Vijana watanabaisha mustakbali wautakao katika mkutano wa awali wa Zama Zijazo
Vijana watanabaisha mustakbali wautakao katika mkutano wa awali wa Zama Zijazo
Mkutano wa awali wa Umoja wa Mataifa wa Zama Zijazo leo umeng’oa nanga kwenye makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani kwa vijana kutamalaki kuzungumzia mustakabali wanaoutaka.
Chini ya mauadhui “Vijana wanaongoza mustakbali” au #YouthLead the future, mengi yamezungumziwa yanayohusu ujumuishwaji wa vijana katika kila Nyanja ili kuhakikisha dunia inakuwa na Zama Zijazo mbazo kwamo vijana wanahisi kushirikishwa, kujumuishwa na kuamua mustakbali wao.
Mkutano wa Zama Zijazo siku za kuchukua hatua umeitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na unafanyika leo tarehe 20 na kesho 21 Septemba 2024 ili kutoa fursa za ziada za ushiriki wa wahusika wote.
Umewaleta pamoja wawakilishi kutoka nchi wanachama, mashirika ya kiraia, sekta ya kibinafsi, wanazuoni, mamlaka za mitaa na kikanda, vijana, na wadau wengine wengine wengi.
Mkataba wa Zama Zijazo
Wadau hawa wote wamechukua jukumu muhimu katika kuunda Mkataba wa Zama Zijazo na itakuwa muhimu kwa utekelezaji wake.
Siku zhizi za kuchukua hatua zinaongozwa na vijana baada ya ufunguzi leo kesho Jumamosi Jumamosi kutakuwa na mada kuu tatu zitakazopewa kipaumbee ambazo ni “Masuala ya kidijitali na teknolojia, amani na usalama, na maendeleo endelevu na ufadhili.”
Mbali na mada hizo tatu, pia kutakuwa na mwelekeo wa kujitolea siku nzima kwa vizazi vijavyo.
Katika hotuba ya ufunguzi Msidizi wa kwanza kabiwa wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya vijana Felipe Paullier, amesema “Hii ni fursa muhimu kwa dunia kutambua na kuthamini mchango wa vijana, kufungua milango ya kukumbatia mchango wao katika masuala mbalimbali yayowahusu vijana kuanzia elimu hadi afya, amani hadi maendeleo wanachohitaji ni kushirikishwa.”
Ameongeza kuwa “Ingawa vijana wanasalia kuwa kizazi chenye imani zaidi katika mfumo wa kimataifa, tuna hatari ya kuwapoteza kama washirika ikiwa hatutatimiza makubaliano haya."
Amesisitiza kuwa "Visingizio vya kutokomesha janga la mabadiliko ya tabianchi, vita, watu kufurushwa, na mwishowe, upotezaji wa vizazi unakwisha. Ikiwa tumekusanyika hapa vijana kutoka ulimwenguni pote, wakuu wa nchi, wawakilishi kutoka mashirika ya kiraia, mawaziri, mabalozi, wanazuoni, sekta za umma na za binafsi ni kuacha kabisa mwelekeo huu na kuchukua hatua.”
Aliendelea kusema kwamba “Jumapili, Mkutano wa Kilele wa Zama Zijazo utaanza, na nina matumaini na imani kwamba Siku hizi za kuchukua hatua zitachagiza mabadiliko chanya tunayohitaji. Hiyo ndiyo nia ya siku hizi mbili tunazozianza.”
Ametoa vito kwa vijana kukumbatia fursa na kupaza sauti zao ili mawazo, fikra na mchango wao utambulike.
Vijana ndio nguzo ya malengo yetu
Pia katika ufunguzi huo, José Maria Pereira Neves, Rais wa Jamhuri ya Cabo Verde almesema, "Vijana wako mstari wa mbele katika malengo yetu na lazima wawe sehemu muhimu ya suluhu tunazofuata kama nguvu zinazoongoza kwa uongozi, mabadiliko na hatua.”
Ameongeza kuwa “vijana inakuwa sio tu kipaumbeleni hitaji la dharura kwa wahusika wote, serikali na wasio wa serikali."
Amehitimisha, kwa kusema "Mkutano huu ni wa kipekee na utakumbukwa kama mkutano wa vijana unaolenga vijana, vijana, na vijana na utafungua sura mpya na shirikishi zaidi katika mshikamano wa kimataifa."
Kikao cha ufunguzi kimelenga kuchagiza msukumo na hatua za kuendeleza ushiriki wa vijana katika Umoja wa Mataifa na kwingineko kama suala muhimu kwa sekta zote na watendaji.
kikao cha ngazi ya juu kitaanza Jumapili ambapo washiriki ni pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali, Mawaziri, maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa akiwemo Katibu Mkuu, Washindi wa Tuzo ya amani ya Nobel na wawakilishi kutoka sekta binafsi, mashirika ya kiraia na watendaji wengine.