Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ECW ilivyorejesha matumaini kwa msichana Fatima wa Nigeria

Wasichana watatu wa shule wa Nigeria wenye tabasamu wakiwa wamevaa sare za bluu na nyeupe zenye miraba wameketi pamoja kwenye dawati darasani. Wanafunzi wengine wanaonekana nyuma.
© UNICEF/Mackenzie Knowles-Cour Wanafunzi katika shule moja ya msingi mashariki mwa Nigeria wakisubiri mwalimu aingie masomo yaanze.

ECW ilivyorejesha matumaini kwa msichana Fatima wa Nigeria

Utamaduni na Elimu

Alipokuwa na umri wa miaka 10 mnamo mwaka 2015, Fatima na familia yake walilazimika kutoroka nyumbani kwao Konduga, ili kuepuka mashambulizi kutoka kwa makundi yenye silaha.

Konduga iko kilomita 25 kusini mashariki mwa mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Familia ya Fatima haikuwa na namna ya kumuandikisha katika shule yoyote rasmi. Alitumia muda wake mwingi kuuza chakula.

Shukrani kwa usaidizi wa mfuko wa kimatifa wa elimu haiwezi kusubiri yaani Education Cannot Wait (ECW) na wadau wake wa kimkakati, Fatima sasa amesajiliwa katika mpango mesto unaolenga kuwapa elimu wasichana walio nje ya shule.

Msichana huyu ni mmoja wa walengwa 250 wa programu ya miezi mitano ya kusoma, kuandika na kuhesabu, ambayo imemwezesha kusoma kwa lugha ya Kihausa na hata kuandika jina lake kama anavyoeleza.

"Niliingia katika shule ya ufundi baada ya kusikia kuihusu wakati nilipokuwa nimeenda kuuza chakua. Mara moja nilihifadhi kile nilichoenda kuuza kisha nikajiandikisha jina langu. Wale ambao tulikuwa hatuendi shule tulitambuliwa na kuchaguliwa. Tulifundishwa jinsi ya kusoma na kuandika. Kabla hapo nilikuwa siwezi hata kuandika jina langu.”

Sehemu ya pili ya programu hii mseto ilihusisha kipengele cha ufundi ambapo wasichana wanaoishi katika mazingira hatarishi hupata mafunzo ya ufundi kwa muda wa miezi mitatu. Mpango unaotekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNICEF, Baraza la Wakimbizi la Norway na Save the Children.

"Pia, sasa ninajua namba, na ninaweza kupima watu  ninaposhona." Anasema Fatima ambaye katika kipengengele cha ufundi yeye amechagua ushoni wa nguo.

Mpango huu tayari umewanufaisha wasichana balehe 600 tangu kuanzishwa kwake, na kuwapa vifaa vya kuanzia na ujuzi wa kujitegemea. Fatima naye ana matumaini.

“Nataka kujifunza stadi hii ili niwahishimishe wazazi wangu na wawe na furaha. Nikimaliza kujifunza nataka kuwa mtu wa kuwashonea ndugu zangu nguo.”

Kama ambavyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatoa wito kwa nchi zote kuwekeza katika elimu na kufanya juhudi za kila namna kulinda elimu na maeneo ya kusomea, kulinda wanafunzi na walimu,   Mkurugenzi Mtendaji wa Education Cannot Wait (ECW) Yasmine Sherif, anaeleza namna ambavyo mfuko wa kimatifa wa elimu haiwezi kusubiri umejizatiti kuendelea kuiunga mkono elimu kote duniani wakati huo akitoa wito kwa kila anayeweza kuwaongezea nguvu afanye hivyo.

"Kuna ustahimilivu na watoto hawa wamepitia kiwewe na mambo mengi. Ni lazima tuwepo kwa ajili yao, na tunaweza kuona matokeo. Tunatazamia kuufanya tena mpango huu mwaka katika mwaka huu, tunatarajia kufanya hivyo kwa takribani dola milioni 15, kama sio zaidi. Ikiwa nyinyi nyote mtakuja na kutusaidia kuongeza."