Netanyahu aitetea Israel na kukanusha alichokiita uongo na kashfa dhidi ya taifa hilo
Netanyahu aitetea Israel na kukanusha alichokiita uongo na kashfa dhidi ya taifa hilo
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akihutubia mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo amesema awali alikuwa na nia ya kutokuja kwenye mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu lakini baada ya kusikia "uongo na kashfa zinazotolewa dhidi ya nchi yake na viongozi wengine, aliamua kwamba anapaswa kuja na kuliweka sawa suala hilo."
Amesema "Niliamua kuja hapa kuwasemea watu wangu, kuongea kwa ajili ya nchi yangu na kusema ukweli," akisisitiza kwamba Israeli inatamani amani. Ameendelea kusema kwamba "Tunakabiliana na maadui wakali na wakubwa wanaotaka kutuangamiza, na lazima tujilinde dhidi ya wauaji hawa wakatili, ambao hawataki tu kutuangamiza bali pia kuharibu ustaarabu wetu wa kawaida na kuturudisha sote kwenye enzi ya giza ya dhuluma na ugaidi."
Israel inakabiliwa na uchaguzi uleule kuvipa vizazi vijavyo baraka au laana
Amekumbusha hotuba yake kwa mjadala mkuu wa mwaka jana, alipokuwa amesema kwamba Israeli inakabiliwa na uchaguzi uleule usio na wakati ambao Musa aliweka mbele ya watu wake maelfu ya miaka iliyopita, “kwamba matendo yetu yataamua ikiwa tunavipa vizazi vijavyo baraka au laana. Na hilo ndilo chaguo tunalokabiliana nalo leo.
Akifafanua kauli hiyo amesema kwamba ni "laana ya uchokozi usio na kikomo wa Iran au baraka ya upatanisho wa kihistoria kati ya Waarabu na Myahudi." Bwana Netanyahu amesema Katika siku zilizofuata, "baraka hiyo ilikaribia kwa njia ya makubaliano ya kuhalalisha kati ya Saudi Arabia na Israeli, lakini ikaja laana ya Oktoba 7 wakati maelfu ya magaidi wa Hamas wanaoungwa mkono na Iran walipovamia Israeli, na kufanya ukatili usioweza kufikiria ikiwa ni pamoja na kuwaua kikatili watu 1,200, wakiwemo watoto, ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na kuwateka nyara watu 251 kutoka nchi tofauti.”
Amesema "Matukio haya yanakukumbusha mauaji ya Nazi,"
Nina ujumbe kwa Iran
Netanyahu amesema “Nina ujumbe kwa madhalimu wa Tehran. Ukitupiga tutakupiga. Hakuna sehemu nchini Iran ambayo mkono mrefu wa Israel hauwezi kufika. Hii inatumika kwa Mashariki ya Kati nzima."
Pia amekuwa na ujumbe mwingine kwa Baraza Kuu na ulimwengu nje ya Baraza lake kwamba “Israeli itashinda”
Ameonya kwamba “Nchi yake inakabiliwa na maadui wakali wanaotaka kutuangamiza. Ni lazima tujilinde dhidi ya wauaji hawa wakatili."
Amesisitiza kuwa Israel itaukataa utawala wowote wa Hamas huko Gaza baada ya vita, akibainisha kwamba wanachotafuta ni Gaza isiyo ya kijeshi na iliyochafuliwa.
"Hapo tu ndio tunaweza kuhakikisha kwamba duru hii ya mapigano itakuwa ya mwisho."
Hatutochoka mpaka mateka warejee nyumbani
Kuhusu mateka ambao bado wanashikiliwa Gaza na Hamas kufuatia mashambulizi ya Oktoba 7 mwaka jana ambayo yalikatili maisha ya watu 1200 na wengine zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka Waziri mkuu huyo wa Israel amesema “Asilani hatutochoka kufanya kila liwezekanalo kuhakisha mateka wote ambao bado wanashikiliwa wanarejea nyumbani salama kuungana na familia zao.”
Ameonya kwamba Israel haitokubali utawala wowote wa Hamas Gaza “Tunachotaka ni Hamas kuondoka, ni lazima iondoke” amesema akisistiza kuwa utawala wowote wa kijesho Gaza hauwezi kukubalika na Israel.
Amesema hadi pale Hamas na washirika wake watakapoacha udhalimu wao na mashambulizi dhdi ya Israel, taifa hilo litafanya kila liwezekanalo kujitetea na kulinda watu wake.