Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujipanga mapema: Fahamu mambo 5 kuhusu Mkutano wa kihistoria wa Zama Zijazo

Mwonekano wa picha ya Eduardo Kobra katika Makao Makuu UN , inayoonyesha mwanamume na mtoto wakiwa wameshika tufe, huku bendera zikiwa mbele.
UN Photo/Rick Bajornas Muonekano wa sanaa ya Eduardo Kobra katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Kujipanga mapema: Fahamu mambo 5 kuhusu Mkutano wa kihistoria wa Zama Zijazo

Masuala ya UM

Je, kuna njia nyingine ambayo dunia inaweza kuendeshwa? Na katika hali ya machafuko mengi duniani, tunawezaje kufanya maisha ya mustakabali kuwa bora zaidi? Mwezi huu wa Septemba, tukio muhimu katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa linatangazwa kama fursa ya kipekee kwa jamii ya kimataifa kuunda njia mpya, kwa manufaa ya wote.

1. Mkutano wa Zama Zijazo ni nini?

Mnamo mwaka wa 2020, Umoja wa Mataifa ulitimiza miaka 75 tangu kuanzishwa, na kuadhimisha tukio hilo kwa kuanzisha mazungumzo ya kimataifa kuhusu matarajio na hofu kuhusu mustakabali.

Huu ulikuwa mwanzo wa mchakato ambao hatimaye, miaka minne baadaye, ulisababisha kufanyika kwa Mkutano wa Zama Zijazo, tukio kuu litakalofanyika mwezi huu wa Septemba katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, kabla ya mjadala wa  ngazi ya juu wa kila mwaka wa Baraza Kuu.

Mkutano huu ulifikiriwa wakati wa kilele cha janga la coronavirus">COVID-19, wakati ambapo kulikuwa na mtazamo katika Umoja wa Mataifa kwamba, badala ya kushirikiana kukabiliana na tishio hili la kimataifa lililoathiri wote, nchi na watu walijitenga.

“Tulikuwa tunakabiliwa na pengo kati ya matarajio ya waanzilishi wetu, ambayo tulikuwa tunajaribu kusherehekea katika maadhimisho ya miaka 75, na hali halisi ya dunia kama ilivyo leo,” anasema Michele Griffin, Mkurugenzi wa Sera wa Mkutano wa Zama Zijazo. 

“Halikadhalika matatizo na vitisho tuliyokutana nayo, lakini pia fursa na dosari katika jinsi tunavyoshughulikia mambo.” Anaongeza..

Msichana mdogo aliyevaa koti la waridi ameketi juu ya mabega ya mwanamume, akiwa ameshika bango la maandamano linalosomeka 'HUJAJALI lakini mimi hujali!' wakati wa maandamano ya hali ya hewa.
© UNICEF/Howard Elwyn-Jones Msichana mdogo akiwa kwenye maandamano ya Ijumaa kwa ajili ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa zilimtwika Katibu Mkuu António Guterres jukumu la kuandaa maono kwa ajili ya mustakabali wa ushirikiano wa kimataifa. Jibu lake kwa wito wao lilikuwa “Ajenda Yetu ya Pamoja”, hii ni ripoti ya kihistoria yenye mapendekezo kuhusu ushirikiano mpya wa kimataifa unaolenga kushughulikia hatari na vitisho mbalimbali, pamoja na pendekezo la kuandaa mkutano unaojikita na mustakabali mnamo mwaka wa 2024.

Tukio hili litajumuisha vikao na mikutano ya wazi itakayojikita na maeneo Matano makuu  (Malengo ya Maendeleo Endelevu na ufadhili; amani na usalama; mustakabali wa kidijitali kwa wote; vijana na vizazi vijavyo; na usimamizi wa kimataifa), pamoja na mada nyingine zinazohusu kazi zote za Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na haki za binadamu, usawa wa kijinsia,na janga la mabadiliko ya tabia nchi.

Matokeo ya moja kwa moja  yatakuwa ni toleo lililokamilika la Mkataba wa Mustakabali, litakalojumuisha  Mkataba wa Kidijitali wa Kimataifa na Tamko kwa Vizazi Vijavyo kama viambatisho, vyote hivi, vinavyotarajiwa kupitishwa na Nchi Wanachama wakati wa Mkutano.

2. Kwa nini Mkutano wa Zama Zijazo ni muhimu?

Kwa sababu, ingawa mada hizi zimejadiliwa hapo awali, na makubaliano ya kihistoria kama vile Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi yameafikiwa, kuna mtazamo mpana kwamba miundo ya Umoja wa Mataifa, mingi ambayo ilianzishwa miongo kadhaa iliyopita, haitoshi tena kuwa yenye haki au ufanisi .

Mkutano wa Zama Zijazo unatoa fursa ya kutimiza kikamilifu ahadi ambazo tayari zimetolewa, kuandaa jamii ya kimataifa kwa ajili ya dunia ya mustakabali, na kurejesha imani.

“Kiungo muhimu zaidi katika ushirikiano wa kimataifa ni imani,” anasema Michele Griffin. “Imani baina yetu. Pamoja na hisia ya ubinadamu wetu na uhusiano wetu wa karibu. Na mkutano huu umeundwa kutukumbusha sote, siyo tu serikali na siyo tu wale watakaokuwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York mwezi Septemba, bali kila mtu, kwamba tunapaswa kufanya kazi pamoja kuyatatua matatizo yetu makubwa.”

