Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjadala Mkuu wa UNGA79 wang’oa nanga leo New York

Philemon Yang, Rais wa Baraza Kuu, atangaza kufungwa kwa Mkutano wa Kilele wa Wakati Ujao kutoka jukwaani.
UN WebTV Philemon Yang, Rais wa Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la UN, UNGA79

Mjadala Mkuu wa UNGA79 wang’oa nanga leo New York

Masuala ya UM

Mjadala Mkuu wa mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA79 unaanza leo kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani ikiwa ni baada ya kutamatika kwa Mkutano wa Zama Zijazo, SOTF.

Kaulimbiu ya kikao hiki cha Septemba, cha 79, ni “Hakuna kumwacha yeyote nyuma: kushirikiana ili kuendeleza amani, maendeleo endelevu na utu wa binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.’’ Katika maamuzi yaliyofanywa kwa ushauriano mkubwa na Rais wa UNGA79, Philemon Yang, viongozi wengi wa nchi wanaweza kuirejelea kaulimbiu hii  katika hotuba zao ingawa hawawajibishwi kufanya hivyo.

Mwaka huu, mjadala huo unafanyika kwa siku sita ambapo wakuu wa nchi na serikali watatoa hotuba zao wakimulika maeneo kama vile utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGS; mabadiliko ya tabianchi; afya ya umma, ukosefu wa usawa; mahitaji ya kibinadamu, amani na usalama bila kusahau maendeleo ya teknolojia.

Viongozi pamoja na kuelezea utekelezaji wa masuala hayo kwenye nchi zao, pia wanamulika maeneo ya vipaumbele kwa nchi zao.

Utaratibu wa utoaji wa hotuba

Kwa mujibu wa ratiba ya mwaka huu, Rais wa Baraza Kuu ambaye mwaka huu ni Philemon Yang kutoka Cameroon, atafungua kikao na kisha atampatia fursa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuhutubia ili kutoa taarifa ya utendaji wa shirika.

Baada ya Guterres, Rais wa UNGA atarejesha kikao katika Ajenda ya kutoa hotuba za Mjadala Mkuu na atahutubia kwa wadhifa wake.

Kisha nchi wanachama zinaanza kutoa hotuba ambapo kwa kawaida, na angalau tangu kikao cha 10 cha Baraza Kuu mwezi Septemba 1955, Brazil ndiyo iliyokuwa ikifungua mjadala. Kulingana na Huduma za Itifaki na Mawasiliano za Umoja wa Mataifa, awali, katika siku za mwanzo za mjadala, hakuna nchi ilitaka kuwa ya kwanza kuzungumza, na mara kadhaa Brazil ilichukua jukumu hilo.

Marekani, kama nchi mwenyeji wa Umoja wa Mataifa, ndiyo inayofuata kwenye jukwaa na ratiba inaonesha itafuatia Uturuki na nchi zingine zitaendelea.

Kwa kipindi cha asubuhi leo, kutoka Afrika nchi zitakazohutubia ni Afrika Kusini,  Sierra Leone na Angola. Baadaye mchana ni Nigeria na Morocco.

Mpangilio wa hotuba wa nchi wanachama 191 zingine unazingatia vigezo kama vile uwiano wa kijiografia pamoja na kiwango cha uwakilishi na mapendeleo yao kwa mfano, kiongozi wa nchi huenda asiwe New York mwanzoni mwa mjadala.

Mjadala mkuu ni nini?

Mjadala mkuu ni mkutano wa kila mwaka wa viongozi wa nchi na serikali unaolenga nchi wanachama 193 za Umoja wa Mataifa, ambao hufanyika mwezi Septemba mwanzoni mwa mwaka mpya wa Baraza Kuu,  UNGA. Mwaka wa Baraza Kuu huanzia Septemba hadi Septemba.

Kwa kawaida, huu ndiyo mjadala wa kwanza wa kikao hicho na, mbali na mikutano mingine ya ngazi ya juu inayofanyika kwa wakati mmoja, huu pekee ndio viongozi wakuu wa nchi na serikali hushiriki mara kwa mara.

Je, ni mjadala halisi kweli?

Hapana, si mjadala halisi. Mjadala mkuu unawapa wawakilishi wa nchi wanachama wote na baadhi ya mashirika mengine fursa ya kutoa hotuba katika mazingira ya heshima ya Ukumbi wa Baraza Kuu.

Hakuna mazungumzo au mjadala wa moja kwa moja baada ya hotuba yoyote. Hata hivyo, Nchi Wanachama zina haki ya kujibu hoja zinazoweza kuwasilishwa na nchi moja dhidi ya nyingine, na hii inafanywa kwa barua inayoandikwa na kiongozi wa nchi.

Barua hiyo hutumwa kwa Katibu Mkuu, ambaye ataisambaza kwa nchi zote wanachama. Wakati wa mjadala mkuu, taarifa zinazozingatia haki ya kujibu hutolewa mwishoni mwa kila siku.

Mbali na Nchi Wanachama, zingine zilizoalikwa kushiriki ni nchi zenye hadhi ya waangalizi zisizo wanachama, ambazo ni Holy See (Vatican) na Palestina, pamoja na Muungano wa Ulaya (EU), ambazo zina hadhi ya waangalizi katika Umoja wa Mataifa.

Fuatilia mubashara hotuba za viongozi kwa kubofya hapa.