Watekelezaji wa sheria wanatumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika
Watekelezaji wa sheria wanatumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika
Ripoti mpya ya jopo la wataalam lililoteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu imebaini kuwa waafrika na watu wenye asili ya kiafrika ambao wamepitia matumizi ya nguvu kupita kiasi na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu kutoka kwa maafisa wa utekelezaji sheria wanaendelea kukumbana na hali ya kutokuwajibika kwa maafisa hao.
Akizungumza leo huko Geneva, Uswisi, Mwenyekiti wa Mfumo Huru wa Wataalam wa Kimataifa wa Kuendeleza Haki na Usawa wa Rangi katika Utekelezaji wa Sheria, Akua Kuenyehia, ameongeza kuwa, “madhihirisho ya ubaguzi wa rangi wa kimfumo dhidi ya Waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika na maafisa wa utekelezaji wa sheria na katika mifumo ya haki za jinai bado yanatawala katika sehemu nyingi za dunia, na hali ya kutokuwajibika inaendelea kwa kiwango kikubwa.”
Wataalam wamesema kuwa, zaidi ya hayo, haki za waathiriwa za kupata haki, ukweli, fidia, na dhamana ya kutorudia makosa hayo “mara nyingi hazitimiziwi,” na wamependekeza hatua kadhaa ambazo Mataifa yanapaswa kuchukua ili kutoa haki, uwajibikaji, na marekebisho.
Kwa upande wake, Tracie Keesee, mmoja wa wataalam hao, amesema, “watu na jamii zinazoathiriwa na ukatili wa polisi na ukiukwaji wa maadili wanaripoti mara kwa mara juu ya changamoto wanazokutana nazo wanapodai haki, uwajibikaji, na marekebisho kwa ukiukwaji unaofanywa na maafisa wa utekelezaji wa sheria, ndiyo sababu tunawasilisha mapendekezo haya maalum yanayolenga hatua.”
Katika ripoti yake kwa kikao cha 57 cha Baraza la Haki za Binadamu, wataalam hao walichunguza vikwazo vinavyowakabili waafrika na watu wenye asili ya kiafrika wanapodai haki, uwajibikaji, na marekebisho. Ripoti hiyo pia imeeleza hatua za kimsingi zinazohitajika ili kupambana na hali ya kutokuwajibika, ikikamilishwa na mapendekezo maalum yanayolenga hatua, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kuanzisha utoaji wa taarifa wenye ufanisi, taratibu za ukaguzi na uchunguzi. Aidha, inapendekeza kuanzishwa kwa mashirika huru vya uangalizi wa utekelezaji wa sheria na kuunda mifumo huru ya kusaidia waathiriwa na jamii.
“Hili limechelewa kwa muda mrefu,” amesema Víctor Rodríguez Rescia, mmoja wa wataalam hao. “Ni wakati wa Mataifa kuwekeza katika kujenga taasisi imara ili kutoa haki, uwajibikaji, na marekebisho kwa waathiriwa kwa ufanisi. Mataifa yana jukumu la kutimiza kwa haraka haki ya fidia ya mwathiriwa, kwa usahihi, na kwa ufanisi, na msaada wa kina na wa kijumla unahitajika katika hili.”
Huko Brazil, wataalamu hao walibaini kuwa ubaguzi wa rangi dhidi ya watu wenye asili ya kiafrika ulikuwa wa kimfumo na umeenea. Kwa sababu ya desturi ya kimfumo ya ubaguzi wa rangi katika utekelezaji wa sheria, waafrika-wabrazil wana uwezekano mara tatu zaidi wa kuuawa na polisi.
Huko Italia, wataalamu hao walibaini kwamba upendeleo dhidi ya waafrika na watu wenye asili ya kiafrika umechangia ubaguzi wa rangi katika utekelezaji wa sheria na uwakilishi wao usio wa uwiano ndani ya mfumo wa haki za jinai wa Italia.
Haja ya kuimarisha uwajibikaji kwa vitendo vya maafisa wa utekelezaji wa sheria zimesisitizwa katika ripoti zote za nchi hizo mbili, ambazo zote zinajumuisha mapendekezo kwa mamlaka za mataifa husika.
Wataalamu watawasilisha ripoti yake kwa Baraza la Haki za Binadamu tarehe 2 Oktoba 2024, katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, pamoja na ripoti za ziara za nchi zilizofanywa Brazil na Italia.