Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afya na ustawi wa vijana barubaru ni muhimu kwa mustakbali wa vizazi vijavyo - WHO

Kundi la wanawake vijana waliovaa shati la bluu UNICEF na KFW wakipiga picha nchini Chad. Mwanamke mmoja katikati anaunda umbo la moyo kwa mikono yake.
© UNICEF/Frank Dejongh Uchechemuzi wa vijana duniani unatarajiwa kuchochewa zaidi na miradi ya kimataifa ya uhamasishaji vijana pamoja na uhakika wa afya bora.

Afya na ustawi wa vijana barubaru ni muhimu kwa mustakbali wa vizazi vijavyo - WHO

Afya

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) imebainisha kuwa uwekezaji wa haraka unahitajika ili kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoongezeka kwa vijana barubaru na kuhakikisha mahitaji ya afya ya akili, afya ya uzazi, na afya ya ngono kwa vijana bilioni 1.3 duniani kote yanatimizwa. Kulingana na ripoti hiyo, ujana ni hatua ya kipekee na muhimu katika maendeleo ya binadamu, ambapo misingi ya afya bora ya muda mrefu huwekwa.

"Kuhamasisha na kulinda afya na haki za vijana ni muhimu kwa kujenga mustakabali bora kwa dunia yetu," amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus huku akionya kuwa kushindwa kushughulikia vitisho vya kiafya vinavyowakabili vijana  baadhi vikiwa vimekuwepo kwa muda mrefu na vingine vikiwa vipya kutaleta athari kubwa kwa vijana wenyewe na kusababisha gharama kubwa kwa jamii. "Hii inafanya uwekezaji katika huduma na programu za afya ya vijana kuwa si tu jambo la kimaadili bali pia ni jambo lenye maana kiuchumi," ameongeza.

Ripoti hiyo imezinduliwa pembezoni mwa mkutano wa mustakabali wa Umoja wa Mataifa na inabainisha mwelekeo wa wasiwasi katika afya ya vijana kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, ikionesha hitaji la hatua za haraka.

Takribani kijana mmoja kati ya vijana 7 duniani wanakabiliwa na matatizo ya afya ya akili kama vile unyogovu na wasiwasi. Aidha, kiwango cha upungufu wa damu kwa wasichana vijana hakijabadilika tangu mwaka 2010, huku karibu kijana mmoja kati ya vijana 10 wakiwa wanakabiliwa na utipwatipwa. Maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STIs), ikiwa ni pamoja na kaswende, klamidia, na virusi vya malengelenge ya sehemu za siri, yanazidi kuongezeka, hali ambayo inahitaji tiba mapema ili kuepusha athari za muda mrefu kwa afya.

Vile vile, ghasia, ikiwemo uonevu, huathiri mamilioni ya vijana kila mwaka, na kuwa na athari mbaya kwa afya zao za kimwili na kiakili.

Wasiwasi umetanda

Kwa wasiwasi zaidi, juhudi za kuzuia vijana kupata huduma za afya ya uzazi zimeongezeka, huku sera zinazozuia upatikanaji wa huduma za magonjwa ya zinaa na VVU kwa vijana zikiendelea kutekelezwa. Hatua hizi zinapunguza mwitikio wa vijana kutafuta huduma, hali inayosababisha athari za kiafya za muda mrefu.

Ripoti hiyo pia inasisitiza changamoto nyingine kubwa zinazokabili mustakabali wa vijana, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, migogoro, na ukosefu wa usawa. Hata hivyo, waandishi wa ripoti hiyo wamebainisha kuwa mafanikio yanawezekana kupitia uwekezaji sahihi na msaada.

Mafanikio kama vile kupungua kwa maambukizi ya VVU miongoni mwa vijana, kupungua kwa mimba za utotoni, na kupungua kwa vitendo vya ukatili kama vile ukeketaji na ndoa za mapema ni matokeo ya juhudi za pamoja. Aidha, ongezeko la wasichana wanaosalia shuleni limechangia katika kuboresha afya za vijana, na tangu mwaka 2000, idadi ya watoto wa umri wa sekondari wasio shuleni imepungua kwa karibu asilimia 30.

Wito wa ripoti hiyo

Kwa kuzingatia changamoto hizi, ripoti inatoa wito wa uwekezaji zaidi katika afya na ustawi wa vijana, kwa kuzingatia masuala ya elimu, huduma za afya, na lishe bora. Waandishi wanasisitiza umuhimu wa kuweka sheria na sera zinazolinda haki za vijana, huku mifumo ya afya ikitakiwa kuwa rafiki kwa mahitaji yao maalumu.

"Vijana wana uwezo mkubwa wa ubunifu wanapopewa fursa ya kushiriki katika maamuzi kuhusu ustawi wao na mustakabali wao," amesema Rajat Khosla, Mkurugenzi Mtendaji wa Ushirikiano wa Afya ya Mama, Watoto wachanga, na Watoto (PMNCH) na kuongeza kuwa "Viongozi lazima wasikilize sauti za vijana na kuhakikisha wanakuwa washirika muhimu katika maamuzi."

Viongozi wa dunia, katika mkutano wa Afya Duniani mwaka huu, wameahidi kuongeza juhudi za kuboresha afya ya vijana, ikiwa ni sehemu ya ahadi zao katika mkataba wa mustakabali wa Umoja wa Mataifa. Utekelezaji wa ahadi hizi utakuwa muhimu katika kulinda na kuboresha afya na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.