Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana mna fursa ya kujenga mustakbali bora wa miji yetu: UN

Makazi yasiyo rasmi ya Korali mjini Dhaka nchini Bangladesh
© UN-Habitat/Kirsten Milhahn
Makazi yasiyo rasmi ya Korali mjini Dhaka nchini Bangladesh

Vijana mna fursa ya kujenga mustakbali bora wa miji yetu: UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya makazi duniani Umoja wa Mataifa umesema vijana wana fursa kubwa ya kuchangia katika kujenga mustakbali bora wa miji ya dunia.

Kupitia ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Katika Siku ya Makazi Duniani, tunathibitisha tena haki ya msingi ya makazi na kutafakari kuhusu mabadiliko ya mazingira ya mijini.”
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Ushirikishwaji wa vijana katika kujenga mustakbali bora wa miji” ikiaangazia jukumu muhimu la vijana katika kujenga mustakabali bora wa mijini.
Katibu Mkuu amesema “Ifikapo mwaka wa 2030, asilimia 60 ya wakazi wa mijini watakuwa chini ya umri wa miaka 18 na kadiri miji inavyoendelea kukua, ndivyo pia fursa ya kutumia nguvu za vijana kugeuza changamoto za miji kuwa fursa ianapanuka.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

Vijana ni muhimu kujenga mustakbali ulio sawa

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameendelea kusema kwamba kama vile Mkutano wa Mwezi uliopita wa Zama Zijazo ulivyowekwa bayana “vijana ni muhimu katika kujenga mustakabali ulio sawa na endelevu. Kutumia uwezo huo kikamilifu kunahitaji kuwekeza katika elimu, kupanua ujuzi wa kidijitali, kukuza ujasiriamali na kukuza mipango inayoongozwa na vijana kuhusu mabadiliko ya tabianchi, makazi ya gharama nafuu na watu kuhama makwao”.
Guterres amesisitiza kuwa haya yote na mengine ni muhimu katika kuunda miji iliyochangamka, iliyojumuishi na thabiti na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs.
Amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba “Tunapoadhimisha Siku ya Makazi Duniani, tuwaunge mkono vijana kila mahali, tujumuishe vijana katika kufanya maamuzi, na tujenge miji ambayo watu wa rika zote wanaweza kustawi.”
Mkurugenzi mtendaji wa UN-HABITAT Anacláudia Rossbach
UN Photo/Mark Garten
Mkurugenzi mtendaji wa UN-HABITAT Anacláudia Rossbach

Mwaka huu tunawasherehekea nyinyi vijana tumaini letu

Naye Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la makazi duniani UN-HABITAT Anacláudia Rossbach katika ujumbe wake amesema “Siku hii ya Makazi Duniani, tunasherehekea ninyi vijana, mashujaa, na waleta amabadiliko wa leo na kesho. Nyinyi ndiye mapigo ya moyo waa miji yetu, nguvu inayotusukuma kuelekea mustakbali bora. Kama kizazi cha Wakuzaji watoto na Kizazi cha X, pitisheni kijiti, tunahitaji vizazi vya milenia na Gen Z ili kuinua na kuunda ulimwengu wetu.”
Bi. Rossbach ameendelea kusema kwamba Siku ya Makazi Duniani ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kutafakari hali ya miji na makazi ya watu na haki ya makazi ya kutosha. Lakini leo, tunakualika sio tu kutafakari, lakini kuchukua hatua.
Amesisitiza kuwa “Kaulimbiu ya mwaka huu, inatoa wito kwa vijana kuongoza njia katika kuunda ulimwengu unaoakisi ndoto zetu za pamoja.”
Mkuu huyo wa UN-HABITAT ameongeza kuwa makazi ya kutosha na ya usawa sio tu haki bali ni  lazima iwe ukweli halisi kwa wote.
“Tunaishi katika wakati wa migogoro mingi, makazi, vita, na janga la mabadiliko ya tabianchi. Watu bilioni moja wanahangaika katika vitongoji duni, na zaidi ya milioni 300 wanakabiliwa na ukweli usiovumilika wa ukosefu wa makao. “
Makazi ya Ciudad Bolivar kusini mwa Bogota Colombia
© UN-Habitat/Hector Bayona
Makazi ya Ciudad Bolivar kusini mwa Bogota Colombia

Hizi sio takwimu tu ni hali halisi

Bi. Rossbach amesisitiza kwamba “Hizi sio takwimu tu  ni familia changa, marafiki zako, na wenzako wanaoto wito wa usalama, utu na matumaini.”
Kwani amesema mipango endelevu ya miji na makazi ndio moyo wa mapambano yetu ya mustakabali bora wa mijini. Nyumba ni msingi wa maendeleo endelevu inaathiri kila kitu kuanzia katika kupunguza umaskini na usawa wa kijinsia hadi hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.”
Amemalizia kwa kusema  kwamba mipango endelevu ya miji “inawapa nguvu nyinyi vijana, kujenga mustakbali unayostahili. Katika Siku hii ya Makazi Duniani, tunakualika ushirikiane nasi ili kutafuta suluhu na kuhakikisha kwamba haki ya makazi na miji na jumuiya endelevu si ndoto bali ni ukweli wetu.”
TAGS: UN-HABITAT, UN Days, vijana, SDGs