Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Zama Zijazo: Mada muhimu za kutazamia

Watu wameketi kwenye madawati yenye rangi nyingi mbele ya Banda la SDG, eneo la sanaa katika UMOJA WA MATAIFA.
UN Photo/Mark Garten Banda la SDG katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wakati wa wiki ya majadiliano kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Mkutano wa Zama Zijazo: Mada muhimu za kutazamia

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Lengo la mkutano huu ni kubwa mno: kuunda mwongozo wa vitendo vitakavyofanikisha mustakabali bora kwa watu na sayari dunia. Ili kufanya jukumu hili liwe rahisi zaidi, waandaaji wamejikita kwenye mada kuu tano, ambazo zitajadiliwa kwa muda wa siku nne za tukio hili muhimu la Umoja wa Mataifa.

Mwisho wa mwezi Septemba kila mwaka huwa ndiyo wakati wenye shughuli nyingi zaidi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, wakati viongozi wa dunia wanapofika New York kwa mjadala wa ngazi ya juu katika Baraza Kuu. Mwaka huu, mambo sio kama kawaida – Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres atatumia fursa hii kuandaa Mkutano wa Zama Zijazo, akihusisha viongozi wa dunia, pamoja na viongozi wa asasi za kiraia na wawakilishi wa vijana.

Kutakuwa na majadiliano mengi ya jopo, hotuba kuu, na matukio ya pembeni yatakayofuatia, na haya yote yatagawanywa katika mada kuu tano, pamoja na mada “mtambuka” kama haki za binadamu, janga la mabadiliko ya tabianchi, na usawa wa kijinsia, ambazo zinahusiana na masuala yote.

Picha inayoonyesha dhana ya maendeleo endelevu, ikionyesha turbine ya upepo, paneli za jua, setilaiti, na jiji kwenye tufe.
Summit of The Future Mkutano wa Zama zijazo

1.      Ufadhili wa Maendeleo

“Muundo wa kifedha wa kimataifa, ulioanzishwa mnamo mwaka wa 1945 baada ya Vita ya Pili ya Dunia, unapata shinikizo zito la kihistoria – na unashindwa kustahimili shinikizo hilo,” anasema Katibu Mkuu wa UN António Guterres.

Hitaji la kufanyia marekebisho mfumo huu limepata dharura zaidi kutokana na kuyoyoma kwa  muda wa kufanikisha Ajenda ya 2030 kwa ajili ya Maendeleo Endelevu; ambao ni mwongozo wa kujenga mustakabali bora ulioundwa na UN.

Nyaraka kuu itakayotokana na mkutano huu, inayojulikana kama Mkataba wa Zama Zijazo, ambayo kulingana na Bwana Guterres, inawakilisha ahadi kutoka kwa  mataifa “kutumia zana zote zilizo mikononi mwetu katika ngazi ya kimataifa kutatua matatizo – kabla matatizo hayo hayajatutawala," na kujitolea kuchukua "hatua za kijasiri" ili kutekeleza ajenda, zinazolenga  hasa kumaliza njaa na umaskini; kupunguza ukosefu wa usawa; na kuongeza mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

2. Amani na Usalama wa Kimataifa

Umoja wa Mataifa umeitaja hali ya sasa ya kimataifa kuwa yenye “hatari ya kipekee,” inayokabiliwa na uwezekano wa mataifa makuu  kuingia katika migogoro kwa viwango vya juu zaidi tangu Vita Baridi, uwezekano wa kuibuka  kwa vita vya nyuklia ukiwa juu kuliko ilivyokuwa kwa miongo kadhaa, na janga mabadiliko ya tabianchi likisababisha  uhamaji na kuongeza mvutano.

Pia kuna vitisho vipya vya kukabiliana navyo, kwani teknolojia mpya zinageuzwa kuwa silaha za kuleta madhara makubwa, katika ulimwengu uliounganika kwa karibu.

Katika mazingira haya magumu, Ajenda Mpya ya Amani, ambao ndio mwongozo wa kwanza wa kimataifa wa amani ulioandaliwa na UN kwa miongo kadhaa, ulitolewa mwaka wa 2023, ukielezea suluhu mbalimbali kuanzia kujenga  na kudumisha amani hadi kupunguza silaha na marekebisho ya Baraza la Usalama.

Mapendekezo yaliyoelezwa katika Ajenda Mpya ya Amani yameingizwa katika Mkataba wa Mustakabali, ambao utaidhinishwa kwenye Mkutano wa Zama Zijazo.

Wanawake watatu vijana wa Kazakhstan wakiwa wamevaa mavazi ya usafi wanafanya kazi pamoja katika maabara ya kusanikisha satelaiti ndogo kama sehemu ya mpango wa elimu wa UniSat.
© UNICEF/Zhanara Karimova Wanawake wachanga wakishiriki katika programu ya kwanza ya maendeleo ya nanosatellite ya Kazakhstan inayolenga wanawake.

3.Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na Ushirikiano wa Kidijitali

Nchi wanachama za Umoja wa Mataifa pia zitapitisha Mkataba wa Kimataifa kuhusu Digitali, ambao unatarajiwa kuongeza uaminifu katika mtandao, kuhakikisha kuwa watu wana chaguzi zaidi kuhusu jinsi data zao zinavyotumika, na kueleza uwajibikaji kwa maudhui ya baguzi na potofu.

