Mkataba wa Zama Zijazo wapitishwa, Katibu Mkuu asema sasa ni vitendo
Mkataba wa Zama Zijazo wapitishwa, Katibu Mkuu asema sasa ni vitendo
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha Mkataba wa Zama Zijazo baada ya kuvuta nikuvute ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameshukuru wawezeshaji wote waliojitolea kufanikisha kupitishwa kwa mkataba huo adhimu.
Akizungumza baada ya nchi kupitisha Mkataba huo, Guterres amesema “ninawashukuru wawezeshaji wenza, Rais aliyepita na wa sasa wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, nchi zote wanachama kwa ushiriki wao thabiti, ubunifu na kulegeza misimamo. Na kwa wafanyakazi wenzangu wote kwa juhudi zenu adhimu kwa miaka mitatu iliyopita.”
Tuko hapa kunusuru ushirikiano wa kimataifa
Guterres amesema aliitisha Mkutano huo wa Viongozi kuhusu Zama Zijazo ili kuzingatia marekebisho makubwa ya taasisi za kimataifa ili ziwe halali, zenye haki na fanisi kwa misingi ya Chata ya Umoja wa Mataifa.
“Niliitisha mkutano huu kwa sababu dunia yetu ilikuwa inaenda mrama na tunahitaji uamuzi mgumu ili turejee katika njia sahihi,” amesema Guterres.
Ametoa mfano kwamba rasilimali ambazo zinaweza kujenga furs ana matumaini zinawekezwa kwenye vifo na uharibifu.
Ukosefu wa usawa unazuia maendeleo endelevu, nchi nyingi zinazoendelea zinazama kwenye madeni na kushindwa kusaidia wananchi wao.
Amegusia kupitwa wakati wa Baraza la Usalama kwani Umoja wa Mataifa ulipoundwa ulikuwa na wanachama 51 na leo una wanachama 193, bado Baraza la Usalama uwakilishi wake ni wa zama zile na si sasa.
Sasa dawa imepatikana, Mkataba wa Zama Zijazo
Amesema hatimaye kwa ushirikiano na nchi wanachama na wadau wote, jawabu limepatikana nalo ni Mkataba wa Zama Zijazo, Mkataba wa Kimataifa wa Dijitali na Azimio kuhusu Vizazi Vijavyo. Amesema nyaraka hizo zitafungua njia kuelekea fursa mpya na mambo yanayowezekana.
Katibu Mkuu amesema tumefungua njia sasa ni wajibu wetu wa pamoja kupita kwenye mlango huo ambao unahitaji sio tu mkataba bali hatua.
Guterres apatia nchi wanachama changamoto
Nawataka sasa mchukue hatua. Kutekeleza Mkataba wa Zama Zijazo kwa kupatia kipaumbele mazungumzo na mashauriano ili kumaliza vita inayosambaratisha dunia yetu, na kurekebisha muundo na utendaji kazi wa Baraza la Usalama.
Ametaka pia wachagize marekebisho ya mfumo wa taasisi za fedha duniani, ikiwemo Mkutano wa mwakaji kuhusu Ufadhili kwa Maendeleo.
Halikdahalika maslahi ya binadamu yawekwe mbele katika teknolojia mpya zinazobuniwa.
Amesema tunasimama imara si kwa kupitisha mikataba bali kwa kuweka vitendo vyetu na athari zake kwa watu tunaowahudumia.
Mkataba za Zama Zijazo ni fursa ya kujirekebisha - Yang
Mkataba wa Zama Zijazo uliopitishwa unawakilisha ahadi yetu ya sio tu kutatua majanga ya sasa hivi, bali unaweka msingi wa mwenendeo wa dunia ulio wa haki na amani kwa ajili ya watu wote na mataifa yote,” amesema Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Philémon Yang alipojongea mimbari ya Baraza Kuu.
Amesema ahadi zilizomo ndani ya Mkataba pamoja na viambatanisho vyake vinaashiria utashi wa pamoja wa nchi wanachama na lazima ziongoze vitendo vyetu na zituongoze kusongesha amani na usalama duniani, kusogesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, zichochee jamii zenye haki na jumuishi na zihakikishe teknolojia mpya kila wakati zinakuwa na maslahi bora kwa wote.
Amesisitiza mshikamano na ushirikiano wa kimataifa akisema Mkutano wa Zama Zijazo ni wito wa kuchukua hatua kuunda mustakabali wetu na kujilinda sisi na sayari dunia.
Wanawake na wasichana wawe na kiti kwenye meza ya mazungumzo
Bwana Yang amekumbusha nchi wanachama kuwa maendeleo yenye maana yanahitaji ujumuishaji wa sauti zote na kwamba mataifa yote bila kujali ukubwa au utajiri lazima yawe na kiti kwenye meza ya mazungumzo.
“Umoja wa Mataifa ni shirika ambalo kila nchi ina kiti kwenye meza ya mazungumzo. Hivyo lazima tutambue kuwa hakuna lengo letu lolote litafanikiwa bila ushiriki wa wanawake na wasichana.”
Vile vile ametaja vijana na dhima yao muhimu katika ujenzi wa mustakabali ujao. “Vijana wetu ndio wabeba kurunzi ya kesho.”
Amesema kwa Afrika hilo ni dhahiri kwani vijana wengi wataingia kwenye nguvukazi kila mwaka kuliko kwenye eneo lingine la dunia.
“Kwa pamoja hebu na tutumie fursa hii tukiwa na ujasiri na azma tunapochagiza safari kuelekea mustakabali wenye nuru kwa kila mtu.”