Ushirikiano wa Kusini-Kusini unaweza kusaidia kutatua changamoto tata za maendeleo: UN
Ushirikiano wa Kusini-Kusini unaweza kusaidia kutatua changamoto tata za maendeleo: UN
Ikiwaleo ni siku ya kimataifa ya ushirikiano wa Kusini-Kusini Umoja wa Mataifa umesema ushirikiano huo ambao ni wa kati ya nchi zinazoendelea, unaweza kusaidia kutatua kile afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa amekielezea kama muktadha wa changamano za maendeleo duniani.
Akizungumza na UN News, Dima al-Khatib, Mkurugenzi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Ushirikiano wa Kusini-Kusini, ameelezea nguvu ya mabadiliko ya ushikamano kati ya nchi zinazoendelea.
Akifafanua kwa nini ushirikiano huo ni muhimu sana Dima al-Khatib amesema “Siku hizi nchi za Kusini zinakabiliana na wingi wa masuala tata ya maendeleo. Masuala hayo yamezidishwa kwa kweli, katika miaka ya hivi karibuni na janga COVD-19 na matokeo yake.”
Ameongeza kuwa nchi pia zinapambana na athari za migogoro mingi inayotokea ulimwenguni leo, iwe ya kijiografia, inayohusiana na chakula, inayohusiana na elimu au kiuchumi. Ni muktadha changamano wa maendeleo.
Ameendelea kusema kuwa ni muktadha ambapo masuala ya maendeleo yaliyopo yanahitaji ushirikiano kati ya nchi.
“Tunapozungumza juu ya mabadiliko ya tabianchi kwa mfano, hatuzungumzi juu ya nchi moja. Mabadiliko ya tabianchi, usimamizi wa maji, majanga ya asili hayajui mipaka ya kijiografia. Amani na maendeleo pia ni kitu ambacho kina pita mipaka.”
Kwa hivyo, ikiwa nchi hazishirikiani ili kuweza kushughulikia changamoto hizi , kujenga mnepo na kuzikabili itakuwa ni kupoteza fursa.
Ushirikiano baina ya Kusini-Kusini na SOTF
Akizungumzia uhusiano uliopo kati ya Kusini-Kusini na Mkutano wa Zama Zijazo Dima al-Khatib amesema” Mkutano ujao wa kilele wa Zama Zijazo ni wakati muhimu kwa sababu tuna miaka mitano mbele yetu kwa ajili ya kuafanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na tuko nyuma sana. Ni asilimia 17 pekee ndio malengo hayo yako kwenye mstari.”
Amesisitiza kuwa “Hii ni fursa ya kuibua upya dhamira yetu kwa ajenda hii ya ushirikiano wa Kusini-Kusini lakini pia kuibua upya dhamira ya kutumia mbinu hii kushughulikia masuala magumu sana ya maendeleo ambayo nchi hizo zinapambana nayo, ikiwa ni pamoja na dhahma ya madeni, mabadiliko ya tabianchi na mnepo wa afya.”
Pia amesema “Ninaamini nchi nyingi za Kusini zimetoa suluhu nyingi na zinangojea kusonga mbele kwa msaada wa nchi nyingine.”