Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki za binadamu zizingatiwe kwenye matumizi ya madini muhimu kama kobalti

Mtazamo wa angani wa mgodi mkubwa wa shimo wazi ukiwa na malori kadhaa mazito ya kubeba mizigo na kifaa cha kuchimba visima kinachofanya kazi kwenye eneo lenye vumbi na lililochimbwa.
© Unsplash/Bruna Fiscuk Uchimbaji madini ya shaba huko Chuquicamata, Chile.

Haki za binadamu zizingatiwe kwenye matumizi ya madini muhimu kama kobalti

Haki za binadamu

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu wamekaribisha msisitizo wa Jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutaka haki za binadamu zizingatiwe wakati wa kipindi cha kuhama kutoka nishati kisukuku kwenda kutumia madini yasiyo na madhara kwa mazingira kama vile Cobalt na Nikeli.

Kupitia taarifa yao iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na ofisi  ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR, wataalamu hao wametaka haki za binadamu zizingatiwe kwenye mnyororo mzima wa thamani ya madini hayo.

“Tunakaribisha kipaumbele kilichowekwa cha haki za binadamu na Jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Madini Muhimu ya Mpito wa Nishati,” wamesema wataalamu katika taarifa yao iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na ofisi  ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR.

Ripoti ya Jopo hilo iitwayo "Resourcing the energy transition," imetoa mwongozo wa haki na usawa katika mzunguko wa maisha wa madini muhimu kwa mpito wa nishati, na ripoti ilizinduliwa tarehe 11 Septemba 2024.

"Nchi zina jukumu la kutumia kanuni ya tahadhari na kutambua haki za jamii za asili pamoja na haki za wakulima, ambao haki zao zinakabiliwa na athari kubwa za uharibifu wa mazingira," wanasema wataalamu hao.

Pia, wataalamu wanabainisha kuwa wafanyabiashara wanapaswa kuheshimu haki za binadamu kwa kuzingatia Kanuni za Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na haki za binadamu. "Wafanyabiashara lazima watathmini hatari za ukiukwaji wa haki za binadamu katika minyororo ya thamani ya madini na kuchukua hatua stahiki kuzuia ukiukwaji huo," wameongeza wataalamu hao.

Aidha, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa kufanya tathmini za kina kabla ya kuanza shughuli za madini ili kuhakikisha kuwa zinazingatia haki za binadamu na viwango bora vya kisayansi. Ushirikishwaji wa jamii husika ni muhimu katika kuepuka ukiukwaji wa haki katika sekta hii.

Ripoti ya jopo imechapishwa  wakati ambapo kuna ongezeko la matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi zinazohusisha uchimbaji wa madini muhimu, hususani Afrika, hali inayosababisha wataalamu kuhimiza hatua za haraka ili madini haya yachangie maendeleo bila kuathiri haki za binadamu.

 

Topic: Haki za Kibinadamu
News tags: Geneva, Haki za Kibinadamu, nishati na madini

Partner: OHCHR