Tumechoka na maneno ya viongozi sasa tunataka vitendo - Vijana
Tumechoka na maneno ya viongozi sasa tunataka vitendo - Vijana
Tunachotaka sasa ni kuona vitendo tumechoka na maneno, na hakuna jambo letu bila sasa. Ni maneno yaliyotamkwa na vijana waliozungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa baada ya viongozi w anchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa kupitisha Mkataba wa Zama Zijazo ulioambatana na Mkataba wa Kimataifa wa Dijitali na Azimio kwa ajili ya Vizazi Vijavyo.
Nyaraka hiyo ilipitishwa Jumapili kupitia azimio namba A/79/L.2 ikiwa ni baada ya miaka mitatu ya majadiliano na miezi kadhaa ya mashauriano.\
Mkataba unajumuisha nini?
Mkataba unalenga kukabili changamoto za karne ya 21 kuanzia mizozo, mabadiliko ya tabianchi, haki za binadamu, hadi taarifa potofu na za uongo.
Maeneo Matano makuu ni pamoja na maendeleo endelevu, amani na usalama duniani, sayansi na teknolojia, vijana na vizazi vijavyo na marekebisho ya usimamizi wa dunia, kipengele muhimu wakati huu ambapo taasisi za fedha za kimataifa na Umoja wa Mataifa wenyewe wameshindwa kuja na majawabu ya karne ya 21.
Mkataba wa Kimataifa wa Kidijitali unaelenga pamoja na mambo mengine usimamizi bora wa Akili Mnemba, huku Azimio kwa ajili ya Vizazi Vijavyo linataka serikali za sasa kutilia maanani vizazi vijavyo zinapopitisha maamuzi yao ya leo.
Gibson Kawago – Mchechemuzi wa nishati safi na salama kutoka Tanzania
Ni kupunguza kuongea sana na kutekeleza vitendo kwa hali ya juu. “Kwa sababu ni mara nyingi vikao hivi vinapofanyika tunafahamu, tunaingia, tunatoa hotuba, halafu tunapiga makofi. Tukishapiga makofi na kuweka mikono mfukoni, tunarudi hotelini, tunapanda ndege na kurejea nyumbani, mambo yanakuwa vile vile.”
Amesema kwa hiyo sasa hivi tupunguze kuongea sana lakini tufanye kazi zaidi, na tuhakikishe maneno yote yaliyozungumzwa miaka mitatu iliyopita, basi mwaka huu ni muda wa kufanyia vitendo zaidi.
Monica Malith – Kijana kutoka Sudan Kusini anayeishi Kenya
Monica ni kijana mkimbizi kutoka Sudan Kusini ambaye sasa anaishi na kusoma sheria Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya. Alipata fursa ya kuhutubia viongozi walioshiriki Mkutano wa Zama Zijazo. Ujumbe wake ni kwamba maneno yametosha sasa ni vitendo, lakini bado vijana hawaamini viongozi. Kwa nini?
“Viongozi wetu ni watu wa kusema na si wa kutenda. Kwa wakati huu hakuna anayewaamini. Kwa hivyo hivi sasa wakisema watende ndio tuanze kuwaamini,” amesema Monica akitolea mfano ahadi za kusaidia wakimbizi akisema, katika mitandao na hata kwenye televisheni watu wanaongelea yale watafanyia nchi au wakimbizi lakini kutenda nayo hakuna.
Ally Mwamzola kutoka asasi ya Umoja wa Mataifa Tanzania
Viongozi wametoa ahadi nyingi ikiwemo kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs yanayofikia ukomo mwaka 2030. Lakini hadi sasa yametekelezwa kwa asilimia 17 pekee. Hivyo ni vema watekeleze. Lakini katika maeneo makuu matano ya Mkataba wa Zama Zijazo akamulika vijana.
“Tunataka kuona nafasi za vijana na vizazi vijavyo zinapatiwa nafasi kubwa zaidi kuanzia kufanya maamuzi, kuanzia ngazi ya kisera lakini vile vile kupatiwa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.”
Bwana Mwamzola amesema wao kama vijana wako tayari kuhakikisha wanashikilia viongozi wa dunia ili watimize ahadi walizoziweka.
Humphrey Mrema - Mtandao wa Vijana wa Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania
Yeye amemulika ajira kwa vijana akisema “suala la ajira kwa vijana lisiwe kama ni huruma, bali wajibu wa kutimizwa na la lazima. Cha pili ni suala la uelewa. Sasa hivi tukijiuliza kuhusu vijana wana uelewa wa ujuzi wa kijani ni wachache. Mwaka jana tulikuwa na kauli mbiu ya masuala ya ujuzi wa kijani, wengi wanaujua kwa jina, lakini ni zipi na wanazipataje ni wachache.”
Jambo lingine amesema hamasa imekuwa ni ndogo, na pia teknolojia ni ndogo na mazingira wezeshi hakuna. Tunachohitaji ni hayo na yatakuja pale kutakapokuweko na rasilimali fedha na ujuzi ukafika hadi mashinani.
“Viongozi wanaweza kusema muda bado, lakini si kweli. Wanatakiwa viongozi waangalie mahitaji ya baadaye wanapotatua changamoto za sasa. Uhiari na utayari unatakiwa unatakiwa uwepo wazi na kushirikiana na sisi mezani,” ametamatisha Humphrey.
Paul Siniga – Mwakilishi wa Maendeleo Endelevu kutoka Tanzania
Mambo yanayoamuliwa na kuazimiwa ni vema yakatekelezwe, amesema Paul ambaye alielezea kauli kutoka kwa Mke wa Rais wa Namibia, Monica Geingos ya kwamba vijana wasichukuliwe kwa namna hasi.
“ Nilipata bahati kuwemo kwenye vikao na Bi. Geingos ambaye alisema ushirikishaji wa vijana usiwe kama wa bendera bali uwe na mizizi.”
Paul amesema viongozi wote wanatambua changamoto zinazokabili vijana na wanajua suluhu ni vijana. Hivyo vijana wanaweza kuwa na mtazamo chanya wa kuleta mabadiliko na maendeleo. Na hicho ndio kitu nilikipenda sana.
Hivyo amesema viongozi wanapoonda hapa wajue kwamba sisi vijana ambao tunaweza kufanya kazi na kuwa suluhu ya SDGs.