Madeni ni mgogoro wa maendeleo ambao haujawahi kushuhudiwa : UNCTAD
Madeni ni mgogoro wa maendeleo ambao haujawahi kushuhudiwa : UNCTAD
Malengo ya Maendeleo Endelevu
Shirika la Umoja wa Mataifa la biashara na maendeleo UNCTAD leo limezindua kampeni maalum inayoainisha gharama ya mgogoro wa madeni katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs.
Ripoti hiyo imezinduliwa kwa msaada wa kampeni ya Umoja wa Mataifa ya kuchukua hatua kwa ajili ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa Maendeleo UNDP.
Kampeni hiyo ya pamoja iliyozinduliwa mjini New York Marekani katika mkutano wa awali wa Zama Zijazo katika siku za kuchukua hatua na kuelekea wiki ya ngazi ya juu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa itasisitiza jinsi nchi zinazoendelea zinavyobeba mzigo mkubwa kutokana na kuongezeka kwa madeni ya umma duniani.
Nchi zinazoendelea zinabeba mzigo mkubwa
Deni la umma duniani kwa mujibu wa UNCTAD limeongezeka zaidi ya mara mbili, kutoka dola trilioni 51 mwaka wa 2010 na huenda likapita dola trilioni 100 mwaka huu wa 2024 na nchi zinazoendelea zinadaiwa karibu theluthi moja ya deni hili
UNCTAD inasema na deni lao linaongezeka mara dufu kuliko katika mataifa yaliyoendelea huku katika baadhi ya nchi za Afrika, deni linazidi asiilimia 60 ya Pato la Taifa
Na kwa baadhi ya nchi zinazoendelea shirika hilo linasema zinaweza kulipa viwango vya riba hadi mara 12 zaidi kuliko katika mataifa yaliyoendelea kiviwanda na ni watu, na si masoko, ndio wanalipa gharama.
Kwa mujibu wa shirika hilo “Leo, watu bilioni 3.3 wanaishi katika nchi
zinazogharamika zaidi kwenye riba ya madeni kuliko kwenye
elimu afya au uwekezaji katika mabadiliko ya tabianchi. Nchi zinazoendelea hazipaswi kuchagua kati ya kulipa deni au kuhudumia watu wao.”
Mfumo jumuishi wa kifedha wahitajika haraka
Mfumo wa kifedha wa kimataifa ulio jumuishi zaidi kwa wote unahitajika haraka limesema shirika la UNCTAD na kwamba nchi zinazoendelea lazima ziwe na kiti kwenye meza katika taasisi za fedha za kimataifa
Pia limeongeza kuwa utaratibu wa kina wa kurekebisha madeni ni muhimu katika kurejesha uhimilivu wa deni la umma
Zaidi yah apo “Kusimamishwa kwa ulipaji wa madeni kunapaswa kuwa chaguo kwa nchi zilizo katika shida”
Limesema Shirika la Fedha la Kimataifa lazima liongeze mikopo ya dharura na kusimamisha malipo ya ziada.
Benki za maendeleo za kimataifa zinahitaji kutumia dola bilioni 500 kila mwaka kwa maendeleo.
Mfumo wa sasa wa kifedha duniani uliundwa miaka 80 iliyopita.
UNCTAD pia imemulika masuala ya ufadhili kwa ajili ya maendeleo na malengo ya maendeleo endelevu pamoja na changamoto za kimazingira katika Uchumi wa kidijitali.