Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO Tanzania yapatia walimu maarifa ya kilimo ili kuboresha lishe shuleni

Meza inaonyesha vyakula mbalimbali vyenye afya vilivyotayarishwa, ikiwa ni pamoja na mishikaki ya matunda na mboga, sahani zilizopikwa, na matunda mapya, wakati wa kipindi cha mafunzo huko Kigoma, Tanzania.
FAO Tanzania Chakula chenye lishe bora ambacho kimeandaliwa katika mafunzo yanayotolewa na FAO Tanzania, sehemu ya programu inayolenga kuzalisha chakula chenye virutubisho muhimu na maandalizi ya mlo bora.

FAO Tanzania yapatia walimu maarifa ya kilimo ili kuboresha lishe shuleni

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kabla ya mradi huu kuja walimu shuleni pamoja na wanafunzi walikuwa wanalima kwa mbinu zao za kawaida za asili ikiwemo kuweka mbolea, lakini unakuta hata kuvuna walikuwa hawavuni kama inavyopaswa, ni kauli ya mnufaika wa mafunzo ya kilimo bora shuleni yaliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO nchini Tanzania.

Emile Mfamwo, mwalimu na pia Afisa Elimu, Taalum wilaya ya Buhigwe, mkoa wa Kigoma, ulioko kaskazini-magharibi mwa Tanzania alikuwa anazungumzia mafunzo hayo yaliyotolewa kwa walimu kwa ushirikiano kati ya FAO na shirika la Uchumi na Maendelo ya Jamii Vijijini (RECODA) chini ya utekelezaji wa  Programu ya Pamoja ya  Kigoma, KJP, awamu ya pili ndani ya Halmashauri ya Buhigwe .

Mradi ni kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi wa shule za msingi tano kuhusu mbinu bora za uzalishaji wa mazao yenye lishe katika wilaya hiyo ya Buhigwe kwa kushughulikia changamoto kubwa zinazotokana na kutokuwepo kwa programu ya lishe shuleni.

Asilimia 36.5 ya wanafunzi wa S/M Kigoma ndio wanapata mlo shuleni

Hawamu Bakari Tambwe  ni Afisa elimu Taaluma mkoa wa Kigoma akizungumza kuhusu hali ya lishe kwa wanafunzi Kigoma anasema, “mkoa wa Kigoma una shule za msingi 702, wanafunzi 665,753na wanafunzi wanaopata chakula ni 240,007, sawa na asilimia na asilimia 36.5.”

Akasema kutokupata chakula shuleni kuna changamoto nyingi ikiwemo mahudhurio ya watoto shuleni kutokuwa mazuri, uelewa wa watoto darasani kutokuwa mzuri, taaluma  taaluma kushuka, mtoto kuzubaa darasani na kutokuwa mchangamfu.

Hivyo akasema mafunzo haya yataleta faida kwani shule zitakuwa na bustani za mazao ya mboga mboga, mahindi, viazi lishe, maharage lishe na ufugaji wa kuku, bata na hata sungura kwa ajili ya watoto shuleni. “Hii itasaidia sana kuongeza taaluma katika shule hizi, na hatimaye taaluma katika wilaya ya Buhigwe na mkoa kwa ujumla.”

Wanafunzi katika Shule ya Msingi ya Buhigwe huko Kigoma, Tanzania, wanapata mafunzo ya kilimo cha bustani kama sehemu ya mpango wa lishe FAO .
FAO Tanzania Wanafunzi wa shule ya msingi ya Buhigwe iliyoko Kigoma nchini Tanzania wakipatiwa mafunzo ya kilimo cha bustani na mbinu bora za uzalishaji wa mazao yenye lishe.

Mradi utanufaisha shule nyingi zaidi Kigoma

Mkuu Idara ya Kilimo, Mifugona Uvuvi wilaya ya Buhigwe Alphonce Haule akaweka bayana kuwa ni shule chache katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ndio zinatoa huduma ya chakula shuleni na pia wanajihusisha sana na kilimo cha mazao yanayoweza kusaidia wanafunzi kupata lishe shuleni.

“Matarajio yetu ni kwamba katika utekelezaji wa mradi huu, baada ya shule hizi 5 za awali kuanza kulisha watoto shuleni, tunataraji kuwa shule nyingine zitajifunza kama ambavyo wito umetolewa kwenye mafunzo haya.”

Bwana Haule anasema ni imani  yake kuwa kiwango cha lishe shuleni ambacho kiko chini sana katika halmashauri ya Buhigwe kitaongezeka.

Kilimo cha mazoea sasa kwaheri!

Mwl Emile akatolea mfano hali ilivyokuwa kabla ya mafunzo akitaja shule ya msingi ya Kilelema ambayo anasema, “mwaka jana walilima ekari tatu lakini pale wamevuna magunia manne. Lakini kwa sasa wanafunzi 50 kutoka kila shule 5 ambao watahusika katika kupanga na kutunza mifugo waliyopewa na pia watapewa kuku wa kwenda kufunga nyumbani kwao. Tunaamini kuwa kule nyumbani kwao watawajengea uwezo wazazi wao ambao wengi hawajasoma.”

Anasema hatua hiyo itakuwa na faida kwenye jamii kwani walizoea kula kimazoea, lakini sasa ni vyakula vyenye virutubisho kama vile madini ya chuma na zinki, hivyo wazazi nao wataeleza mbinu hizo kwa wenzao.

Mafunzo yatahusisha mbinu kuhusu bora za kilimo cha mahindi ya ProvitA, maharagwe yaliyoimarishwa na madini chuma na zinki, viazi vitamu vyenye lishe na mboga mbalimbali na matunda.

FAO inasema hatimaye mafunzo yataongeza maarifa ya kilimo, kuongeza uzalishaji chakula, kukuza ushirikishwaji wa jamii na kuboresha upatikanbaji wa lishe bora kwa wanafunzi.