kufanya Gaza pawe pahala ambako watu hawawezi kuishi. Ameainisha hali ya sasa kama “mauaji ya halaiki yaliyopangwa kufanyika kimya kimya.”

Ameiambia  jamii ya kimataifa kuwa kuwa kimya na kutochukua hatua haikubaliki.

Ameonya kuwa kinachoendelea sio tu kinatishia maisha ya wapalestina, bali pia utulivu kwenye ukanda wa MAshariki ya Kati.

Hamas inatumia misaada kuimarisha mfumo wake wa kigaidi

Danny Danon, Mwakilishi wa Kudumu wa Israeli kwenye Umoja wa Mataia alianza hotuba yake kwa kusema kwamba siku 376 zimepita tangu “mauaji makubwa ya wayahudi zaidi ya wayahudi baada ya yale ya halaiki”, huku watu 101 bado wanashikiliwa mateka na Hamas  huko Gaza.

Danny Danon, Mwakilishi wa Kudumu wa Israel katika UMOJA WA MATAIFA, akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama mjini New York.
UN /Evan Schneider

“Leo tunajadili hali ya kibinadamu Gaza, huku raia wa Israeli wanalengwa kila siku na wale wanaosaka kutumaliza,” amesema Balozi Danon.

Ameliambia Baraza kuwa wakati Israeli inakabiliana “na kitisho kinachoendelea Gaza, sambamba na maeneo mengine sita ambako tunaendelea kushambuliwa, juhudi zetu za kibinadamu zinasalia za kina kuliko wakati wowote.”

Ametaja jitihada hizo kuwa ni hatua ya hivi karibuni ya mafanikio ya kusafirisha wagonjwa kutoka hospitali moja Jabalya kwenda eneo lingine, hatua iliyofanikishwa kwa uratibu na shirika la Msalaba Mwekundu na Umoja wa Mataifa.

“Tumejizatiti kufanikisha misaada ya kibinadamu, hasa kwenye sekta ya matibabu, licha ya juhudi za Hamas kujijumuisha wenyewe kama wahudumu wa afya na wagonjwa,” amesema.

Balozi Danon amesisitiza kuwa suala la Gaza si ukosefu wa misaada, bali Hamas imeteka misaada kwa manufaa yake.

“Wanaiba, wanahifadhi, na hata kuuza misaada inayolenga raia wa Gaza, na kugeuza misaada ya kibinadamu kuwa fursa yao ya kujinufaisha.”