Israel ondokeni katika eneo la Palestina mnalolikalia kwa mabavu – Baraza Kuu UN
Israel ondokeni katika eneo la Palestina mnalolikalia kwa mabavu – Baraza Kuu UN
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Jumatano Septemba 18 jijini New York, Marekani limepitisha azimio la kuitaka Israel "ikomeshe bila kuchelewa kuwepo kwake kinyume cha sheria" katika eneo la #Palestina linalokaliwa kwa mabavu, na ifanye hivyo ndani ya miezi 12.
Kura hizo zimepigwa katikati ya kikao maalum cha dharura cha 10 kilichoanza jana Jumanne Septemba 17 kikizingatia hatua za Israel katika Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na maeneo mengine ya Eneo la Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Waliounga mkono: 124
Waliopinga: 14
Waliojizuia kupiga kura: 43
Baraza Kuu pia "linataka kwamba Israeli itii bila kuchelewa na majukumu yake yote ya kisheria chini ya sheria za kimataifa, pamoja na yale yaliyoainishwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki, hasa kwa:
(a) kuviondoa vikosi vyake vyote vya kijeshi katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ikijumuisha anga na eneo la bahari;
na (b) kukomesha sera na mazoea yake haramu, ikiwa ni pamoja na kusitisha mara moja shughuli zote zaidi za makazi, kuwahamisha walowezi wote kutoka eneo linalokaliwa kwa mabavu la Palestina na kubomoa sehemu za ukuta uliojengwa na Israel ambazo ziko katika eneo hilo, na kufuta sheria zote na hatua za kuunda au kudumisha hali hiyo haramu."
Rasimu ya azimio hilo, iliyodhamini kwa pamoja na zaidi ya nchi 20, iliwasilishwa kwa Baraza Kuu na Riyad Mansour, Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa.