Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuanzia Gaza hadi Haiti hali ya usalama ni tete duniani, tushikamane kuitatua: Rais William Ruto

Rais William Samoei Ruto wa Kenya akihutubia mjadala mkuu katika kikao cha sabini na tisa cha Baraza Kuu la UMOJA WA MATAIFA .
UN Photo/Loey Felipe Rais William Samoei Ruto wa Kenya ahutubia mjadala mkuu wa kikao cha 79 cha Baraza Kuu.

Kuanzia Gaza hadi Haiti hali ya usalama ni tete duniani, tushikamane kuitatua: Rais William Ruto

Masuala ya UM

Rais wa Jamhuri ya Kenya William Samoei Ruto amesema “Dunia iko katika wakati wa changamoto kubwa za kiusalama, ahati ya chata ya Umoja wa Mataifa kuokoa viizazi kutokana na vita iiko katika hatihati.” Amesema hayo akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Amesema nadharia ya wao dhidi yetu ni chachu ya changamoto kubwa ikiwemo vita

Kuanzia Gaza, Darfur, Ukraine, Yemen, Mashariki mwa DRC, Sudan, Sahel na uhalifunchini Haiti,migogoro inasambaratisha maisha na uwezi wa watukuishi katika kiwangocha kihistoria

Ametaka ushirikiano wa kimataifa kushughulikia changamoto hizo

Familia, wakiwemo watoto, imekusanyika kwenye mlango uliojaa watu, pengine katika mazingira ya wakimbizi au watu waliokimbia makazi yao huko Haiti.
UNICEF/Herold Joseph Maelfu ya raia wa Haiti wamekimbia ghasia katika maeneo yanayodhibitiwa na magenge, wakitafuta usalama na makazi kote nchini.

Kuhusu Haiti

Akizungumzia suala la Haiti Rais Ruto ametoa wito kwa mataifa yote Wanachama "kusimama katika mshikamano na watu wa Haiti kwa kutoa msaada unaohitajika," akiongeza kuwa nchi yake itapeleka kikosi cha ziada nchini Haiti ili kufikia lengo la maafisa wote wa polisi 2,500 ifikapo Januari mwaka ujao.

Ameongeza kuwa "Uungaji mkono wetu kwa polisi wa kitaifa wa Haiti umeendeleza kwa kiasi kikubwa utulizaji wa miji na miji, kulinda miundombinu muhimu, na kuachilia jamii nyingi zilizokuwa zimefungwa na magenge ya wahalifu hapo awali."

Rais wa Kenya pia ameupongeza “uongozi wa kisiasa wa Haiti kwa kuunda makubaliano na ramani inayotia matumaini kuelekea uchaguzi huru, wa haki na wa kidemokrasia.”

Amesema "Kenya na nchi nyingine za Caribbean na Afrika ziko tayari kutumwa lakini zinazuiwa na uhaba wa vifaa na ufadhili.”

Akaribisha kupitishwa azimio namba 2719

Rais Ruto pia amekaribisha kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama nambari 2719, kuanzisha mfumo wa kufadhili shughuli za usaidizi wa amani wa Muungano wa Afrika kupitia michango iliyotathminiwa na Umoja wa Mataifa, na hivyo kuimarisha juhudi zetu za pamoja za kulinda amani," amesema.

Amesema "Operesheni za amani za AU zinazofadhiliwa vyema sio tu kipaumbele cha Afrika lakini ni hitaji la kimataifa, kwa kuzingatia utata na asili ya jumuishi kwa amani na usalama wa kimataifa."

Rais wa Kenya pia amesisitiza kwamba usanifu uliopo wa usalama wa kimataifa, unaowakilishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, unaendelea kutatiza juhudi za kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Amesema, "Taasisi ambayo haijumuishi nchi 54 za Afrika, zinazowakilisha watu bilioni 1.4, huku ikiruhusu taifa moja kupiga kura ya turufu ya nchi wanachama 193 zilizosalia katika karne ya 21, ni jambo lisilokubalika."

Amesisitiza kuwa "Lazima tufanye haraka kulifanya Baraza la Usalama, kuwa shirikishi, lenye uwazi, demokrasia, ufanisi, na kuwajibika."

Mchanganyiko wa rangi mbalimbali wa sarafu za kimataifa na sarafu kutoka nchi tofauti zimeenea juu ya uso.
Unsplash/Jason Leung Ripoti ya UNCTAD kuhusu maendeleo ya uchumi Afrika inataka udhiibiti wa utoroshaji wa fedha barani humo ambao hupora mitaji yenye thamani ya takribani dola bilioni 89 kila mwaka. (Maktaba)

Nafasi ya Afrika kiuchumi

Pia amesisitiza kuwa nchi zinazoendelea zina misingi muhimu ya kudai nafasi yao halali katika uchumi wa dunia wa karne ya 21.

Rais Ruto amesema, "Kurahisisha msamaha wa madeni, ufadhili wa masharti nafuu, ruzuku, na vyombo vya kutoa mikopo ni muhimu ili kuongeza uwekezaji ili kuendeleza miundombinu muhimu na kupanua sekta muhimu."

Rais Ruto amehitimisha kwa kusema kwamba “Fikiria uwezo mkubwa wa Afŕika ambao haujatumiwa katika rasilimali za nishati safi. Kutumia uwezo huu ni muhimu sio tu kwa ukuaji wa uchumi wa bara la Afrika na mnepo wa kijamii, lakini pia kwa vipaumbele vya kimataifa kama kuongeza kasi ya mpito wa kuelekea nishati jadidifu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na minyororo ya usambazaji”.

Kufuatia idhini ya Baraza la Usalama chini ya azimio nambari 2699, Kenya imetuma maafisa wa polisi 382 waliopewa mafunzo maalum.

Siku chache tu zilizopita, Ruto amesema “nilipata fursa ya kutembelea Haiti, kushuhudia kazi ya maofisa wetu mashinani, na kuona maendeleo makubwa walitopiga.”