Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa watangaza Julai 6 kuwa siku ya Maendeleo Vijijini

Maafisa ugaji wanaelezwa dira ya mkulima, na hivyo anajifunza ni vipi na aina gani ya takwimu zinapaswa kukusanywa na kuingizwa kwenye wavuti ambayo yenyewe sasa inachakata na kumpatia mhusika mpango wa biashara autakao.
© FAO/Luis Tato Maafisa ugaji wanaelezwa dira ya mkulima, na hivyo anajifunza ni vipi na aina gani ya takwimu zinapaswa kukusanywa na kuingizwa kwenye wavuti ambayo yenyewe sasa inachakata na kumpatia mhusika mpango wa biashara autakao.

Umoja wa Mataifa watangaza Julai 6 kuwa siku ya Maendeleo Vijijini

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuanzia mwaka ujao wa 2025 tarehe 6 ya mwezi Julai kila mwaka itaadhimishiwa kuwa siku ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo vijijini.

Hii inafuatia kupitishwa hii leo jijini New York, Marekani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa azimio namba A/78/L.84/Rev. 2 lengo likiwa kuangazia umuhimu wa maendeleo  vijijini na marekebisho yanayotakiwa ili kuweza kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs yanayofikia ukomo mwaka 2030.

Mchango wa wanawake vijijini watambuliwa

Monica Grayley ambaye ni Msemaji wa Rais wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa, amewaambia waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuwa azimio hilo linatambua mchango wa  wanawake wa vijijini katika kusongesha kilimo, kuimarisha uhakika wa kupatikana kwa chakula na kutokomeza umaskini vijijini.

“Wanafanya hivyo huku wakijitahidi kujiinua kiuchumi na kuhakikisha wana uwezo wa kumiliki ardhi na kufanya ajira zenye utu na wakati huo huo kushiriki katika kupitisha uamuzi,” amesema Bi. Grayley.

Uwekezaji wa huduma za kifedha kidijitali vijijini

Azimio pia linasisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye maeneo na huduma muhimu vijijini kama njia fanisi ya kutatua umaskini vijijini, njaa, kuanzisha ajira zenye tija, kampuni na kusongesha ujumuishwaji wa kifedha kidijitali kwa jamii za maeneo hayo na kuweka taasisi za kutoa huduma hizo vijijini.

Mathalani Vyama Vya Kuweka na Kukopa, Vyama vya Ushirika hasa kwa wanawake na vijana kupitia mikakati ya kikanda na kitaifa.

Katibu Mkuu ahamasishe kuhusu siku hii

Wajumbe wa Baraza Kuu kupitia azimio hilo, wamemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwasilisha azimio hilo kwa nchi wanachama, mashirika ya Umoja wa Mataifa, na wadau wengine yakiwemo mashirika ya kiraia, vyama vya wakulima, watu wa jamii ya asili, jamii nyinginezo, sekta binafsi na wanazuoni ili siku hii iweze kutambuliwa na kuzingatiwa.

Siku hii ni tofauti na ile ya kimataifa ya wanawake wa vijijini inayoadhimishwa tarehe 15 mwezi Oktoba kila mwaka.