Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ya juu kwa wakimbizi, UNHCR yatoa wito wa uwekezaji zaidi

Mpango wa ufadhili wa DAFI umesaidia mamia ya wanafunzi wakimbizi nchini India kufuata elimu ya juu na kufikia ndoto zao.
©UNHCR/Ali Johar
Mpango wa ufadhili wa DAFI umesaidia mamia ya wanafunzi wakimbizi nchini India kufuata elimu ya juu na kufikia ndoto zao.

Elimu ya juu kwa wakimbizi, UNHCR yatoa wito wa uwekezaji zaidi

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) linatoa wito wa uwekezaji zaidi katika elimu ya juu kwa wakimbizi pamoja na kuimarisha fursa za ajira kwa wahitimu wa elimu hiyo, ili kuwasaidia kufikia uwezo wao kamili.

 taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Septemba 03 mjini Geneva, Uswisi, UNHCR imesisitiza kuwa, licha ya ongezeko la wakimbizi wanaopata fursa ya elimu ya juu, wengi wao bado wanakumbana na changamoto za sera zisizo jumuishi, ukosefu wa uwezo, ada kubwa, na vikwazo vya kiutawala katika nchi nyingi. Kwa mujibu wa Kelly T. Clements, Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR, “bila mabadiliko ya sera na utekelezaji wake, upatikanaji wa elimu ya juu hauwezi kutafsiriwa kuwa ajira endelevu kwa namna ya mfumo rasmi.”

Duniani kote, takriban wakimbizi milioni 4 kati ya milioni 31.6 walio chini ya uangalizi wa UNHCR wako kati ya umri wa miaka 18 hadi 24, lakini ni asilimia 7 pekee ya wakimbizi hawa walio na fursa ya kujiunga na vyuo vikuu au taasisi nyingine za elimu ya juu. Hata hivyo, hii ni ongezeko kubwa kutoka asilimia 1 iliyoripotiwa mwaka 2019.

Utekelezaji unaendelea

UNHCR kwa sasa inasherehekea kufikia hatua ya kati ya lengo lililowekwa na wadau miaka mitano iliyopita kufikia asilimia 15 ya uandikishaji wa wakimbizi katika elimu ya juu ifikapo mwaka 2030 (ahadi ya kimataifa ya ‘15by30’). Hata hivyo, ushirikiano ulioratibiwa, wa kujitolea na endelevu wa washirika ni muhimu ili kufikia lengo hili ifikapo 2030.

Sehemu muhimu ya mkakati huu ni mpango wa ufadhili wa masomo wa DAFI (Albert Einstein German Academic Refugee Initiative), ambao umetoa nafasi kwa wakimbizi zaidi ya 26,300 kupata elimu ya juu tangu uanzishwe miaka 32 iliyopita. Ripoti ya hivi karibuni ya DAFI inaangazia njia za ajira kwa wahitimu baada ya kumaliza masomo yao, ikisisitiza umuhimu wa kuunganisha mpango wa DAFI na fursa za ajira.

Kwa mwaka uliopita, zaidi ya wanafunzi wakimbizi 9,300 kutoka nchi 54 walikuwa wamesajiliwa katika mpango wa ufadhili wa DAFI katika nchi 59. Asilimia 42 ya wanafunzi hawa walikuwa ni wanawake, na kufikia usawa wa kijinsia ni lengo kuu la mpango huu.

Vikwazo kwa  wakimbizi

Hata hivyo, vikwazo vya kisheria au kiutendaji kwa wakimbizi kupata haki ya kufanya kazi katika nchi nyingi vinafanya wahitimu wengi wa kambi za wakimbizi kushindwa kutimiza uwezo wao na kuchangia kwenye jamii zinazowahifadhi. Mpango wa DAFI unalenga kupunguza kikwazo hiki kwa kutoa msaada wa kitaalamu, kuwezesha mitandao, na kushirikiana na makampuni ili kuongeza uelewa na kuimarisha njia za ajira kwa wahitimu.