UNHCR yatoa wito wa msaada zaidi kwa wakimbizi wanaokimbia mashambulizi nchini Lebanon
UNHCR yatoa wito wa msaada zaidi kwa wakimbizi wanaokimbia mashambulizi nchini Lebanon
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) linatoa wito wa msaada wa haraka kwa watu 250,000 waliokimbia mashambulizi ya anga nchini Lebanon na kuvuka mpaka kuingia Syria. Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi, anahitimisha ziara yake ya dharura nchini Syria huku akisisitiza hitaji la msaada kwa wakimbizi wapya na jamii zinazowahifadhi.
Grandi ametembelea kituo cha mpakani cha Jdeidet Yabous, ambako amekutana na wakimbizi wa Lebanon na raia wa Syria wanaokimbia mashambulizi makali ya anga ya Israeli. "Familia ninazozungumza nazo zinakimbia kuokoa maisha yao na zinahitaji msaada wa haraka," amesema Grandi, huku akielezea wasiwasi wake kuhusu hatari inayowakumba wakimbizi hao wanapovuka kwa miguu kutokana na uharibifu wa barabara kuu unaosababishwa na mashambulizi ya anga.
UNHCR, kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Syria na mashirika mengine ya kimataifa, inatoa msaada mpakani ikiwemo maji, chakula, na vifaa vya kujikinga na baridi. Timu zinasaidia pia wakimbizi kwa kuwapa usaidizi wa kisheria na ushauri wa kiutawala.
"Wimbi hili jipya la wakimbizi linaongeza changamoto wakati ambapo mamilioni ya Wasyria tayari wanahitaji msaada wa kibinadamu," anasisitiza Grandi, akibainisha umuhimu wa kuimarisha msaada wa kimataifa kwa jamii zinazowapokea wakimbizi hao.
Akiwa Damascus, Grandi amezindua ombi la dharura la dola milioni 324 kwa ajili ya kusaidia wakimbizi wapya kwa kipindi cha miezi sita, huku akihimiza msaada wa muda mfupi na mrefu kwa jamii zinazowahifadhi.
Grandi pia amekutana na Rais Bashar al-Assad pamoja na maafisa wa serikali kujadili usalama wa wakimbizi wanaoingia Syria na ushirikiano wa kimataifa katika kuwalinda.
"Natoa shukrani kwa serikali kwa kuweka mipaka wazi na kuhakikisha usalama wa wakimbizi," amesema Grandi.
UNHCR inaendelea kupanua programu zake za kibinadamu nchini Syria ili kutoa msaada wa haraka kwa wakimbizi wapya na kuhakikisha wanapata huduma muhimu wanapowasili.