Hatutanyamaza wakati ubaguzi wa rangi unafanywa dhidi ya wengine: Ramaphosa
Hatutanyamaza wakati ubaguzi wa rangi unafanywa dhidi ya wengine: Ramaphosa
Masuala ya UM
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa leo ameuambia mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba taifa lake limefaidika na wimbi la mshikamano wa kimataifa katika vita vya kukomesha ubaguzi wa rangi na kuanzisha enzi mpya ya kidemokrasia.
Katika hotuba yake kwa mjadala mkuu huo wa kila mwaka wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu amesema, "Hadithi ya Afrika Kusini inatoa ushahidi wa jukumu la kudumu la Umoja wa Mataifa katika masuala ya kimataifa. Katika kuunga mkono mapambano yetu, Umoja wa Mataifa ulithibitisha kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa za haki za kimsingi za binadamu, utu na thamani ya kila mtu, na haki sawa kwa mataifa makubwa na madogo."
Wakati mapambano ya kihistoria ya nchi yake ya kupata demokrasia inayostawi yakiwa akilini mwake, Rais Ramaphosa amesisitiza kwamba “Sisi Waafrika Kusini tunajua jinsi ubaguzi wa rangi ulivyo na asilani hatutakaa kimya na kutazama jinsi ubaguzi wa rangi unavyofanywa dhidi ya wengine huko Gaza huku Israel ikiendelea kutoa adhabu ya Pamoja kwa Wapalestina.”
Alitoa wito wa kuwepo kwa juhudi za pamoja kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa kukomesha mateso ya raia na hatua za kisheria za Afrika Kusini zilizochukuliwa dhidi ya Israel kupitia Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ zifuate.
Suluhu ya kudumu ni kuwa na taifa la Palestina
Rais Ramaphosa amesisitiza kuwa "Suluhu pekee ya kudumu ni kuanzishwa kwa taifa la Palestina ambalo litakuwepo bega kwa bega na Israel na Jerusalem Mashariki kama mji mkuu wake".
Katika masuala mengine, amesema ni lazima kila juhudi zichukuliwe kuleta amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Sudan, Yemen, Ukraine na eneo la Sahel, lakini yote yanahitaji uwakilishi wa kweli na Baraza la Usalama shirikishi.
“Baraza la Usalama lazima lifanyiwe mageuzi kwa haraka. Lazima liwe jumuishi zaidi ili sauti za mataifa yote zisikike na kuzingatiwa.”
Ameongeza kuwa, "Afrika iko tayari kutekeleza jukumu lake katika kujenga utaratibu salama wa kimataifa kwa kushiriki katika kazi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa misingi ya heshima na kukubalika."
Rais Ramaphosa amesema kama sehemu ya kutafuta mfumo salama wa dunia ni lazima kuwe na ushirikiano mkubwa kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika ili kutatua chanzo cha vita katika bara hilo.