Wawezeshaji wenza wa mkutano wa Zama Zijazo wapongeza kupitishwa kwa makubaliano
Wawezeshaji wenza wa mkutano wa Zama Zijazo wapongeza kupitishwa kwa makubaliano
Wawezeshaji wenza wa mkutano wa mkataba wa Zama Zijazo wamepongeza juhudu zilizofanyika hadi kufikia kupitishwa kwa mkataba huo.
Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa kauli moja mkataba huo Olaf Scholz, Kansela wa Ujerumani amesema "Tunahitaji zaidi Mkataba wa Zama Zijazo hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote."
Amesisitiza kwamba mkabata huo ni dira ya kutuongoza kwenye ulimwengu bora kwani "Umethibitisha kuwa umoja wa kimataifa uko hai. Zama Zijazo zinaanza sasa."
Kesho ni ya watu wanaojipanga leo - Namibia
Naye Rais Nangolo Mbumba wa Namibia amekumbusha methali ya Kiafrika ya wahenga inenayo kwamba kesho ni ya watu wanaopanga leo.
Rais Nangolo amesema "Mkutano huu wa kilele wa Zama Zijazo ni wito wa wakati na wa haraka wa kuchukua hatua, unaotuhimiza kuchagua njia ya amani na endelevu kwa wote."
Ameongeza kuwa "Tunakusanyika hapa ili kutengeneza mustakabali bora zaidi. Matatizo ya kimataifa yanahitaji suluhu za kimataifa."
Kwa kupitisha mkataba za Zama Zijazo nchi wanachama wa UN wanaahidi, miongoni mwa mambo mengine
• Kuchagiza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Mkataba wa Paris, mikataba miwili ya kihistoria ya 2015 ambayo imeshujudia maendeleo yakisuasua na kukosa hatua muhimu.
• Kuondokana na nishati ya mafuta kisukuku katika mifumo ya nishati, kwa njia ya haki na usawa, na kuharakisha hatua katika muongo huu, ili kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo 2050.
• Kusikiliza vijana na kuwajumuisha katika kufanya maamuzi, katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
• Kujenga ushirikiano imara na mashirika ya kiraia, sekta binafsi, mamlaka za mashinani na kikanda na zaidi.
• Kufanya juhudi maradufu za kujenga na kudumisha jamii zenye amani, umoja na haki na kushughulikia vyanzo vya migogoro.
• Kulinda raia wote katika vita.
• Kuharakisha utekelezaji wa ahadi zetu kwa wanawake, amani na usalama