Maendeleo Endelevu
Mwanzoni mwa hotuba yake kwa katija Mjadala huu mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA59, Bwana Majaliwa amewaeleza viongozi wengine wa ulimwengu namna Tanzania inavyoyatekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) akisema, “ni mwanga wa matumaini katika kutatua changamoto za kimataifa.” Safari ya Tanzania kuelekea maendeleo endelevu inaakisi ile ya mataifa mengi, yanayokabiliwa na changamoto kubwa kutokana na athari mbaya za COVID-19 kwenye mifumo ya afya na kiuchumi. Mabadiliko ya tabianchi, yanayodhirika kwa hali mbaya ya hewa kama vile mvua kubwa na ukame, yamezorotesha masuala ya afya na miundombinu iliyodorora.
“Tuna wasiwasi kuhusu kasi ndogo ya kufikia malengo haya, ambapo kufikia mwaka wa 2023, ni asilimia 17 tu ya malengo yaliyokuwa yamefikiwa, huku zaidi ya theluthi moja ikirudi nyuma au kukwama. Hatua za haraka na mshikamano wa kimataifa zinahitajika ili kuondokana na vikwazo kama vile kukosekana kwa usawa wa kiuchumi, mabadiliko ya taianchi, migogoro na ukosefu wa usawa wa kijinsia.” Amisisitiza.
Tanzania inavyotekeleza SDGs
Waziri Mkuu wa Tanzania ameeleza kwamba ahadi ya Tanzania kuelekea utekelezaji wa SDGs, zinalenga katika ukuaji endelevu wa uchumi kupitia uwekezaji wa kimkakati katika kilimo, ufugaji wa samaki, mifugo, uvuvi, maendeleo ya miundombinu, nishati na teknolojia ya kidijitali. “Lengo letu ni kuboresha uhakika wa chakula, kupunguza umaskini, kuhakikisha uanzishwaji wa ajira na kukuza ukuaji wa uchumi jumuishi. Kuna simulizi nyingi za mafanikio nchini Tanzania zinazotokana na uwekezaji huu, kama vile uwezeshaji wa vijana kupitia Mpango wa Kilimo Bora wa Kesho (BBT) Tanzania Bara, na kuwawezesha wanawake wa ndani Zanzibar kupitia kilimo cha mwani.” Kwa upande mwingine, Tanzania inatekeleza sera za kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya na elimu kwa wananchi wote, ikiwa ni pamoja na sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na Elimu ya Msingi Bila Malipo. Serikali pia inawekeza katika mafunzo ya ufundi stadi na elimu ya STEM ili kuwaandaa vijana katika soko la ajira na uchumi wa kidijitali.
Kutetea Utu, Ushirikishwaji na Usawa
Kassim Majaliwa Majaliwa akijielekeza katika kutetea maslahi ya nchi nyingine amekumbushia kwamba kwa miongo kadhaa, sera ya mambo ya nje ya Tanzania imetanguliza heshima ya utu wa binadamu. Akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 14 Desemba 1961, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Waziri Mkuu wa Tanganyika wakati huo alisema: “Msingi wa matendo yetu, ya ndani na nje, yatakuwa ni jaribio, jaribio la uaminifu, la kuheshimu utu wa mwanadamu.” Mheshimiwa Rais, Tanzania imedumisha ahadi hii kwa kuongoza mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi.
Ondoeni vikwazo kwa Cuba na wengine
Kwa msingi huo, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Kamati ya Ukombozi ya OAU, ikiwaunga mkono wapigania uhuru katika harakati zao za kupigania uhuru. Licha ya kupata ukombozi wa kisiasa, nchi nyingi bado zinakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi na hali isiyo ya kibinadamu ambayo inazuia kupatikana kwa maendeleo ya kweli. “Hivyo, tunatoa wito wa kupatikana kwa haki ya kujitawala kwa watu wote chini ya ukoloni na kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi yao. Baraza hili linapaswa kuendelea kwa ujasiri zaidi kutoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya watu wa Cuba na nchi nyingine, ili kuruhusu watu wa nchi hizi kutambua haki zao za msingi, ikiwa ni pamoja na haki ya maendeleo.” Akaipigia chepuo Cuba ambayo imekuwa ikiathirika kwa miongo mingi kutokana na vikwazo vya kiuchumi.
Tanzania inaamini kila mtu anapaswa kuishi huru na salama
Aidha Bwana Majaliwa ameukumbusha Umoja wa Mataifa wajibu wake akianza kwa kueleza kwamba migogoro ya kimataifa ya kibinadamu kutokana na vita, migogoro na maafa ya asili inahitaji ufikiaji usio na kikomo wa misaada ya kibinadamu, matibabu bila ubaguzi kwa waathirika, uwajibikaji kwa ukatili, na ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kudumisha utu wa binadamu kwa ulimwengu wa amani. Tanzania inaamini kuwa kila mtu anastahili kuishi kwa heshima, uhuru na usalama ili kufikia uwezo wake kamili. Umoja wa Mataifa haupaswi kubaki katika hali ya kutojali katika hali hizi, kwani kufanya hivyo kutadhoofisha tu uhalali wake.
Amani na Usalama
Usalama na amani ni muhimu katika kupata maendeleo. Mbele ya matishio ya kiafya ya kimataifa, yanayodhihirishwa na milipuko kama vile Covid-19 na kwa sasa Mpox, inayozidisha mivutano ya kijiografia na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi, “usemi kwamba hakuna mtu aliye salama hadi kila mtu awe salama utapata maana”. “Ni muhimu kwamba tunapaswa kuwekeza zaidi katika amani, kukuza umoja na kujenga upya uaminifu.” Amekazia.