Wanaharakati vijana wa hali ya hewa, akiwemo Greta Thunberg, wanakusanyika mbele ya Makao Makuu UN kwa maandamano, wakiwa na mabango kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.
UN Photo/Manuel Elías Greta Thunberg (kati kati), mwanaharakti wa maswala ya mabadiliko ya tabianchi kutoka Sweden akiungana na vijana wanaharakati katika maandamano ya kila Ijumaa kwa ajili ya kuchagiza hatua kwa mustakabali kwenye Makao Makuu ya UN Agosti 30.

3 Wahusika wakuu ni akina nani?

Mkutano huu utatanguliwa na Siku mbili za Kuchukua Hatua, zitakazofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, ambapo wawakilishi kutoka mashirika ya kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu, mamlaka za mitaa na kanda, vijana, nchi Wanachama na wengine wengi, watakuwa na fursa ya kushiriki katika mada kuu za tukio hilo.

“Unapotazama Umoja wa Mataifa, unaweza kufikiria kwamba serikali ndizo wahusika wakuu,” anasema Griffin. “Na hilo ni kweli. Serikali ndizo zilizoketi mezani, lakini zinafanya hivyo kwa niaba ya watu wao.”

“Mashirika ya kiraia na vijana wamehusika tangu mwanzo na watakuwa kwenye mkutano,” anaeleza Bi. Griffin. “Sekta binafsi itakuwepo kama ishara ya jukumu kubwa walilo nalo katika kuabadilisha maisha na kutoa  fursa kwa watu leo. Mkutano huu ni kwa ajili ya kila mmoja na kwa kila mmoja, na kila mtu anapaswa kuona mwakilishi wake katika mkutano huu.”

Kundi kubwa la wajumbe wa vijana wakipiga picha ya pamoja katika mkutano wa LDC5 huko Doha, Qatar.
UN News/Anold Kayanda Vijana walioshiriki jukwaa la vijana kabla ya kuanza kwa mkutano wa 5 wa LDCs Doha, Qatar 5 Machi 2023

4. Nini kitafuatia?

Waandaaji wa mkutano wametilia mkazo kwamba kufungwa kwa tukio hilo hakutakuwa mwisho wa mijadala na masuala yaliyoibuliwa katika siku hizi nne.

Michele Griffin anaelezea kuwa huu ni mwanzo tu wa mchakato: “Mbegu nyingi tutakazopanda katika mkutano huu zitachukua muda kukua na kustawi,” anasema, “na sote tunapaswa kuwa sehemu ya kuhakikisha kwamba serikali zinawajibika kwa kutimiza ahadi zao katika jukwaa la kimataifa.”

Baada ya Mkutano, mkazo utaelekezwa katika kutekeleza mapendekezo na ahadi zilizo katika Mkataba wa Mustakabali. Mnamo mwezi Novemba, Azerbaijan itakuwa mwenyeji wa mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, (COP29), ambapo ufadhili wa masuala ya tabianchi utapewa kipaumbele katika ajenda; mwezi Desemba kutakuwa na Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa nchi zisizo na Bahari utakaofanyika nchini Botswana, ambapo suluhu za maendeleo endelevu zitatafutwa; na mwezi Juni ijayo, juhudi za kufanyia marekebisho muundo wa kifedha wa kimataifa (ikiwemo taasisi kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, ambazo zinafanya uamuzi kuhusu jinsi, na katika hali gani, kutoa mikopo, misaada na usaidizi wa kiufundi kwa nchi zinazoendelea) zitapanuliwa nchini Hispania, katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (https://financing.desa.un.org/ffd4Ffd4).

5. Ninawezaje kushiriki?

Act Now ni kampeni ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa inayohimiza watu wote kuchangia kwa ajili ya mustakabali bora, wenye amani na endelevu. Jukwaa hili linataka kuongeza idadi ya wale ambao wanachangia kwa kuzungumza na kufanya mabadiliko chanya, iwe kwa kujitolea katika jamii zao za mitaa, kushiriki katika maamuzi ya mitaa, au kubadilisha tabia zao za matumizi ili kuishi maisha yenye uwajibikaji zaidi wa mazingira.

Kuelekea mkutano huu, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Vijana, pia inawaunganisha vijana na washirika kwa kuzindua #YouthLead, mwito kwa viongozi wa dunia kuongeza uwakilishi wa jamii wanazohudumia katika kupanga sera za kimataifa.

KISANDUKU CHA MAANDIKO

Nembo ya kampeni ya UN ya Act Now for the Development Goals, ikiwa na maneno 'ACT SASA' katika duara jeupe lililozungukwa na miale ya rangi ya aikoni ya SDG.
United Nations ActNow ni kampeni ya Umoja wa Mataifa ya kuhamasisha watu kuchukua hatua kwa ajili ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Mwelekeo wa Baadaye

Ni kwa jinsi gani raia  wanaweza kulindwa katika dunia inayozidi kuwa na mashaka? Jinsi gani tunaweza kupunguza pengo kati ya matajiri na maskini, na kuhakikisha kwamba dunia tunayoachia vizazi vyetu ni bora kuliko ya leo?

Mwelekeo wa Baadaye unachunguza haya na masuala mengine muhimu ya kimataifa, na kueleza jinsi yatakavyoshughulikiwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Zama Zijazo mwezi huu wa Septemba.