Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kambi ya huduma za macho ya UNICEF yawezesha watoto akiwemo Candy kuona vema

Mtoto mwenye umri wa miaka 7 mwenye ulemavu wa ngozi, anayeitwa Candy, ameketi kwenye hafla nchini Kenya kwa ajili ya watoto wenye ulemavu, kama sehemu ya mpango wa UNICEF . Amevaa gauni la beige na kahawia na miwani ya jua, huku wanaume wawili wakiwa wamesimama kando yake.
UNICEF Kenya Candy, mtoto mwenye umri wa miaka 7 nchini Kenya ambaye ana ualbino.

Kambi ya huduma za macho ya UNICEF yawezesha watoto akiwemo Candy kuona vema

Afya

Nchini Kenya, Idara ya Taifa ya Ulinzi wa Jamii kwa kushirikiana na Baraza la Kitaifa la watu wenye ulemavu na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF, wameendesha kambi ya kusaidia uoni kwa watu wenye changamoto.  Mmoja wa wanufaika wa juhudi hii ni Candy, msichan wa  mwenye umri wa miaka 7 ambaye ana ualbino.

Akiwa mwingi wa matumaini, Eric Odhiambo Okeyo, baba mzazi wa mtotohuyo alimpeleka kwenye kambi hiyo  jijini Kisumu ambapo alifanyiwa uchunguzi na matibabu.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi, Candy alielekezwa kwa daktari wa macho  ili abaini aina ya miwani ambayo ingemfaa.

“Mtoto alipoanza shule niligundua kwamba mwendo wake katika masomo ulikuwa wa polepole sana na pia alikuwa analamika kwamba haoni anachoandika mwalimu. Hata akienda kucheza  niliona kwamba alikuwa akifunga macho mara kadhaa. Ilikuwa inanikosesha amani kwa sababu nilihisi kuwa alikuwa akiteseka,” amesema Eric.

Mpango huu wa kielelezo wa UNICEF na wadau wake unashughulikia changamoto zinazowazuia watoto wenye ulemavu na familia zao kupokea msaada muhimu wanaohitaji wakati wa majanga na dharura.

Msichana mdogo wa Kiafrika mwenye ualbino na miwani ya jua amesimama nje kwenye nyasi, akimkabili mwanamume anayeashiria kwa mkono wake.
UNICEF Kenya Candy, Mtoto mwenye umri wa miaka 7 nchini Kenya ambaye ana ualbino.

Akiwa mwingi wa furaha, Eric anasema, “imechukua muda wa miaka sita ambapo nimekuwa nikizunguka tu kuhusu miwani. Mahali nilipoenda hapo awali, niliambiwa kulipia shilingi elfu arobaini ($313) lakini sikuweza kupata hiyo pesa. Nimefurahi kwamba leo nimepewa bila gharama yoyote.”

Baada ya uchunguzi na mawaidha mbalimbali katika hii kambi, Eric na mwanaye Candy hawakuweza kuificha furaha yao kwa kupata suluhisho la tatizo ambalo limewaathiri kwa miaka sita.

Hatimaye, Candy alipewa miwani yake maalum ili kumsaidia kuona vizuri zaidi.

“Nimefurahia sana sina jukumu tena la  kutafuta pesa za kununua miwani. Na nimefurahi pia mtoto wangu atakuwa na wakati rahisi. Amefurahia kabisa na anaipenda sana miwani yake. Amesema anajihisi vizuri. Kwa sababu ana miwani, natumaini anaweza kucheza bila shida yoyote, bila kujali kuhusu jua kwa sababu miwani inamkinga.”