Afrika inastahili viti 2 vya kudumu na 2 vya mzunguko kwenye Baraza la Usalama: Uganda Nabbanja
Masuala ya UM
Waziri Mkuu wa Uganda Robinah Nabbanja amerejea kutoa wito wa mageuzi ya "haraka na ya kina ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ili Afrika iwakilishwe katika viti vya kudumu na visiyo vya kudumu”.
Waziri Mkuu huyo ambaye amehutubia leo mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York amesema “Uganda inaamini kwamba manufaa ya dunia hii lazima yafurahiwe na kuganywa kwa wanadamu wote na inachukia aina zote za kutengwa na mataifa machache tajiri”.
Amesema katika Baraza la Usalama Afrika inapaswa kuwa na viti viwili vya ujumbbe wa kudumu wenye kura ya veto na wajumbe wawili wa mzunguko.
Waziri Robinah Nabbanja amesisitiza kwamba Uganda inakataa kuongezeka kwa ushindani na makabiliano kati ya mataifa makubwa, ambao amesema unadhoofisha hatua ya pamoja ya kimataifa kwa aili ya usalama, amani, utulivu na maendeleo ya kiuchumi ya kijamii."
Ufadhili ni changamoto kubwa
Bi. Nabbanja amesema ufadhili unasalia kuwa moja ya changamoto kubwa zaidi zinazodhoofisha juhudi za nchi zinazoendelea kutekeleza kikamilifu Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.
Amebainisha kuwa kukopa ni muhimu kwa kufadhili uwekezaji katika maendeleo endelevu.
Waziri Nabbanja amesema, "Madeni ni nyenzo muhimu ya kufadhili maendeleo endelevu, kuwezesha nchi za kipato cha chini kuwekeza katika miundombinu, afya, elimu na maeneo mengine muhimu."
Amesisitiza kwamba "mikopo kwa nchi zinazoendelea yenye mapato duni inapaswa kuwa ya masharti nafuu na bila riba."
Waziri Mkuu pia ametoa wito wa mageuzi ya haraka ya usanifu wa kimataifa wa masuala ya fedha.
"Ikiwa ni pamoja na taasisi za fedha za kimataifa na sheria zao ili kuhakikisha uwakilishi sawa wa nchi zinazoendelea katika maamuzi ya utawala wa kiuchumi wa kimataifa unaoathiri mwelekeo wa maendeleo ya kitaifa."
Teknolojia na tabianchi
Kuhusu teknolojia, amesema, "Hakuna shaka kwamba nishati nafuu na fursa ya kuunganishwa na mtandao wa intaneti wenye ubora wa juu ni muhimu ili kuchochea utekelezaji kamili kuweza kufikia matokeo ya maendeleo jumuishi na manufaa kwa watu wetu."
Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Waziri Mkuu Nabbanja amesema, "Nchi zenye kipato cha juu zinapaswa kupunguza uzalishaji wao wa nishati chafuzi na kusaidia kwa usawa nchi zinazoendelea katika mpito wao wa hatua kwa hatua kwenda kwenye njia za maendeleo zenye uzalishaji mdogo wa hewa ukaa bila kutumia mazingira kama nyenzo ya kisiasa na kiuchumi ya kuzuia au kupunguza kasi ya maendeleo yao.”