Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nini cha kutarajia kwenye mjadala mkuu wa UN-UNGA79

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katika jukwaa) akihutubia ufunguzi wa kikao cha 78 cha mjadala wa kila mwaka wa Baraza Kuu.
UN Photo/Cia Pak
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katika jukwaa) akihutubia ufunguzi wa kikao cha 78 cha mjadala wa kila mwaka wa Baraza Kuu.

Nini cha kutarajia kwenye mjadala mkuu wa UN-UNGA79

Masuala ya UM

Ni wiki yenye shughuli nyingi zaidi na labda yenye hadhi kubwa zaidi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, ambapo viongozi kutoka kote ulimwenguni wanakusanyika kujadili masuala ya kimataifa au kuangazia vipaumbele maalum vya nchi zao.

Kikao cha 79 cha Baraza Kuu kinaanza katikati ya mwezi Septemba na tukio kuu kwa wengi ni mjadala mkuu wa kila mwaka. Lakini, ni nini hasa mjadala mkuu?

Haya hapa ni mambo unayohitaji kujua kuhusu mjadala unaoanza Jumanne, tarehe 24 Septemba:

Mjadala mkuu ni nini?

Mjadala mkuu ni mkutano wa kila mwaka wa viongozi wa nchi na serikali unaolenga nchi wanachama 193 za Umoja wa Mataifa, ambao hufanyika mwezi Septemba. Hufanyika mwanzoni mwa kikao cha Baraza Kuu, ambacho mara nyingi kinajulikana kama UNGA. Kwa kawaida, huu ndiyo mjadala wa kwanza wa kikao hicho na, mbali na mikutano mingine ya ngazi ya juu inayofanyika kwa wakati mmoja, huu pekee ndio viongozi wakuu wa nchi na serikali hushiriki mara kwa mara.

Afisa wa ulinzi wa usalama wa Umoja wa Mataifa amesimama chini ya ngazi za jukwaa kwenye Ukumbi wa Mkutano Mkuu.
UN Photo/Cia Pak
Afisa wa ulinzi wa usalama wa Umoja wa Mataifa amesimama chini ya ngazi za jukwaa kwenye Ukumbi wa Mkutano Mkuu.

Je, ni mjadala halisi kweli?

Hapana, si mjadala halisi. Mjadala mkuu unawapa wawakilishi wa nchi wanachama wote na baadhi ya mashirika mengine fursa ya kutoa hotuba katika mazingira ya heshima ya Ukumbi wa Baraza Kuu.

Hakuna mazungumzo au mjadala wa moja kwa moja baada ya hotuba yoyote. Hata hivyo, Nchi Wanachama zina haki ya kujibu, na hii inafanywa kwa barua inayoandikwa na kiongozi wa nchi. Barua hiyo hutumwa kwa Katibu Mkuu, ambaye ataisambaza kwa nchi zote wanachama. Wakati wa mjadala mkuu, taarifa zinazozingatia haki ya kujibu hutolewa mwishoni mwa kila siku.

Kaulimbiu ya kikao hiki cha Septemba, cha 79, ni “Hakuna kumwacha yeyote nyuma: kushirikiana ili kuendeleza amani, maendeleo endelevu na utu wa binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.’’ Katika maamuzi yaliyofanywa kwa ushauriano mkubwa na Rais wa Baraza Kuu, viongozi wengi wa nchi wanaweza kuirejelea kaulimbiu hii  katika hotuba zao ingawa hawawajibishwi kufanya hivyo.

Hugo Chávez (katikati), Rais wa zamani wa Venezuela akiwasili katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Septemba 2006.
UN Photo/Mark Garten
Hugo Chávez (katikati), Rais wa zamani wa Venezuela akiwasili katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Septemba 2006.

Nani huzungumza lini?

Katika mpangilio wa sasa, baada ya kufunguliwa kwa mkutano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hutoa taarifa, akifuatiwa na Rais wa Baraza Kuu.

Kwa kawaida, na angalau tangu kikao cha 10 cha Baraza Kuu mwezi Septemba 1955, ni Brazil ndiyo iliyokuwa ikifungua mjadala. Kulingana na Huduma za Itifaki na Mawasiliano za Umoja wa Mataifa, awali, katika siku za mwanzo za mjadala, hakuna nchi ilitaka kuwa ya kwanza kuzungumza, na mara kadhaa Brazil ilichukua jukumu hilo.

Marekani, kama nchi mwenyeji wa Umoja wa Mataifa, ndiyo inayofuata kwenye jukwaa.

Mpangilio wa hotuba wa nchi wanachama 191 zingine unazingatia vigezo kama vile uwiano wa kijiografia pamoja na kiwango cha uwakilishi na mapendeleo yao kwa mfano, kiongozi wa nchi huenda asiwe New York mwanzoni mwa mjadala.

