Ukeketaji wa wanawake unasababisha vifo wakati wa kujifungua, janga linaloweza kuzuilika: Jamii Uganda
Ukeketaji wa wanawake unasababisha vifo wakati wa kujifungua, janga linaloweza kuzuilika: Jamii Uganda
Josephine Telo, ambaye alipoteza dada yake katika Wilaya ya Amudat, Uganda, aliliambia kundi la wanawake waliopona baada ukeketaji kwamba, "dada yangu hakupaswa kufariki jinsi alivyofariki. Hii ilikuwa ni desturi." Anaongeza, akimaanisha ukeketaji wa sehemu za siri za mwanamke au msichana bila sababu za kiafya, uliosababisha kifo cha dada yake.
Bi. Telo na dada yake, Napala Nangiro, wanatoka wilaya ya Amudat nchini Uganda, nchi ambayo ukeketaji wa wanawake umekatazwa tangu mwaka 2010 na ambapo matukio ya desturi hii yamekuwa yakipungua.
Kufikia mwaka 2022, takriban asilimia 0.2 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 walikuwa wamekeketwa, kwa mujibu wa tafiti, lakini kulikuwa na tofauti kubwa ndani ya nchi. Uwepo wa ukeketaji wa wanawake katika maeneo ya Karamoja na Sebei, kwa mfano, ulikadiriwa mwaka 2016 kuwa ni asilimia 8 kati ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.
Hata hivyo, kwa Bi. Nangiro, kulikuwa na sababu ndogo ya kuwa na wasiwasi kuhusu ukeketaji wa wanawake. Katika jamii yake, ambayo ni sehemu ya kikundi cha kabila la Karamojong, desturi hiyo haifanyiki. Na alipoolewa na mumewe Ikomol, ambaye anatoka kwenye kabila linalofanya ukeketaji, hakuwa na hamu ya kumwekea desturi hiyo.
Lakini bila ya vijana hao wawili kujua, mama ya Ikomol alikuwa na mawazo mengine.
Kudanganywa wakati wa uchungu wa kujifungua
Bi. Nangiro alijifungua muda mfupi baada ya kuolewa, akiwa na umri wa miaka 18. “Mama mkwe wake alikuwa wa msaada mkubwa na alihusika sana wakati wa ujauzito,” Bi. Telo anasimulia. Hali hiyo ilibadilika ghafla alipokuwa kwenye uchungu wa kujifungua.
Bi. Telo anaelezea kwamba dada yake alikwenda katika Kituo cha Afya cha Loroo III, akiandamana na mama mkwe wake, asubuhi ambayo uchungu wake ulianza. Baada ya uchunguzi, wafanyakazi wa afya waliwaelekeza warudi nyumbani na kurejea baada ya masaa kadhaa, wakati uchungu huo utakapokuwa umeongezeka kidogo.
Lakini badala ya kurudi nyumbani, mama mkwe alipendekeza waende kupumzika nyumbani kwa rafiki aliyekuwa jirani. Bi. Nangiro hakuwaza kwamba rafiki huyu, mzee ambaye alikuwa msaidizi wa jadi wa kujifungua, pia alikuwa mtaalamu wa ukeketaji wa wanawake.
“Baada ya kipindi fulani, Nangiro alianza kujihisi wasiwasi kutokana na muda kusonga sana,” Bi. Telo anaelezea. “Alisisitiza umuhimu wa kurudi kwenye kituo cha afya.”
Lakini mama mkwe alisema hakukuwepo na haja ya kurudi kwenye kituo cha afya; alimwambia kwamba badala yake, mzee huyo angeweza kusaidia katika kujifungua.
Kudhulumiwa na kuachwa
Bi. Nangiro aliteseka kwa uchungu kwa masaa mengi usiku huo.
Wakati wa alikuwa kwenye uchungu mkali, mzee huyo alifanya aina ya ukeketaji wa wanawake inayojulikana kama excision, inayohusisha kuondolewa kwa klitoris na labia za ndani.
“Nangiro hakuwa na habari kuhusu kitendo hicho,” Bi. Telo anasema. “Alidhani kwa makosa kwamba mwanamke huyo alikuwa akimsaidia katika kujifungua.”
Lakini wakati Bi. Nangiro alianza kuvuja damu nyingi, mzee huyo alikimbia.
Alipogundua binti-mkwe wake angeweza kufa kwa kuvuja damu, mama mkwe alimuacha Bi. Nangiro peke yake ili kutafuta familia ya binti huyo.
“Dada yangu aliachwa kupigania maisha yake, kwani hapakuwa na mtu aliyepatikana kumkimbiza hospitalini,” Bi. Telo anasema.
Asubuhi ya siku inayofuata, mama wa Bi. Nangiro alipokea taarifa kutoka kwa majirani kwamba binti yake alikuwa karibu kufa.
Mwanamke huyo alikuwa hana fahamu wakati mama yake alipofika. Teksi ya pikipiki, inayojulikana kama boda boda, ilipatikana na kumpeleka kwenye Kituo cha Afya cha Loroo III.
Huko, daktari aligundua kwamba “baadhi ya sehemu za mwili wake zilikuwa zimeondolewa,” kama ambavyo wanajamii wangeelezea baadaye, na mwanaye pia alikuwa amekufa.
Bi. Nangiro alikimbizwa hospitali ya Amudat kwa gari la wagonjwa wa dharura, lakini alifariki njiani.
Mapambano kwa ajili ya kupata haki
Consolata Aleper, mwenyekiti wa timu ya ufuatiliaji wa ukeketaji wa wanawake wa Wilaya ya Loroo, amekuwa akisaidia familia na jamii baada ya janga hili.
Anasema kifo cha Bi. Nangiro kilichotokea miaka mitatu iliyopita kimeacha pengo katika familia na katika jamii kwa ujumla.
Mume wa Bi. Nangiro, Ikomol, alihama kutoka kijiji hicho, akiwa kwa huzuni nyingi. Inasemekana hajaolewa tena huku wajamii wa eneo hilo wakisema wamepoteza binti.
Kwa upande wake, Bi. Telo amebaki na huzuni kuhusu kupoteza dada yake licha ya miaka iliyopita. Anasema anasumbuliwa na mateso ya dada yake pamoja na ukosefu wa haki.
Tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Loroo, lakini mwanamke aliyefanya ukeketaji na mama mkwe aliyeandaa zoezi hilo walitoroka.
Lakini watu wengi zaidi wanazungumza wazi kuhusu suala hili — hasa tangu mwaka wa 2021, wakati shirika la ActionAid International Uganda na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi duniani UNFPA, lilipoanzisha mradi katika Wilaya ya Amudat.
Programu hiyo, chini ya Mpango wa Pamoja wa UNFPA na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF wa Kukomesha Ukeketaji wa Wanawake, ina lengo la kukabiliana na ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ukeketaji wa wanawake. Kupitia mradi huo, timu za ufuatiliaji zimeanzishwa katika maeneo yote ya kata hiyo.
Matukio ya ukeketaji wa wanawake yanapungua nchini Uganda, ambayo ni nchi pekee katika kanda ya Afrika Mashariki na Kusini inayokaribia kukomesha desturi hiyo ifikapo mwaka 2030. Hata hivyo, vikundi vya ufuatiliaji huko Amudat bado vinapokea tahadhari mbili hadi tatu za matukio ya ukeketaji kwa mwezi.
Bi. Telo pia amehusishwa katika mradi huo. Ameweza kupata msaada kutoka kwa washauri katika kituo kilichopo karibu cha waathirika wa ukatili wa kijinsia, na amekuwa na uwezo wa kushiriki hadithi ya dada