Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Matumaini ya wazazi kuona watoto wao wanastawi yanazidi kuyoyoma- Kaag

Sigrid Kaag, Mratibu Mwandamizi wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya kiutu na ujenzi mpya wa Gaza akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo
UN Photo/Eskinder Debebe Sigrid Kaag, Mratibu Mwandamizi wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya kiutu na ujenzi mpya wa Gaza akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo

GAZA: Matumaini ya wazazi kuona watoto wao wanastawi yanazidi kuyoyoma- Kaag

Amani na Usalama

Utu wetu wa pamoja huko Gaza uko njiapanda, amesema Mratibu Mwandamizi wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya kiutu na ujenzi mpya wa Gaza, Sigrid Kaag, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo.

Akifafanua kauli hiyo ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu wanamgambo wa Hamas washambulie Israeli, kuua na kuteka waisraeli na kisha Israeli kujibu mashambulizi na kusabaisha vita inayoendelea hadi leo, Bi. Kaag amesema huko Gaza, zaidi ya wapalestina 41,000 wameuawa, zaidi ya 93,000 wamejeruhiwa.

Takwimu za hivi karibuni za shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO zinakadiria watu zaidi ya 22,000 wamepata majeraha yanayobadili mwenendo wa maisha yao. Majeraha makubwa ya miguu yaliyosababisha watu kati ya 13 hadi 17,000 kukatwa miguu yao, ni tathmini ya machungu ya vita hii.

Takribani watoto 652,000 hawako shuleni na hivyo mustakabali wao kuwa mashakani, na matamanio ya kila mzazi ya kuona mtoto wake anastawi yanazidi kuyoyoma kwa wazazi huko Gaza, amesema Bi. Kaag.

Mustakabali wa watoto huko Gaza uko mashakani kwani kila wakati wanahamahama wakisaka pahala salama
© UNRWA Mustakabali wa watoto huko Gaza uko mashakani kwani kila wakati wanahamahama wakisaka pahala salama

Muda unayoyoma kutatua janga hili lililosababishwa na binadamu

Mratibu huyo Mwandamizi kwa Gaza ambaye hivi karibuni alikuwa Gaza, amesema muda unayoyoma tunahitajia sitisho la haraka la mapigano, kuachiliwa kwa mateka bila masharti yoyote na wahudumu wa kiutu waweze kufikisha misaada kwa wahusika bila vikwazo vyovyote. Hadi sasa waisraeli 101 kati ya 250 waliotekwa na Hamas, bado wanashikiliwa Gaza.

Amekumbusha pia miundombinu ya kiraia isishambuliwe na pande zote kwenye mzozo ziheshimu sheria za kimataifa za kiutu, akirejelea kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala hilo.

UNRWA ni uti wa mgongo wa operesheni za kiutu Gaza

Amegusia pia dhima muhimu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA katika kampeni inayoendelea ya chanjo dhidi ya polio akisema, inaonesha kazi muhimu ya UNRWA sio tu kwa mujibu wa jukumu lake, bali ni taasisi muhimu na inayoaminiwa katika muundo wa kijamii wa Gaza kama uti wa mgongo wa operesheni za kibinadamu.

Majukumu yanayoendelea kufanywa na Ofisi ya Kaag

Amesema wanaendelea kuhakikisha bidhaa za kibinadamu na kibiashara zinaingia Gaza. “Kuna maendeleo kwenye usimamizi wa maji taka na taka lakini hatua zaidi zinahitajika bado kuna uhitaji. Mathalani fedha taslimu, nishati ya mafuta na bidhaa za kujisafi zinahtajika haraka. Kuna vikwazo vya kufikisha bidhaa hizo.

Bi. Kaag ametaja pia uratibu na kupunguza  mzozo akisema Bodi ya Pamoja ya Uratibu imeundwa na inafanya kazi.

Mtoto mchanga anatibiwa katika hospitali moja huko Gaza.
© WHO Mtoto mchanga anatibiwa katika hospitali moja huko Gaza.

Kuhusu hatua ya karibuni ya wagonjwa 251 kuhamishwa nje ya Gaza, amesema ni hatua nzuri lakini haitoshi kwani bado wengine wengi wanahitaji huduma hivyo nchi wanachama zioneshe ukarimu kuwapokea.

Ametamatisha akisema msaada wa kibinadamu ni suluhisho la muda mfupi, amani ya kina na ya kudumu ndio suluhisho la kudumu kupitia jawabu la mataifa mawili, yaani Palestina na Israeli yakiishi pamoja na yakiwa huru kwa amani na usalama na wakati huo huo hoja za usalama za Israeli zizingatiwe.

Ilikuwa pia ni nafasi ya Jorge Moreira ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya  Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi, UNOPS, kuhutubia Baraza kuelezea jinsi wanavyofanikisha jukumu la Bi. Kaag kwa mujibu wa azimio namba 2720 ambalo lilitaka ofisi hiyo lihakikishe jukumu linakwenda bila vikwazo.

Mathalani walitakiwa kuwa na njia na mfumo mmoja wa kufikisha misaada Gaza kuanzia pale mdau wa kibinadamu ameonesha nia ya kupeleka msaada hadi msaada unapoingia Gaza.

Pili kushughulikia suala la ukosefu wa uhakika wa kufikisha misaada, ucheleweshaji kwenye vituo vya ukaguzi, na ukosefu wa mfumo wa kufuatilia mumbashara uingizaji wa misaada Gaza.

Na tatu ni kujenga Imani na uwazi wa uingizaji wa misaada sio tu kwenye kasi na kiasi bali upatiaji kipaumbele.

Jorge Moreira da Silva, Mkurugenzi Mtendaji wa UNOPS, anatoa taarifa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali katika Mashariki ya Kati na Palestina.
UN /Eskinder Debebe Jorge Moreira, Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya UN ya Huduma za Miradi, UNOPS akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Gaza.

Bwana Moreira amesema tayari wana njia kuu moja ya kupitisha bidhaa kupitia Jordan njia ambayo inawzesha misaada kutoka Jordan moja kwa moja  hadi Gaza, na tayari njia hiyo imejumuishwa kwenye kile kiitwacho Mfumo 2720.

Halikadhalika hivi sasa mtu anaweza kufuatilia mumbashara uingizaji wa misaada ya kiutu Gaza.

Hata hivyo amesema “Ufikishaji misaada kwa ufanisi kwa kiwango kinachotakiwa hautawezekana bila utashi wa kisiasa, hakikisho la ulinzi na usalama na mazingira yatakayowezesha hatua hiyo ifanyike,” amesema Moreira.

Amesisitiza naye pia dhima muhimu isiyohamishika ya UNRWA huko Gaza kama watekelezaji wakuu wa utashi wa pamoja.

Bi. Kaag na Bwana Moreira walikuwa wanahutubia Baraza la Usalama wakitoa maelezo kwa mujibu wa azimio namba 2720 la mwaka 2023 lililoanzisha nafasi yake Kaag na kuwataka wawe wanatoa ripoti ya utekelezaji wa jukumu la huduma za kiutu na kuikwamua Gaza.