Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la kibinadamu Sudan wanawake na wasichana ni wahanga wakubwa wa ukatili wa kijinsia ukishika kasi: UN

Watoto waliohamishwa wanashiriki katika kikao cha kujifunza kidijitali katika kambi ya watu waliohamishwa ndani ya Al Salam katika jimbo la Kassala, Sudan, kwa kutumia vifaa vya simu na vichwa vya sauti.
© UNICEF/Ahmed Mohamdeen Elfati Wasichana waliokimbia makazi yao nchini Sudan wanashiriki katika somo la kidijitali katika jimbo la Kassala.

Janga la kibinadamu Sudan wanawake na wasichana ni wahanga wakubwa wa ukatili wa kijinsia ukishika kasi: UN

Wanawake

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya Wanawake UN Women inaangazia athari kubwa za janga la kibinadamu linaloongezeka kwa kwa wanawake na wasichana wa Sudan, wakiwemo milioni 5.8 ambao ni wakimbizi wa ndani.

Katika tipoti hiyo iliyotolewa jijini Nairibi na New York, UN Women inasema  “Mzozo nchini Sudan umesababisha janga kubwa kubwa zaidi la wakimbizi wa ndani kuwahi kutokea duniani tangu vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria mwaka 2011 na mzozo huo umekuwa na madhara makubwa kwa wanawake na wasichana, kutokana na tathimini ya masuala ya kijinsia iliyofanywa na shirika letu.”

Ripoti inasema “Idadi ya watu wanaohitaji huduma zinazohusiana na unyanyasaji wa kijinsia imeongezeka kwa asilimia 100 tangu mwanzo wa mgogoro, hadi watu milioni 6.7 kufikia Desemba 2023, na takwimu hizi zinakadiriwa kuwa kubwa zaidi leo. Wakati wanaume na wavulana pia ni waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia, nyingi ya kesi hizo zinahusisha wanawake na wasichana.”

Vurugu zinazoendelea, haswa Khartoum, Darfur, na Kordofan, zimezidisha hatari zinazowakabili wanawake na wasichana, huku kukiwa na ripoti zinazoongezeka za unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro, unyanyasaji wa kijisnia na ukatili imeongeza ripoti.

“Takriban wanawake na wasichana milioni 5.8 waliokimbia makazi yao wamo hatarini zaidi, huku visa vingi vya unyanyasaji vikiendelea bila kuripotiwa kutokana na ukosefu wa usaidizi wa kutosha na hofu ya unyanyapaa na kuadhibiwa.”

Zahma ya kutokuwa na uhakika wa chakula

Kwa mujibu wa ripoti Sudan hivi sasa inakabiliwa na viwango vya juu zaidi vya uhaba wa chakula kuwahi kurekodiwa nchini humo. Huku asilimia 64 ya kaya zinazoongozwa na wanawake zinakabiliwa na uhaba wa chakula ikilinganishwa na asilimia 48 ya kaya zinazoongozwa na wanaume katika majimbo kumi, wanawake na wasichana wanakula kidogo na wankula wa mwisho.

Pia Ripoti inasema upatikanaji wa huduma za afya ni changamoto nyingine wanawake milioni 1.63 walio katika umri wa kuzaa hawana huduma za kutosha. Miongoni mwao, zaidi ya wanawake 160,000 ni wajawazito, na inakadiriwa watoto 54,000 wanatarajiwa kuzaliwa katika miezi mitatu ijayo.

Wanawake na wasichana pia wanaendelea kuathiriwa kwa kiasi kikubwa cha ukosefu wa maji salama, yanayofikika kwa urahisi, na ya bei nafuu, usafi wa mazingira na usafi.

Angalau asilimia 80 ya wanawake waliokimbia makazi yao ripoti inasea  hawawezi kupata maji safi kutokana na gharama, wasiwasi wa usalama na umbali.

Mgogoro wa elimu nchini Sudan kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UN Women ni matokeo mengine mabaya ya mzozo huo.

Zaidi ya wasichana milioni 2.5, wanaowakilisha asilimia 74 ya wasichana wenye umri wa kwenda shule kwa sasa hawako shuleni, na hivyo kuongeza hatari ya kufanyiwa vitendo viovu kama vile ndoa za utotoni na ukeketaji.

Hodan Addou, kaimu Mkurugenzi waUN Women wa Kanda  ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika amesema "Wanawake na wasichana nchini Sudan wanakabiliwa na changamoto zisizofikirika, lakini mnepo na uthabiti wao unaendelea kututia moyo. Hatuwezi kuruhusu Sudan kuwa mgogoro uliosahaulika. Sasa, zaidi ya wakati mwingine wowote, jumuiya ya kimataifa inapaswa kushikamana pamoja ili kusaidia wanawake nchini Sudan, kuhakikisha wana rasilimali na ulinzi wanaohitaji ili kuishi na kujenga upya maisha yao,”

Hatua lazima zichukuliwe sasa

Ripoti imesisitiza kwamba Hatua lazima zichukuliwe haraka ili kuhakikisha ulinzi wa kimwili wa wanawake na wasichana pamoja na upatikanaji salama wa chakula, maji salama, na huduma za afya ya ngono na uzazi.

UN Women imesema inaunga mkono mipango ya kijamii, kwa ushirikiano na mashirika yanayoongozwa na wanawake, kujenga mnepo na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za kibinadamu kwa wanawake, wanaume, wasichana na wavulana walioathiriwa na janga hilo.

UN Women inaitaka jumuiya ya kimataifa, wafadhili na washirika wa kibinadamu kuweka kipaumbele katika ulinzi na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wa Sudan, ikiwa ni pamoja na kuongeza ufadhili kwa mashirika yanayoongozwa na wanawake, ambayo yalipata asilimia 1.63 pekee ya rasilimali za kifedha za Mfuko wa Kibinadamu wa Sudan mwaka 2023.

UN Women imesisitiza kwamba inasimama na watu wa Sudan wakati wa mzozo huu wa kibinadamu unaozidi kuzorota na kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa vita na kurejea kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya majadiliano ya amani.