UNGA78 yafunga mlango kwa wito wa mshikamano huku UNGA79 ikifungua pazia
UNGA78 yafunga mlango kwa wito wa mshikamano huku UNGA79 ikifungua pazia
Leo septemba 10, mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78 unakunja jamvi na kuhitimisha mwaka wa misukosuko katika diplomasia ya kimataifa ukisisitiza haja ya azimio la pamoja miongoni mwa mataifa kukabiliana na changamoto kubwa za sasa.
Kikao hicho kiliambatana na mikutano na mijadala mbalimbali . Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza katika hafula ya kufunga kikao hicho mjini New York Marekani kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa hii leo amesema mwaka uliopita umekuwa na umaskini unaoendelea, ukosefu wa usawa na migogoro, akisisitiza kuwa mwaka huo pia umekuwa ni mwaka wa joto zaidi katika rekodi ya dunia.
Guterres ameangazia tumaini na msukumo katika kile kinachoweza kupatikana ikiwa jumuiya ya kimataifa itafanya kazi kama kitu kimoja. Pia amepongeza uongozi wa Rais wa Baraza Kuu wa kikao cha 78 Dennis Francis.
Amesisitiza kuwa "Changamoto zinazokabili ubinadamu wetu haziwezi kushindwa ikiwa tutashirikiana".
Bwana Guterres ameendelea kusema kuwa Umoja wa Mataifa, na mfumo wa kimataifa wenyewe, unaweza tu kuwa na ufanisi kama ahadi ya nchi wanachama inavyoruhusu.
"Tunaposherehekea mafanikio ya Mkutano wa Baraza Kuu wa 78, tuangalie pia kikao cha 79 kama wakati ambao ulimwengu unaweza kutimiza uaminifu, suluhu na amani ambayo ulimwengu wetu unahitaji."
Mwaka ulioghubikwa na matukio
Akihutubia Baraza Kuu kwa mara ya mwisho katika wadhifa huo, Rais Dennis Francis, mwanadiplomasia mkongwe kutoka Trinidad na Tobago, amekumbusha mafanikio muhimu ya kikao na kazi ya Urais wake.
"Tulianza kikao mnamo Septemba kwa wiki ya ngazi ya juu yenye shughuli nyingi ingawa ilikuwa yenye mafanikio iliyoshirikisha Mkutano wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs na majadiliano ya ngazi ya juu ya ufadhili wa maendeleo, pamoja na mafanikio mengine muhimu kwa diplomasia ya kimataifa."
Amesisitiza kwamba kipengele muhimu cha kazi yake ni kuhakikisha umuhimu wa Umoja wa Mataifa kwa wapiga kura wake bilioni nane duniani, baada ya kutembelea nchi 31 na kukutana na wadau mbalimbali kuanzia viongozi wa serikali hadi wanafunzi, wanawake, mashirika ya kiraia na familia zilizofurushwa makwao.
"Ziara zangu nchini Haiti, Sudan Kusini, na Ukraine zilikuwa za kuhuzunisha sana, kwani mataifa haya yanakabiliwa na migogoro, ukosefu wa usalama, na ukatili," amesema, akisisitiza kwamba juhudi za Umoja wa Mataifa katika maeneo haya "Kwa hakika ni za kuokoa maisha".
Rais Francis amesema Israeli, Palestina, ni masuala ya juu kabisa katika akili yangu.
Ameongeza kuwa ingawa hakuweza kukutana na Waisraeli na Wapalestina uwanjani, karibu na ukumbi wa mapambano wa mgogoro unaoendelea, "maendeleo huko yalibaki kuwa ya juu zaidi katika akili yangu."
Amesema amejadili mgogoro huo na viongozi duniani kote, akiwemo Papa Francis.
Ameonyesha matumaini ya dhati kwamba juhudi zinazoendelea za kidiplomasia zitaleta usitishaji vita, hata kama wa muda mfupi, na kwamba hii inaweza kwa njia fulani kusababisha mchakato wa kisiasa kufikia amani ya kudumu kwa ajili ya watu wa eneo hilo.
Changamoto haziko nje ya uwezo wetu
Rais wa Baraza Kuu amehitimisha hotuba yake akiwakumbusha mabalozi kwamba ingawa changamoto zinazoikabili jumuiya ya kimataifa ni ngumu, kwa hakika haziko nje ya uwezo wetu kuzishinda."
Amesisitiza umuhimu wa umoja, akihimiza mataifa kukabiliana na changamoto za kimataifa kwa rasilimali zote zilizopo ili kujenga mustakabali salama zaidi, huku akisisitiza umuhimu wa Umoja wa Mataifa kama "mojawapo ya nguvu kuu kwa ajili ya mema duniani na kwamba lazima tufanye bidii kudumisha maisha yake marefu."
Amesema “Tujitokeze kwenye hafla hiyo. Wacha tutimize ahadi tulizoahidi na tushirikiane kwa mshikamano kujenga mustakabali unaoheshimu matumaini na ndoto za watu wote na unaounganisha mataifa yote kama alivyosema wakati mmoja Nelson Mandela kwamba siku zote inaonekana kuwa ni vugumu hadi inapotfanyika."
Philemon Yang apokea kijiti
Mkutano huo pia umemshuhudia Philemon Yang, kutoka nchini Cameroon Rais Mteule wa kikao cha 79 cha Baraza Kuu akila kiapo cha kushika wadhifa wa Rais wa Baraza Kuu.
Bw. Yang ametangaza kwamba atatekeleza wajibu wake kwa uaminifu kama Rais wa Baraza, "kwa uaminifu, busara na dhamira."
Amehidi kujitolea kutumia mamlaka yake kama rais kila wakati kwa maslahi ya Umoja wa Mataifa na kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kanuni za maadili.
Rais Dennis Francis kisha alitangaza kuwa kikao cha 78 kimefungwa na kumkabidhi Rais Yang zawadi ya nyundo.
Kikao cha 79 cha Baraza Kuu kinakutana alasiri saa tisa kwa (saa za New York), huku mjadala mkuu wa ngazi ya juu wa kila mwaka wa kikao hicho utafanyika kuanzia tarehe 24 Septemba.
Pia mwezi huu wa Septemba utaghubikwa na mikutano ya ngazi ya juu ukiwemo wa vitisho vinavyotokana na kupanda kwa kina cha Bahari utakaofanyika tarehe 25 na utokomezaji wa silaha za nyuklia na usugu wa vijiua vijiumbe maradhi au antimicrobial tarehe 26 Septemba.