Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muhtasari wa habari: Dag Hammarskjöld, Gaza na UNGA

Katibu Mkuu UN Dag Hammarskjöld akizungumza na wajumbe katika sebule ya wajumbe wakati wa Kikao Maalum cha Tatu cha Dharura cha Baraza Kuu la UN .
UN Photo Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo Dag Hammarskjöld (anayesimama wa 2 kutoka kushoto) akiwa katika mazungumzo kwenye Ukumbi wa Wajumbe kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kufuatia Mkutano Maalum wa Dharura mwaka 1958.

Muhtasari wa habari: Dag Hammarskjöld, Gaza na UNGA

Masuala ya UM

Miaka 63 tangu kifo cha ajali ya ndege cha Katibu Mkuu wa pili wa Umoja wa Mataifa Dag Hammarskjöld huko Ndola Zambia, bado majibu hayajapatikana ya nini kilisababisha ajali hiyo wakati akielekea kusaka amani kwa iliyokuwa Congo, sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hii leo kwenye Umoja wa Mataifa kumefanyika kumbukizi ya kifo chake na wafanyakazi wengine aliokuwa nao, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na kumshukuru Jaji Mkuu wa zamani wa Tanzania Mohamed Chande Othman kwa kuendelea na uchunguzi, amesema,… nitaendelea kufanya kila kitu kuunga mkono kazi yake ikiwemo kushirikisha nchi wanachama. Natoa wito nchi hizo zilete taarifa mmuhimu walizo nazo. Hebu na turejelee azma yetu na ahadi ya kusaka ukweli wa kilichotokea usiku ule wa mwaka 1961.

Mfanyakazi wa afya wa kike akimpa mvulana mdogo chanjo ya polio huko Gaza.
© WHO Mtoto anapokea chanjo ya polio huko Gaza.

Chanjo ya Polio Gaza

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA limesema kampeni ya chanjo eneo la kaskazini mwa Gaza imeendelea leo jumanne licha ya tukio la jana la jeshi la Israeli kuzuia kwa saa nane msafara wa wafanyakazi waliokuwa wanasafiri kwenda kutoa huduma hiyo. Tayari maelfu ya watoto wamepatiwa chanjo hii leo kwenye eneo hilo katika kampeni itakayomalizika tarehe 12 mwezi huu.

Katibu Mkuu UN António Guterres akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la UN mjini New York.
UN Photo/Mark Garten Rais wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la UN, UNGA78 Balozi Dennis Francis akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani mwishoni mwa jukumu lake hilo lililoanza mwezi Septemba mwaka jana.

UNGA78/79

Na leo septemba 10, mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78 unakunja jamvi baada ya mwaka mzima wa mikutano na mijadala, na hivyo kuashiria kuanza kwa mkutano wa 79 au UNGA79 ambapo kuanzia tarehe 22 vitaanza vikao vya ngazi ya juu na Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu. Rais anayemaliza muda wake ni Balozi Dennis Francis kutoka Trinidad na Tobago na anayempatia kijiti ni Philemon Yang kutoka Cameroon.