Siku ya chakula duniani, ilhali mamilioni hawana chakula mezani - FAO
Siku ya chakula duniani, ilhali mamilioni hawana chakula mezani - FAO
Leo ni siku ya chakula duniani ambako huko Roma, Italia makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, kumefanyika tukio maalum la kuadhimisha siku hiyo, washiriki wakisisitiza umuhimu wa kila mtu duniani kupata chakula bora, cha kutosha, salama na kwa bei nafuu.
Maadhimisho yamefanyika wakati kukiwa na mivutano na mizozo duniani, sambamba na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, mambo ambayo yanachochea mamilion iya watu duniani kote kukumbwa na njaa huku mabilioni wengine wakiwa hawana uwezo wa kupata lishe bora.
Ujumbe wa Mkurugenzi Mkuu wa FAO
Akifungua maadhimisho hayo, Mkurugenzi mkuu wa FAO, QU Dongyu amesema maudhui ya siku hii mwaka huu ambayo ni Haki ya Chakula Kwa Maisha Bora na Mustakabali Bora, yamekuja wakati muhimu kukumbusha kwamba watu wote wana haki ya kupata chakula cha kutosha.
“Natoa wito kwa ahadi mpya ya kujenga mifumo ya kilimo cha mazao ya chakula iliyo fanisi, jumuishi, yenye mnepo na endelevu zaidi itakayowezesha kulisha vema dunia.”
Qyu amesema mifumo ya aina hiyo inatakiwa kusaidia wakulima wadogo, wakulima wa kaya na wafanyabiashara wadogo kwenye mnyororo wa thamani ambao katika nchi nyingi ndio msingi wa kuwezesha kuzalisha vyakula tofauti tofauti vyenye lishe na kuwezesha vipatikane na viwafikie watu, na wakati huo huo wakihifadhi tamaduni za asili za vyakula.
Watu milioni 730 wakikabiliwa na njaa duniani kote na wengine zaidi ya bilioni 2.8 wanashindwa kupata lishe bora, “hatuna wakati wa kupoteza, na lazima tuchukue hatua,” amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO.
Ujumbe wa Guterres
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia video amesema, "kuna kitu hakiko sawa katika ulimwengu ambao njaa na utapiamlo ni ukweli wa maisha kwa mabilioni ya watoto, wanawake na wanaume." Akasema ulimwengu usio na njaa unawezekana, lakini "mifumo ya chakula inahitaji mabadiliko makubwa," ili kuwa na ufanisi zaidi, ujumuishi, mnepo na endelevu.
Naibu Mkuu wa IFAD na uwekezaji vijijini
Gérardine Mukeshimana, Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ametoa wito wa "uwekezaji wa haraka, wa pamoja na thabiti kwa wakulima maskini wa vijijini kutambua kwa ngazi ya chini kabisa haki yao ya msingi ya chakula chenye lishe." Akabainisha kuwa wakulima wadogo wanazalisha karibu nusu ya chakula cha dunia, ingawa pia wanakabiliwa na njaa na umaskini.
Balozi Mwema Maalum wa FAO
Mfalme Letsie III wa Lesotho, ambaye ni Balozi Mwema Maalum wa FAO katika upande wa lishe anaeleza anavyoiunga mkono FAO kwa “kujaribu kuwa mtetezi mwaminifu na mwenye kujitolea katika masuala ya lishe, katika masuala ya uhakika wa chakula.” Anasema, “na mara kwa mara, mimi hutembelea sehemu nyingine za bara la Afrika nikivaa kofia yangu ya FAO, hasa kuhimiza serikali na viongozi kama bara kuwekeza zaidi katika masuala ya lishe na masuala ya uhakika wa chakula.”