Vijana wataka mkataba uliopitishwa wa Zama Zijazo kuzingatia yanayowasibu
Vijana wataka mkataba uliopitishwa wa Zama Zijazo kuzingatia yanayowasibu
Vijana wamepewa fursa ya kupanda kwenye mimbari ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo kupaza sauti zao kuhusu changamoto zinazowakabili na matarajio yao kutoka kwa viongozi wa dunia wanaokutana katika mkutano huu wa ngazi ya juu wa Zama Zijazo.
Wanataka kuhakikisha kwamba viongozi wa dunia wanazingatia athari ambazo matendo yao yatakuwa nayo kwa mabilioni ya watu ambao bado hawajazaliwa karne hii, huku wakishughulikia ushirikishwaji wa vijana katika maamuzi muhimu ya kitaifa na kimataifa, ambayo ni msingi wa Mkutano huu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Zama Zijazo.
Lazima uwe mabadiliko unayotaka kuona: Mjumbe wa vijana kutoka Qatar
Mwakilishi wa Vijana wa Umoja wa Mataifa Ghanim Mohammed Al Muftah kutoka Qatar amesema anawashirikisha baadhi ya yale anayoyajua binafsi akizungumza kama mtu mwenye ulemavu.
"Maamuzi tunayofanya leo hayahusu tu sera, yanahusu kuunda ulimwengu ambapo watoto wote wanaweza kustawi katika zama zijzo zilizo jumuishi, salama na endelevu."
Ameyasema hayo huku akiangaza huku na kule ndani ya chumba cha mkutano na kusema "Sioni mtu mwingine anayefanana na mimi", lakini alijiona amekubalika bila upendeleo.
Ameongeza kuwa nyote mmenikubali mimi na ulimwengu ambao haki zake za msingi zinathaminiwa lakini, hakuna chaguo kwa watoto wanaoishi katika eneo la vita.
"Suala liko mikononi mwetu kukomesha ghasia huko Gaza," amesema, akitoa wito wa kukomesha mateso na kuwataka viongozi wote kuwasikiliza watu na kuendesha mabadiliko yenye maana.
Amehitimisha akisema “Zama zinazjo ni za vijana wetu. Ni lazima tuhakikishe kuwa wamejitayarisha kuchukua nafasi za uongozi ili kuwa waleta mabadiliko. Lazima uwe mabadiliko unayotamani kuyaona katika ulimwengu huu.”
Janga la wakimbizi halipaswi kupewa kisogo
Naye Monicah Malith, mkimbizi kutoka Sudan Kusini aliyepata fursa ya elimu akiwa kambini nchini Kenya amesema fursa kwa wakimbizi ni finyu na huu ni wakati wa kuyapa kipaumbele madhila yanayowakabili hasa suala la elimu na ujumuishwaji.
Malith amesema “Janga la wakimbizi ni moja na changamoto kubwa sana katika zama hizi na dunia inapaswa kutambua kwamba hakuna aliyetaka kuwa mkimbizi isipokuwa mazingira yamemlazimu.”
Hivyo ametoa wito kwa viongozi wa dunia kushughulikia mzizi wa masuala yanayochangia janga la wakimbizi ikiwemo vita, mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili.
Amesema “Hivi sa sa mifumo ya kimataifa ina kutu, anatoa wito wa kuwa na zama ziijazo ambazo mifumo ya kimataifa inafanyakazi Pamoja kwa ushirikiano, ikijumuisha vijana , kukomesha vita, kupata suluhu za amani , kudumisha haki zaidi, usawa, na kutoa fursa kwa wote ili kuweza kufikia uwezo wao.”
Monicah alizungumza na Idhaa ya Kiswahili kuhusu mkataba huo wa zama zijazo.