Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya kibinadamu ya UN yaonya juu ya kutokuwa na dalili ya kuisha zahma Gaza Kaskazini

Mwonekano wa angani wa kambi kubwa ya wakimbizi yenye makazi na mahema mengi ya muda huko Gaza.
© UNICEF/UNDP/Abed Zagout Wapalestina waliokimbia makazi yao wanaendelea kuishi kwenye mahema huko Gaza.

Mashirika ya kibinadamu ya UN yaonya juu ya kutokuwa na dalili ya kuisha zahma Gaza Kaskazini

Amani na Usalama

Matarajio ya vita kamili nchini Lebanon yanaonekana kutopungua leo huku mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, akisema kuwa hakuna dalili ya "mwisho wa hali ya kuzimu kaskazini mwa Gaza, ambako misaada ya kuokoa maisha imezimwa.”

Onyo hilo kutoka kwa Philippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa UNRWA limechochewa na amri mpya za kuondoka kutoka kwa jeshi la Israeli, ambalo "wengi wanalikataa kwa sababu wanajua vyema kwamba hakuna sehemu yoyote katika Ukanda wa Gaza iliyo salama".

Haya yanajiri huku kukiwa na ripoti za mamlaka za mitaa zikieleza mashambulizi makali ya Israel kaskazini mwa eneo lililosambaratishwa ambako operesheni za ardhini pia zinaendelea.

Kambi ya wakimbizi ya Jabalia imezingirwa, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema mwishoni mwa juma, kabla ya kutoa maagizo ya watu kuhama jana Jumanne.

Mwanamume wa Mashariki ya Kati mwenye ndevu, amevaa shati jeusi la polo, amesimama kwenye uwanja wa vifusi na anaelekeza majengo yaliyoharibika katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia huko Gaza.
© UNOCHA Ahmed Abu Aita akionyesha ishara kuelekea kwenye nyumba yake kaskazini mwa Gaza ambayo imesalia vifusi baada ya kuharibiwa na makombora.

Mashambulizi yanaendelea

Kamishina huyo mkuu wa UNRWA amesema mashambulizi pia yamemeripotiwa katika miji ya Beit Lahia na Beit Hanoun, kaskazini mashariki mwa Gaza, huku barabara pia zikiwa zimefungwa.

"Operesheni za kijeshi zilizoimarishwa kaskazini mwa Gaza zinatulazimisha kuzima huduma za kuokoa maisha," amesema Bwana Lazzarini leo kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Ameongeza kuwa shule saba kati ya shule zilizogeuzwa za shirika la Umoja wa Mataifa kuwa makazi ya muda ya wakimbizi wa ndani zinahamishwa, wakati visima viwili tu kati ya vinane vya maji katika kambi ya Jabalia ndivyo bado vinafanya kazi.

Pia amesema takriban watu 400,000 wanaaminika kusalia kaskazini mwa Gaza.

"Watoto ndio, kama ilivyokuwa zamani, ndio wa kwanza na wengi kuteseka," amesema mkuu huyo wa UNRWA akiongeza kuwa “njaa inazidi kuenea na kuongezeka tena kwa sababu ni kama hakuna vifaa vya huduma za msingi vinavyopatikana.”

Kwa mujibu wa mamlaka za afya za eneo la Gaza, takriban watu 45 wameuawa na 130 kujeruhiwa katika muda wa saa 24 zilizopita.

Tangu mashambulio ya kigaidi yanayoongozwa na Hamas katika maeneo mengi ya Israel na kusababisha vifo vya watu 1,250 na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka, Oktoba 7 mwaka jana idadi ya watu waliouawa Gaza imeripotiwa kufikia takriban watu 42,000, wengine 97,700 wamejeruhiwa, na mara nyingi ni majeraha ya kubadilisha maisha.

Majengo na vifusi viliharibiwa katika vitongoji vya Kusini mwa Beirut baada ya mashambulizi ya anga, huku moshi ukipanda nyuma na watu kwenye skuta mbele.
© UNICEF/Dar al Mussawir/Ramzi Haidar Vitongoji vya kusini mwa Beirut viko magofu kufuatia mashambulizi ya anga.

Hali si hali Lebanon

Huko Lebanon, wakati huohuo, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, imeripoti mashambulizi yasiyokoma na ya kuongezeka katika maeneo ambayo hayakuathiriwa hapo awali, huku kukiwa na mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel kutoka kwa Hezbollah.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo OCHA imesema "Katika siku moja pekee ya 6 Oktoba  zaidi ya mashambulizi 30 ya anga yalipiga vitongoji vya kusini mwa Beirut na maeneo ya jirani, na kuwatia hofu wakazi na kulazimisha watu wengine kukimbia kutoka maeneo yenye wakazi wengi, ikiwa ni pamoja na kambi ya wakimbizi ya Palestina ya Shatila," OCHA ilisema katika taarifa yake iliyochapishwa leo.

Takwimu za hivi karibuni kutoka kwa wizara ya afya zinaonyesha zaidi ya vifo 2,083 vya pamoja na majeruhi 9,869 tangu tarehe 8 Oktoba 2023, wakati mashambulizi ya roketi ya Hezbollah yalipoongezeka kaskazini mwa Israeli wakati na vita huko Gaza vilipozuka.

Majeruhi wengi zaidi nchini Lebanon wametokea katika muda wa wiki mbili zilizopita, huku kukiwa na mashambulizi makali ya Israel na mashambulizi ya ardhini kusini mwa Lebanon.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR, asilimia 25 ya maeneo ya Lebanon yameathiriwa na amri za jeshi la Israel za watu kuyahama makazi yao.

Amri za kuhama hutolewa "kila siku kwa zaidi ya vijiji 100 na vitongoji vya mijini kote kusini mwa Lebanon, na kulazimisha watu kukimbia na kusukuma watu wengi hadi kilomita 30 kaskazini kwa nchi hiyo.

Mwanamume amebeba godoro kubwa kama sehemu ya usambazaji wa misaada UNICEF kwa familia zilizopoteza makazi katika Chuo Kikuu cha Lebanon huko Beirut.
© UNICEF/Fouad Choufany Vifaa vya dharura vinasambazwa kwa familia zilizohamishwa nchini Lebanon.

Watu wengi wametawanywa

OCHA imeripoti kuwa kwa jumla, takriban watu milioni 1.2 sasa ni wakimbizi wa ndani, huku watu 180,700 wakitafuta hifadhi katika makazi 978, 775 ambapo miongoni mwake tayari yamejaa kufikiauwezo wake kamili.

Vurugu hizo pia zimechelewesha kuanza kwa mwaka wa shule, wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limesema kuwa takriban watoto 350,000 wameyakimbia makazi yao.

"Madhara makubwa ya raia yanatokea kutokana na silaha za milipuko katika maeneo yenye wakazi wengi na amri za kulazimishwa kuwahama makazi yao," OCHA imebainisha kuwa "Hatua za haraka ni muhimu ili kuwalinda raia dhidi ya kuongezeka kwa ghasia na kuhakikisha kwamba wahudumu wa kibinadamu na wa misaada wanaweza kutoa msaada muhimu kwa usalama."