Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umasikini uliniachisha shule, asante mradi wa UNICEF sasa naendelea na ndoto yangu: David Tumaini

David Tumaini, mvulana wa miaka 16 kutoka Kaunti ya Kilifi, Kenya, anapigwa picha katika mtindo wa picha.
UNICEF Kenya David Tumaini kijana mwenye umri wa miaka hivi sasa 16 kutoka kaunti ya Kilifi nchini Kenya, ambaye ni mmoja wa wanafunzi waliolazimika kukatiza masomo kwa sababu ya umaskini.

Umasikini uliniachisha shule, asante mradi wa UNICEF sasa naendelea na ndoto yangu: David Tumaini

Utamaduni na Elimu

Maelfu ya watoto katika Kaunti ya Kilifi Pwani ya Kenya kwa miaka mitatu iliyopita wamelazimika kuacha shule kutokana na umasikini na ukame na mafuriko yaliyochangiwa na mabadiliko ya tabianchi. Lakini sasa wizara ya elimu ya Kenya kwa kushirikiana na mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, wakfu wa Education Above all na wadau wengine juhudi zinafanyika kuwarejesha watoto shuleni.

David Tumaini kijana mwenye umri wa miaka hivi sasa 16 mmoja wa wanafunzi  waliolazimiika kukatiza masomo  miaka miwili iliyopita katika shule ya msingi ya Soyosoyo kutokana na umasikini. Kwa miezi kadhaa alihaha kusaka njia ya kuendelea na masomo, anasema

“Niliacha shule darasa la nne  ilikuwa mwaka 2022, kwasababu shuleni walikuwa wananirejesha nyumbani nikalete ada. Sasa nikifika nyumbani wazazi wanasema hawana. Nilikaa nyumbani kwa muda wa miezi mitano, wakati wenzangu wanakwenda shule na ni siku za masomo na wewe uko nyumbani. Hii inakufanya ujihisi kama wewe si mtu muhimu.”

Wanafunzi wakiwa darasani katika shule moja huko Kilifi, Kenya.
UNICEF Kenya Wanafunzi wakiwa darasani katika shule moja huko Kilifi Kenya, akiwemo David Tumaini (anayetabasamu nyuma), mvulana mwenye umri wa miaka 16 ambaye alilazimika kuacha shule kwa sababu ya umaskini. Shukrani kwa UNICEF na wawadau wake sasa yeye amerejea shuleni.

Hisia kama hizo na mustakbali wa watoto hao ndio kilicholisukuma shirika la UNICEF kuanzisha mradi wa “Elimisha mtoto” likishirikisha wizara ya elimu ya kenya na wadau wengine ili kuhakikisha watoto kama David wanarejea shuleni. Elizabeth Waitha ni afisa elimu wa  UNICEF.

“Tuliweza kubaini Kaunti 16 ambazo zilikuwa na watoto zaidi ya 10,000 ambao wanaendi shuleni, na hii ilikuwa ni kwa shule za msingi tu. Na tukaangalia ni jinsi gani ya kuhakikisha mazingira bora ya kusoma kwa watoto waliosajiliwa kwenye mradi. Na tumeweza kuwasaidia zaidi ya wanafunzi milioni kwa vifaa vya shule na pia kwa waalimu vifaa vya kuandikia kama chaki, kalamu na vingine.”

Na ndipo David akasikia kuhusu mradi huo..

“Nilipata taarifa kutoka kwa walimu ya kwamba kuna mradi ambao unawasaidia watoto walioacha shule ili warehjee shuleni kuendelea na masomo. Sasa nilipokuja shuleni nikaambiwa wewe tutakusajili katika huu mradi wa msaada , ndipo nikaweza kurejea masomoni, hadi sasa nipo shuleni kwa sababu ya msaada huu. Vitu ambavyo nilipewa ni pamoja na mkoba wa madaftari, vitabu, kalamu na vifutio.”

Hii imemrejeshea David matumaini ya ndoto yake.

“Mimi nikimaliza kusoma nataka kuwa Daktari ili kusaidia wagonjwa. Na katika kusaidia wagonjwa mshahara nitakaolipwa ntajisaidia mwenyewe na pia kusaidia familia yangu”

Kupitia mradi huu mbali ya vifaa umewezesha zaidi ya watoto 256,000 kurejea shuleni na bado wanaendelea na masomo.