Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mustakbali wa kidijitali kwa wote kufungua milango ya ubunifu, teknolojia na maendeleo: ITU

Kundi la wasichana wa Kiafrika wamekusanyika kuzunguka kompyuta mpakato nchini Rwanda.
UN Women Vijana wa kike hushiriki katika warsha ya teknolojia huko Kigali, Rwanda.

Mustakbali wa kidijitali kwa wote kufungua milango ya ubunifu, teknolojia na maendeleo: ITU

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la muungano wa mawasiliano ITU linalohusika na teknolojia ya kidijitali limesema mada ya “Mustakbali wa kidijitali kwa wote” itakayopewa fursa katika mkutano wa Zama Zijazo mwishoni mwa wiki una lenga “kufungua milango ya ahadi za kutumia uvumbuzi na teknolojia zinazoibukia kwa mustakabali endelevu zaidi, ulio jumuishi na wa kuwajibika.”

Mkutano huo wa kando utafanyika Jumamosi ya tarehe 21 Septemba kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na mtandaoni chini ya mada “Mkutano wa Zama Zijazo, ufuatiliaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDG’s kidijitali.”

Ukiwa umeandaliwa na na Ofisi ya Mjumbe wa Katibu Mkuu kuhusu Teknolojia (OSET), Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano ITU na Shirika la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa UNDP, mkutano huo wa ufuatiliaji wa malengo ya SDG kidijitali ukihusisha sehemu nyingine zinazohusiana na teknolojia zinazoibukia ikiwa ni pamoja na akili mnemba AI ni msingi wa juhudi za kimataifa za kutumia uvumbuzi wa kidijitali kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa SDGs.

Washiriki wa mkutano huo

Mkutano huo utawaleta pamoja viongozi kutoka serikalini, mashirika ya kiraia, sekta binafsi, vuguvugula vijana na wanazuoni ili kuchunguza mienendo, hatari, fursa na suluhu zinazoletwa na teknolojia za kidijitali na zinazoibukia.

Mkutano wa "Mustakabali wa Kidijitali kwa Wote" unaenda sanjari na mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Mkutano wa Kilele wa Zama Zijazo ili kutoa mfano wa jinsi teknolojia za kidijitali zinavyoweza kuweka msingi wa mustakabali endelevu zaidi, unaojumuisha watu wote, na wa kuwajibika.