Mbali na Nchi Wanachama, zingine zilizoalikwa kushiriki ni nchi zenye hadhi ya waangalizi zisizo wanachama, ambazo ni Holy See (Vatican) na Palestina, pamoja na Muungano wa Ulaya (EU), ambao una hadhi ya waangalizi katika Umoja wa Mataifa.

Kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi, akihutubia Baraza Kuu mnamo Septemba 2009.
UN Photo/Marco Castro
Kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi, akihutubia Baraza Kuu mnamo Septemba 2009.

Taa za tahadhari zinapowaka

Muda wa hiari wa dakika 15 kwa ajili ya kutoa taarifa hupendekezwa kwa njia isiyo rasmi wakati wa mjadala mkuu, na wazungumzaji hupewa onyo kwa njia ya taa ya mwanga mwekundu unaong'aa muda wao unapokuwa umekwisha, ingawa kamwe hawakatiziwi au kusimamishwa.

Neno kuu hapa ni hiari, na wengi, wa viongozi wa nchi huzungumza kwa muda mrefu zaidi.

Kiongozi wa zamani wa Cuba, Fidel Castro, bado anashikilia rekodi ya hotuba ndefu zaidi tangu mwaka 1960, akizungumza kwa dakika 269, au karibu masaa manne na nusu, baada ya kuahidi "tutajitahidi kuzungumza kwa kifupi."

Kumekuwa na hotuba nyingine ndefu na za muda mrefu, lakini labda zinazojulikana zaidi kwa maudhui yake badala muda wa hotuba.

529198 - israel

Mnamo mwaka wa 2006, katikati ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Marekani na Venezuela, Rais wa Venezuela, Hugo Chávez, alimuita Rais wa Marekani wakati huo, George W. Bush, kama “shetani” kutoka jukwaani.

Mnamo mwaka wa 2009, marehemu kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi, alitoa hotuba kali ya dakika 100 akilikosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nguvu ya kura ya turufu ya wanachama watano wa kudumu.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alionyesha picha ya kibonzo cha bomu mwaka 2012 ili kuionya dunia kwamba Iran ilikuwa miezi michache tu mbali na kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Na rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, mwaka 2017 alitishia “kuharibu kabisa Korea Kaskazini,” akimtaja kwa dhihaka kiongozi wake Kim Jong Un kama “Rocket Man.”

Nyundo ya hakimu, Kutoka nje kwa ghadhabu

Mjadala mkuu wa kwanza ulifanyika mwaka wa 1946, na ni katika miaka karibu 80 iliyopita, mila nyingi, mapambo na taratibu, pamoja na baadhi ya hadithi, zimehusishwa na tukio hilo.

Nyundo ya hakimu, ambayo ilitolewa kwa Umoja wa Mataifa na Iceland mnamo mwaka 1952, inatumika kuashiria mwanzo wa vikao vya asubuhi na jioni vya mjadala mkuu na, inapohitajika, pia kudumisha utaratibu.

Ilitumika kujaribu kumyamazisha kiongozi wa wakati huo wa Muungano wa Kisovyeti, Nikita Khrushchev, ambaye, kwa mujibu wa hekaya, alichukua kiatu chake na kupiga juu ya jukwaa ili kuwasilisha kwa nguvu msimamo wake.

Wakati mwingine, adabu ya kidiplomasia huonekana kuvurugwa pale ambapo ujumbe mzima unachagua kuondoka katika Ukumbi wa Baraza Kuu kama njia ya kupinga maoni na vitendo vya nchi nyingine Mwanachama, ingawa katika miaka ya hivi karibuni, jambo hili limekuwa la kawaida kiasi kwamba halishangazi tena.

Mara kwa mara Israel hupinga hotuba za Iran, nayo Iran pia huifanyia vivyo hivyo Israel.

María Fernanda Espinosa Garcés (kulia), Rais wa kikao cha sabini na tatu cha Baraza Kuu, akishikilia zawadi baada ya makabidhiano kutoka kwa Miroslav Lajčák (katikati), Rais wa kikao cha sabini na mbili cha Baraza Kuu. Kushoto ni Katibu Mkuu António Gute…
UN Photo/Manuel Elías
María Fernanda Espinosa Garcés (kulia), Rais wa kikao cha sabini na tatu cha Baraza Kuu, akishikilia zawadi baada ya makabidhiano kutoka kwa Miroslav Lajčák (katikati), Rais wa kikao cha sabini na mbili cha Baraza Kuu. Kushoto ni Katibu Mkuu António Guterres.

Jinsi ya kufuatilia mjadala mkuu

Ingawa mjadala haufunguliwi kwa umma, shughuli zote zinapatikana moja kwa moja na kwa kwenye UN Web TV panapo mahitaji.

Hotuba zote za mjadala mkuu zinapatikana katika Maktaba ya Dag Hammarskjöld ya Umoja wa Mataifa.

Mengi ya mijadala mkuu 78 ya awali, au muhtasari wake, yanapatikana katika Maktaba ya Kielektroniki ya Umoja wa Mataifa.