Mkataba huo unaonya kuhusu madhara ya kutumia akili mnemba (AI) kwa nia mbaya, kama vile kuendeleza migawanyiko ndani na kati ya mataifa, kuongeza ukosefu wa usalama, kukiuka haki za binadamu, na kuendeleza ukosefu wa usawa.

Hati hiyo inajumuisha orodha ya ahadi na hatua, baadhi yake zikilitaja tatizo la ‘ukosefu wa usawa katika ufikiaji wa kidijitali’: watu bilioni 2.6 hawana kabisa upatikanaji wa Intaneti, jambo linalowakosesha fursa zinazotolewa na zana za mtandaoni. Mkataba unatoa wito wa shule na hospitali zote kuunganishwa mtandaoni, kuwekeza kwenye Mpango wa Giga unaoungwa mkono na UN, pamoja na mafunzo ya ujuzi wa kidijitali. Jopo la Kimataifa la Sayansi kuhusu akili mnemba (AI) na Mazungumzo ya Kimataifa ya Kila Mwaka juu ya Usimamizi wa akili mnemba vitaundwa. Ifikapo 2030, mpango uliopo ni kuweka viwango vya kimataifa vya akili mnemba ambavyo vitanufaisha wote.

4. Vijana na Vizazi Vijavyo

Hati ya tatu itakayoidhinishwa katika Mkutano huo wa Zama Zijazo itakuwa Tamko kwa Vizazi Vijavyo. Aidha, ahadi za kumaliza ukosefu wa usawa, kuleta elimu bora kwa wote, na kuhakikisha mipango ya muda mrefu. Tamko hilo linapendekeza nyongeza mpya kwa UN, yaani Mjumbe Maalum wa Vizazi Vijavyo, ambaye atakuwa na jukumu la kutetea fikra zenye mtazamo wa  muda mrefu ndani ya mfumo wa UN na kushiriki matokeo ya Maabara ya Masuala ya Mustakabali ya UN, kitengo cha utafiti cha shirika hilo.

Sauti za vijana zitafungua na kufunga mkutano huo: Siku ya kuchukua hatua inayoongozwa na vijana itafanyika Ijumaa, tarehe 20 Septemba, katika ukumbi maarufu wa Baraza Kuu, ikijumuisha wanaharakati, watu mashuhuri, maonesho ya muziki, na mazungumzo itakayowahusisha Felipe Paullier ambaye Naibu Katibu Mkuu wa kwanza wa Masuala ya Vijana, na Bwana Guterres; na Jumatatu, tarehe 23 Septemba, mazungumzo shirikishi yatafanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wadhamini, kuhusu jinsi ya kuimarisha mfumo wa kimataifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katibu Mkuu UN António Guterres, Naibu Katibu Mkuu Amina Mohammed, na Guy Ryder wakishiriki katika simu ya video ya kimataifa kabla ya Mkutano wa Kilele wa Siku za Usoni katika Makao Makuu UN .
UN Photo/Manuel Elías Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati kushoto) akishiriki katika mkutano wa wito wa kimataifa wa kuchukua hatua kabla ya Mkutano wa kilele wa siku zijazo.

5. Utawala wa Kimataifa

Wakati Umoja wa Mataifa ulipoundwa karibu miaka 80 iliyopita, dunia ilikuwa katika hali ya mushtuko, kwani ilikuwa inatoka kwenye mgogoro wa kimataifa uliokuwa na uharibifu kiasi kwamba viongozi wa dunia walikuwa tayari kuunda taasisi zilizokusudia kuhakikisha kuwa hali kama hiyo haitatokea tena.

Ingawa hamasa hiyo bado ni muhimu leo, kuna makubaliano mapana kwamba zana zilizoundwa wakati wa kuanzishwa kwa UN zinahitaji marekebisho makubwa ili ziweze kutimiza madhumuni yake. Katika Mkutano huo wa Zama Zijazo, viongozi wa dunia watashiriki katika mijadala inayolenga kuleta mabadiliko haya na watajadili suala tata kuhusu moja ya zana hizo, ambalo limezua mjadala mkali kwa miaka mingi: Marekebisho ya Baraza la Usalama la UN.

Pia kutakuwa na mkazo kwenye masuala ya anga za juu. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na wito wa kuimarisha miundo ya utawala inayohusu shughuli hizi, huku matumizi ya anga za juu na sekta binafsi yakikua kwa kasi, na mataifa mapya yanayoshiriki katika uchunguzi wa anga yakijiunga na wahusika waliostawi.

Mipango mikubwa ya kimataifa ya kuanzisha uwepo wa kudumu wa binadamu kwenye mwezi inaendelea, programu za kuaminika za kuendeleza safari za watu kwenda Mars pia zinaendelea, na dhana mbalimbali za kuchimba rasilimali kutoka mwezi na ukanda wa asteroidi zinafanyiwa uchunguzi. Kwa hiyo, aina mpya za utawala zinahitajika ili kuhakikisha kwamba ukuaji huu wa haraka unafanyika kwa njia salama na endelevu.