Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti: Kilichoonekana hakiwezekani sasa kinasonga – Ruto

Rais wa Kenya William Ruto akizungumza kwenye jukwaa wakati wa Mkutano wa Kilele wa Mustakabali katika Makao Makuu UN jijini New York.
UN Rais wa Kenya, William Ruto akihutubia Mkutano wa Zama Zijazo jijini New York, Marekani

Haiti: Kilichoonekana hakiwezekani sasa kinasonga – Ruto

Masuala ya UM

Rais wa Kenya, William Ruto amehutubia Mkutano wa Zama Zijazo na kusema operesheni za kikanda za ulinzi wa amani zinazofadhiliwa na Umoja wa Mataifa ni muhimu katika kutatua changamoto kubwa za sasa za ulinzi na usalama.

Amesema hayo akigusia ujumbe wa kimataifa wa kusaidia ulinzi wa amani nchini Haiti, unaoongozwa na Kenya ambao amesema alipata fursa ya kuutembelea jana huko Port-au-Prince, mji mkuu wa Haiti.

“Mwaka mmoja uliopita nilisimama hapa mbele ya mkutano na kutangaza azma ya Kenya kuchangia kwenye ujumbe wa kimataifa wa usaidizi wa usalama  nchini Haiti. Jana nilikuwa Port-au-Prince kushuhudia maendeleo makubwa yaliyofanywa na Kenya kupitia ujumbe unaoongozwa na Afrika licha ya rasilimali kidogo zilizoko.”

Amesema kile kilichoonekana kuwa hakiwezekani sasa kipo na na ni fursa halisi ya amani kwa Haiti,” amesema Rais Ruto.

Rais Ruto amezungumzia pia umuhimu wa marekebisho ya muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na harakati za Kenya za kupanda miti kama njia ya kukabili mabadiliko ya tabianchi. Amesema amezindua mradi wa kuajiri vijana 200,000 katika miradi endelevu ya umma kwa lengo la kurejesha mazingira na miundombinu.

Akagusia pia madini muhimu ambayo Afrika inayo na ambayo ni muhimu sana katika mapinduzi ya kidijitali akisema, Afrika ina madini muhimu sana kwa mapinduzi ya teknolojia lakini inapata faida kidogo.”