Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani inashambuliwa, raia wanatapatapa - Guterres

Wavulana wawili wadogo wakibeba makopo ya mitungi yaliyojaa maji kutoka sehemu ya usambazaji katika kambi inayoungwa mkono na UNICEF huko Bulengo, karibu na Goma, DRC.
© UNICEF/UNI418288/Ndebo Vijana wawili wakiwa wamebeba madumu ya maji baada ya kuteka maji kutoka kituo cha kuteka maji kilichojengwa na UNICEF na wadau wake kwenye kambi ya Bulengo magharibi mwa mji wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Amani inashambuliwa, raia wanatapatapa - Guterres

Amani na Usalama

Kila tunakoangalia, amani inashambuliwa, kuanzia Gaza, hadi Sudan, hadi Ukraine na kwingineko tunaona, raia wakishambuliwa, nyumba zinasambaratishwa, raia wenye kiwewe, hofu ambao wamepoteza kila kitu – na wengine kila mtu.

Tweet URL

Ndivyo alivyoanza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwenye ujumbe wake wa siku ya amani duniani hii leo Septemba 21 maudhui yakiwa kupanda na kupalilia utamaduni wa amani.

Siku ya kimataifa ya amani ilianzishwa mwaka 1981 na azimio namba A/Res/36/67 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo miongo miwili baadaye, yaani mwaka 2001 Baraza hilo lilitambua siku hii kuwa siku ya kutokuweko kwa vurugu na kuweko kwa sitisho la mapigano.

Guterres anasema tabia ya kushambulia amani ni tabia ya machungu ya binadamu na ni “lazima ikome kwani dunia yetu inahitaji amani. Amani ni tuzo kubwa zaidi ya ubinadamu.”

Katibu Mkuu anasema , kama Siku ya Amani Duniani kupitia ujumbe wake inavyotukumbusha – majawabu yamo mikononi mwetu.

Nafasi za mgawanyiko na kudhoofika zigeuzwe kuwa haki na usawa

Anafafanua kuwa kukuza utamaduni wa amani inamaanisha mgawanyiko, kudhoofisha na kukata tamaa vinakuwa haki, usawa na matumaini kwa wote.

Guterres anasema kuwa jambo hilo linamaanisha kuwa kujikita katika kuzuia mizozo. Kuchagiza Malengo ya Maendeleo Endelevu, kuendeleza haki za binadamu na  kutatua aina zote za ubaguzi na chuki.

Nafasi ya mkutano wa Zama Zijazo

Katibu Mkuu amerejelea mkutano wa mwezi huu wa Zama Zijazo kuwa ni fursa muhimu mno ya kusongesha malengo haya.

Hivyo amesema, hebu tutumie fursa hii.Kwa pamoja, tuweke msingi wa amani. Na hebu tukuze utamaduni ambamo usawa, amani na haki vinastawi.