Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jaribio la kuishinda Urusi ni ‘kutaka kujiua', Lavrov aionya Ukraine na mataifa ya Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nje Sergey Lavrov wa Shirikisho la Urusi akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha sabini na tisa cha Baraza Kuu katika jukwaa lenye nembo ya UN .
UN Photo/Loey Felipe Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Urusi Sergey Lavrov akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha sabini na tisa cha Baraza Kuu.

Jaribio la kuishinda Urusi ni ‘kutaka kujiua', Lavrov aionya Ukraine na mataifa ya Magharibi

Masuala ya UM

Matumaini ya Ukraine ya kuishinda Urusi kwenye uwanja wa vita hayana maana ikizingatiwa kwamba Moscow ina silaha za nyuklia na juhudi zozote za muungano wa NATO kuendelea kuisaidia Kyiv zitakuwa "kutaka kujiua", Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov amesema akihutubia Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Jumamosi Septemba 29.

Sergey Lavrov amesema ukosoaji wa "operesheni maalum" ya Urusi kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kuheshimu eneo la Ukraine, ulipuuza ukweli kwamba mkataba huo pia "unatangaza wajibu wa kuheshimu kanuni za usawa na kujitawala kwa watu", amesema, akitetea hoja kwamba huu ulikuwa ndio msingi wa juhudi zinazoendelea za kuondoa ukoloni.
 
Bwana Lavrov amesema Rais Vladimir Putin alikuwa na "mpango wa kweli wa suluhu" na alikuwa tayari kujadiliana, akizilaumu nchi za Magharibi kwa kuhujumu majaribio ya hapo awali ya kujadiliana.
 
Amesema jaribio la mhimili wa Washington (Marekani) – London (Uingereza) - Brussels (Ubelgiji) kuishinda Urusi linabatilisha majaribio ya Umoja wa Mataifa ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kupitia makubaliano kama vile Pact for the Future ,Mkataba wa Zama Zijazo ambayo Urusi ilikataa kuunga mkono  na "inazuia utendakazi wa mfumo mzima" wa utawala wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Baraza la Usalama.
 
"Hilo sio jambo tulilochagua na hatuwajibiki kwa matokeo yake hatari," ameongeza.
 
Ameshutumu nchi za Magharibi kwa "kuharibu kwa kasi mfano wa utandawazi ambao wao wenyewe walitengeneza", akionya kwamba maeneo mengine ya dunia yalikuwa yanaunda ushirikiano wao wenyewe, wakikaribisha Ulaya na Asia yote kujiunga na "nafasi moja ya ‘Eurasia’" tofauti na ushawishi wa Marekani.

Azishukia Israel na Marekani

Akizungumza kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati, Bwana Lavrov amesema hakuna uhalali wa mashambulizi ya kigaidi ya Hamas na wengine yaliyofanyika Oktoba 7 lakini "adhabu kubwa ya pamoja" ya Wapalestina tangu wakati huo imesababisha "janga la kibinadamu ambalo halijawahi kutokea."
 
Amesikitika kuongezeka kwa "mauaji ya kisiasa ambayo yanakaribia kuwa ya kawaida" na akabainisha kuripotiwa mauaji ya kiongozi wa Hezbollah siku ya Ijumaa huko Beirut.
 
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Urusi ameongeza kwamba Umoja wa Mataifa wenyewe unahitaji kuwa na mkono zaidi katika kuchunguza "mbinu za kigaidi" zinazotumiwa na Israeli, Marekani na wengine, kama vile wakati wa mashambulizi ya vifaa vya mawasiliano nchini Lebanon wiki iliyopita.
 
Zaidi ya hayo, Umoja wa Mataifa ulihitaji "kuepusha jaribu la kucheza mikononi mwa Mataifa binafsi, hasa yale ambayo hayatoi wito kwa ushirikiano bali kugawanya ulimwengu kati ya bustani ya maua na msitu au kwa wale wanaoketi meza ya demokrasia, na wale walio kwenye ‘orodha ya vyakula’."