Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwongozo hadharani ili Nikeli, Kobalti, Shaba na Lithiamu zitumike kwa manufaa ya wote

Picha ya karibu ya miamba na madini yaliyotumwa katika Australia.
© Unsplash/Paul-Alain Hunt Ore iliyo na shaba, kobalti na nikeli kwenye mgodi huko Australia Magharibi.

Mwongozo hadharani ili Nikeli, Kobalti, Shaba na Lithiamu zitumike kwa manufaa ya wote

Tabianchi na mazingira

Ukisoma kichwa cha habari unajiuliza ni kwa sababu gani? Sababu ni kwamba mahitaji ya madini hayo muhimu zaidi kwa ajili ya teknolojia za nishati endelevu yanatarajiwa kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2030.

Ni kwa mantiki hiyo hii leo jopo la watalaamu lililoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres limetoa mapendekezo na miongozo kwa serikali, viwanda na wadau wengine ili kuhakikisha fursa ya sasa ya mpito wa kuelekea matumizi ya nishati salama dunani na kuondokana na nishati kisukuku, inakuwa ya haki, usawa, endelevu na yenye uwiano.

Faida za madini hayo

Madini hayo kwa mujibu wa shirika la Umoja wa  Mataifa la Mazingira, UNEP ambayo ni pamoja na shaba, lithiamu, nikeli na kobalti ni muhimu kwenye teknolojia rafiki kwa mazingira kuanzia tabo za kuzalisha nishati kwa upepo, paneli za sola na magari ya umeme.

Jopo hilo limetoa mapendekezo na miongozo hiyo hii leo jijini New York, Marekani kupitia ripoti yao ya kwanza kabisa tangu kuundwa kwake  mwezi Aprili mwaka huu.

“Ripoti ya leo ni mwongozo wa kusaidia kuchochea ustawi na usawa sambamba na kupata nishati salama. Ripoti inatoa mapendekezo ya matumizi ya madini muhimu wakati muafaka,” amesema António Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia taarifa  yake iliyotolewa baada ya kuchapishwa kwa ripoti.

Ripoti inaainisha mbinu za kuanzisha mapinduzi ya nishati salama kwa haki na uwiano, ili yachochee maendeleo endelevu, heshima kwa watu, kulinda mazingira na kuchochea ustawi kwenye nchi zinazoendelea ambazo ni tajiri wa rasilimali, amesema Katibu Mkuu.

Jopo lifanye nini?

Sasa Guterres amewataka Wenyeviti Wenza na Jopo zima kushauriana na kushirikishana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine ripoti hiyo kabla ya mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 baadaye mwaka huu huko Baku, Azerbaijan.

Ikipatiwa jina – Ufadhili wa Mpito wa Nishati: kanuni kuongoza madini muhimu wakati wa mpito kuelekea nishati salama kwa uwiano na haki ripoti inabainisha msingi wa kuhakikisha mapinduzi ya nishati salama yanazingatia haki na uwiano ili yachochee maendeleo endelevu, ustawi kwa nchi zinazoendelea zenye utajiri wa madini hayo.

Mapendekezo ya usawa, uwazi, uwekezaji, uendelevu, haki za binadamu sio tu kule ambako madini yanachimbwa, bali kwenye mnyororo mzima wa thamani ya madini hayo. Kuanzia kuyachenjua hadi kutengeneza, kusafirisha na kurejeleza.

Kauli za wenyeviti wenza- Mapendekezo yatekelezwe

"Huu ni wakati ambapo ushirikiano baina ya mataifa ni muhimu ili mataifa yaweze kutatua majanga lukuki,” amesema Balozi Mxakato-Diseko, Mwenyekiti Mwenza wa Jopo hilo.

Kwa upande wake, Ditte Juul Jørgensen, ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Jopo amesema “tabianchi ikiwa ndio kitovu cha majanga ya sasa, kuna udharura wa kufanya kazi pamoja kukiwa na uelewa wa wazi ya kwamba tuzame pamoja au tuibuke pamoja, kwa misingi ya maadili ya pamoja ambayo yanaunganisha dunia pamoja hivi sasa huku haki za binadamu, haki na usawa na maslahi ya pande zote kwa ajili ya ustawi wa pamoja.

Amepongeza Katibu Mkuu kwa uongozi wake wa kutatua jambo hili la kuleta mabadiliko akisema hii ndio hasa ushirikiano wa kimataifa.

Lazima hivi sasa tutumie fursa ya kukuza uchumi wetu, kulinda jamii zetu, kuhifadhi mazingira yetu na kunufaika pamoja zaidi tena kwa haki huku tukitatua janga la tabianchi.

“Hatuwezi kurudia makosa yaliyopita. Natumaini tunaweza kugeuza kanuni na mapendekezo haya na kuyatekeleza.”

Jopo linahusisha wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia, wanazuoni, sekta za viwanda.