Dhamira ya Tanzania katika kuleta amani haitadhoofika
Kwa kutambua hitaji hili, Tanzania kwa miongo kadhaa imeshiriki katika juhudi za kulinda amani, kujenga amani na upatanishi. Tanzania ina na inaendelea kuchangia katika kuleta amani duniani kupitia uanachama wake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la Amani na Usalama la Muunguno wa Afrika. Mchango huu pia unadhihirika kupitia uongozi wake katika mipango ya kikanda, kama vile Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu ya Afrika na sasa uenyekiti wa Chombo cha Siasa, Ulinzi na Usalama cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.
Kiongozi huyo amelihakikishia Baraza la Umoja wa Mataifa akisema, “napenda kulihakikishia Baraza hili tukufu kwamba dhamira ya Tanzania katika kuleta amani haitadhoofika. Tanzania itaendelea kutekeleza kwa bidii majukumu yanayotokana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”
Lugha ya Kiswahili iwe lugha rasmi ya 7 ya UN
Waziri Mkuu Majaliwa ameeleza namna ambavyo Tanzania imepokea kwa mikono miwili kupitishwa kwa azimio la Baraza Kuu la 78/312, linalotangaza tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili. Kiswahili, lugha inayozungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 katika mabara yote ya dunia, ni nyenzo muhimu ya kuendeleza amani, umoja na tofauti za kitamaduni. Wakati Tanzania na nchi nyingine zinazozungumza Kiswahili zikitarajia kuadhimisha siku hii mwaka 2025 na kuendelea, “tunaliomba Baraza hili pia kuangalia uwezekano wa kuitambua kuwa ni lugha rasmi ya 7 ya Shirika letu Tukufu.” (Kwa sasa lugha rasmi za Umoja wa Mataifa ni 6 nazo ni Kiarabu, Kichina, Kiingereza, Kirusi, na Kispaniola).
“Muungano wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika tayari zimeongoza njia.” Amesema Kassim Majaliwa.
Mabadiliko ya Tabianchi
Tanzania, kama nchi nyingine nyingi zinazoendelea, iko katika hatari kubwa ya ukame, mafuriko, jangwa na athari za kupanda kwa kina cha bahari. Inakadiriwa kuwa kina cha bahari kitapanda kwa sentimita 41 ifikapo mwaka 2080. Ingawa kupanda kwa kina cha bahari hakuwezi kurejeshwa nyuma, Tanzania inachukua hatua kadhaa za kukabiliana na hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kurejesha na kupanda mikoko, uimarishaji wa miundombinu ya pwani, na kukuza utalii unaozingatia utunzaji wa mazingira na pia ufugaji wa samaki. “Kwa hivyo ni muhimu kwamba lazima tuwekeze zaidi katika ufadhili wa tabianchi ili kusaidia kurejesha uchumi ambao tayari unakabiliwa na athari hizi na kuimarisha upatikanaji wa ufadhili wa hasara na uharibifu katika nchi zilizoathirika zaidi.” Amesisitiza Waziri Mkuu wa Tanzania.
Nishati Safi
Tunapojiandaa kwa ajili ya COP 29 huko Baku, Azerbaijan ( Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi COP29), inafaa kukumbuka kuwa duniani kote, inakadiriwa kuwa watu bilioni 2.4 bado wanatumia nishati chafuzi kwa kupikia. Hii inachangia matatizo ya afya, ukosefu wa chakula, usawa wa kijinsia, na uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na mamilioni ya vifo vya mapema, upatikanaji mdogo wa elimu na ajira kwa wanawake na watoto, na kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi chafuzi na ukataji miti. Kufanikisha ufikiaji wa kupikaj usio chafua mazingira kwa wote barani Afrika ifikapo 2030 kutahitaji kiasi kinachokadiriwa cha Dola za Kimarekani bilioni 4 kila mwaka, ambacho ni kiasi kidogo cha matumizi/gharama za nishati duniani.
Mkutano wa Nishati kufanyika Tanzania mwakani
“Napenda kuliarifu Baraza hili tukufu kwamba Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Afrika mwezi Januari 2025, utakaoratibiwa pamoja na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.” Amesema Majaliwa akiongeza kuwa mkutano huo unalenga kuharakisha utekelezaji wa Kundi la Benki ya Dunia na dhamira ya Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika kutoa huduma ya umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo 2030. Tunatazamia kufanya kazi pamoja na washirika wote ili kufungua uwezo wa nishati na kujenga mwangaza zaidi, mustakabali thabiti zaidi wa Afrika.
Demokrasia
Waziri Mkuu Majaliwa amewaeleza viongozi wenzake wa ulimwengu kuwa mwezi Novemba mwaka huu, Tanzania itafanya uchaguzi wa serikali za mitaa, na kufuatiwa na uchaguzi wa rais na wabunge Oktoba mwakani.
Tunapojiandaa kwa matukio haya ya uchaguzi, napenda kulihakikishia Baraza hili kwamba demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria vitadumishwa kulingana na maono ya Rais Samia kama yalivyoainishwa katika falsafa ya R 4, ambayo ni: maridhiano, mnepo au ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya. “Tangu kutangazwa kwa kanuni za falsafa 4R mwaka 2021, Serikali ya Tanzania imeendelea kuhimiza utangamano na kuendeleza umoja katika migawanyiko ya kisiasa, kidini na kikabila. Katika utekelezaji wa 4R, serikali pia imefanya mageuzi kadhaa makubwa ambayo yanalenga kushughulikia mapungufu ndani ya mfumo wa haki ya jinai, kuruhusu michakato ya kisiasa yenye ufanisi na kuimarisha kufurahia haki za binadamu.”