Nina imani na UN licha ya changamoto za sasa – Balozi Francis
Nina imani na UN licha ya changamoto za sasa – Balozi Francis
Hatimaye Rais wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Dennis Francis ametamatisha jukumu hilo hii leo na hivyo kuashiria kufungwa kwa pazia la UNGA78 na kufunguliwa kwa UNGA79 hapo kesho Septemba 10, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani leo ambayo ndio ukomo wa jukumu lake, Balozi Francis ameelezea mwaka mzima wa mkutano huo wa 78 kuwa ni kipindi kilichokuwa kimejaa matukio muhimu yaliyoliainisha vema Baraza hilo.
“Ulikuwa ni mkutano uliosongesha mbele zaidi juhudi za kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs,” amesema Balozi Francis.
Mikutano ya UNGA78 ilikuwa na matokeo
Mathalani ametaja matokeo ya mikutano mitatu ya ngazi ya juu kuhusu afya, akisema iliweka kwenye ajenda ya kimataifa hoja ya afya na huduma zinazojali watu.
Hoja nyingine ni suala la marekebisho ya mfumo wa ufadhali wa fedha duniani, ambapo amesema kumekuwa na maridhiano au kukubaliana juu ya umuhimu wa kufanyia marekebisho mfumo wa sasa wa taasisi za kimataifa za fedha duniani, makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mkutano wa Ufadhili kwa Ajili ya Maendeleo. Lengo ni kuhakikisha kuwa ufadhili unachochea ufanikishaji wa SDGs.
Akiangazia maadhimisho mbali mbali ya Baraza Kuu, Balozi Francis ametaja maadhimisho ya miaka 75 ya Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu na Wiki ya Uendelevu.
Katika Wiki ya Uendelevu, ya kwanza kabisa kuadhimishwa na Baraza Kuu, Balozi Francis amesema masuala ya utalii, nishati na madeni yalijadiliwa.
Ghasia Gaza ikome
Amegusia pia kuongezeka kwa ghasia Mashariki ya Kati, ambapo Baraza Kuu lilirejelea Kikao chake cha 10 Maalum cha Dharura na kupitisha maazimio matatu muhimu: kulinda raia, kutaka kuweko kwa sitisho la mapigano na kutambua sifa ya Palestina kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
“Wakati umefika kwa vita ikome Gaza,” amesisitiza Balozi Francis.
Ametamatisha mkutano wake kwa kuelezea matumaini yake kuhusu mnepo wa Umoja wa Mataifa licha ya changamoto inayozikabili. “Nina uhakika na Umoja wa Mataifa, tuna utashi, na tuna uwezo na azma ya kufanya kile kilicho muhimu.”
Balozi Francis alichukua jukumu hili tarehe 5 mwezi Septemba mwaka jana kutoka kwa Rais wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN, UNGA77 Csaba Kőrösi.