Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muhtasari wa habari - Chanjo ya polio Gaza, Janga la njaa Afrika, Utaifa

Mfanyakazi wa afya UNICEF akimpa mtoto mdogo chanjo ya polio aliyelala mezani katika kituo cha chanjo huko Gaza.
UN News/Ziad Taleb Awamu ya pili ya chanjo ya polio katika ukanda wa Gaza ulianza Deir El Balah, central Gaza.

Muhtasari wa habari - Chanjo ya polio Gaza, Janga la njaa Afrika, Utaifa

Afya

Licha ya mashambulizi, awamu ya pili ya chanjo kwa watoto dhidi ya polio huko Gaza iliyoanza jana imeendelea leo Jumanne eneo la kati mwa Gaza na hadi sasa watoto wapatao Elfu 93 wenye umri wa chini ya miaka 10 wameshapatiwa dozi ya pili.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA Philippe Lazzarini kupitia mtandao wa X amesema hatuwezi kupatia watoto chanjo chini ya anga lililosheheni mabomu, pande zote zizingatie makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano.

Janga la nja Afrika

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP hii leo linatoa wito wa msaada wa dharura kuepusha janga la kibinamu eneo la kusini mwa Afrika kutokana na ukame uliochochewa na El- Niño.

Msemaji wa WFP Tomson Phiri [PIRI] amewaambia waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi hii leo kuwa watoto milioni 21 wana utapiamlo kwenye eneo hilo. Kwa jamii nyingi hii, hili ni janga baya zaidi la chakula katika miongo kadhaa. Oktoba ni mwanzo wa msimu wa mwambo na kila mwezi unatarajiwa kuwa na hali mbaya zaidi kuliko uliotangulia hadi msimu wa mavuno Machi na Aprili mwakani.

Utaifa

Na ubia mpya wa kutokomeza watu kukosa utaifa umezinduliwa huko Geneva, Uswisi ukilenga kutokomeza hadhi hiyo inayoathiri mamilioni ya watu duniani. Zaidi ya nchi 100, mashirika ya kiraia, taasisi zinazopigia chepuo kuondokana na hadhi hiyo, wanazuoni na wadau wengine wameanzisha ubia huo ikiwa ni kuendeleza kampeni ya muongo mmoja iliyopatiwa jina Mimi ni wa! au I Belong.