Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lebanon: Saa 24 zilizopita zamtia hofu Guterres

Moshi unafuka kutoka eneo lililolengwa na makombora katika kijiji cha kusini mwa Lebanon cha Zaita mnamo Septemba 23, 2024.
© UNICEF/Dar al Mussawir Moshi ukifuka kutoka kwa eneo lililolengwa kwa makombora katika kijiji cha Zaita kusini mwa Lebanon.

Lebanon: Saa 24 zilizopita zamtia hofu Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ana hofu kubwa kutokana na hali ya usalama inavyozidi kuzorota kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut katika saa 24 zilizopita.

Guterres amesema hayo kupitia taarifailiyotolewa na msemaji wake, Stéphane Dujarric jijini New York, Marekani hii leo.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa katika saa 24 zilizopita mashambulizi ya Israeli dhidi ya kundi la Hezbollah kusini mwa Lebanon yamesababisha vifo ikiwemo cha kiongozi wa kundi hilo Hassan Nasrallah.

Vyombo hivvyo vinaeleza kuwa tayari wanamgambo wa kihouthi nchini Yemen na Hamas huko Gaza wamedai kuwa watalipiza kisasi dhidi ya Israeli kutokana na kifo chake.

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu kupitia msemaji wake anasisitiza kuwa mzunguko wa ghasia lazima ukome sasa, na pande zote lazima zijizuie kuendeleza mwenendo wa sasa.

“Wananchi wa Lebanon, wananchi wa Israeli na wote kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati, hawaweze kukumbana na vita,” amesema Katibu Mkuu.

Amesihi pande zote kuazimia kurejea katika azimio namba 1701 la mwaka 2006 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na zikomeshe mara moja uhasama.

Amerejelea tena wito wake wa kutaka sitisho la mapigano ukanda wa Gaza kati ya Israeli na Hamas na kuachiliwa huru kwa mateka wote wanaoshikiliwa kwenye eneo hilo.

Mapigano kati ya Israeli na wanamgambo wa Hezbollah wa nchini Lebanon yameanza baada ya Israeli kudai kuwa kundi hilo linahusika na makombora yanayorushwa kutokea kusini mwa Lebanon.