Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tshisekedi ‘aishitaki’ Rwanda kwa Umoja wa Mataifa

Rais Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha sabini na tisa cha Baraza Kuu.
UN Photo/Loey Felipe
Rais Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha sabini na tisa cha Baraza Kuu.

Tshisekedi ‘aishitaki’ Rwanda kwa Umoja wa Mataifa

Amani na Usalama

Hali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inatia wasiwasi hasa kuibuka upya kwa kundi la kigaidi la M23, linaloungwa mkono na Rwanda, kumesababisha maafa ya kibinadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa, ambapo takriban watu milioni 7 wamekimbia makazi yao. Uchokozi huu unajumuisha ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa kitaifa, amesema Rais Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo wa DRC akihutubia leo Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA79 jijini New York, Marekani.

Tweet URL
Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kulaani vikali vitendo hivi na kuweka vikwazo dhidi ya Rwanda kutokana na uhusika wake wa kuleta uvunjifu wa amani. Tunataka kuondolewa mara moja na bila masharti kwa wanajeshi wa Rwanda katika eneo letu. Ingawa mipango ya hivi karibuni ya kidiplomasia, kama vile mazungumzo ya Luanda, inatia moyo, haipaswi kwa vyovyote kuficha uharaka wa hatua hii muhimu.
 
Aidha Tshisekedi amelieleza Baraza kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imejitolea kikamilifu kuanzisha amani ya kudumu mashariki mwa nchi hiyo na kukuza maendeleo ya kiuchumi na vile vile ustawi wa kijamii wa jamii zilizoharibiwa na vita hivi. Hata hivyo, haifungi mlango wa fursa yoyote ambayo itailetea amani hii huku ikiwa haitenganishi mamlaka yake, hata chini ya uadilifu wake wa kimaeneo.
 

Nia ya kutekeleza mazungumzo ya Luanda

 
Kwa kuzingatia hili, “DRC imejitolea kwa dhati katika utekelezaji mpango uliopitishwa kama sehemu ya mchakato wa Luanda, ambayo ninaiunga mkono kwa dhati, ambayo inahamasisha mazungumzo ya ngazi ya juu yenye lengo la kurejesha imani kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda, wakati ikipunguzwa hatari kwamba mzozo wa sasa wa usalama unaweza kuongezeka na kuwa mzozo wa kikanda. Zaidi ya hayo, nchi yangu bado iko wazi kwa mpango mwingine wowote kutoka kwa wadau wetu ambao unaweza kuchangia katika kufikia lengo hili zuri la amani. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inathibitisha tena nia yake thabiti ya kuhakikisha amani ya kudumu.”
 

Mpango wa kupokonya silaha

 
Chini ya uongozi wangu, tumedhamiria kuendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kupokonya Silaha, Uondoaji, Urejeshaji wa Jamii katika hali yake na Uimarishaji, P-DDRCS, ambalo ni jambo muhimu katika mkakati wetu wa kitaifa wa kuwapokonya silaha, kuwaondoa na kuwaunganisha tena wapiganaji katika jamii, kwa kuwapa matarajio ya kiuchumi na endelevu; huku tukiimarisha maeneo yaliyoathiriwa na migogoro. Kwa kuhakikisha mabadiliko ya baada ya MONUSCO, pia tunatanguliza uondoaji wa wapiganaji wa kigeni. P-DDRCS ni kichocheo muhimu cha amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na ninawaalika washirika wetu na marafiki kuunga mkono.