Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za kimataifa zinahitajika kumaliza ubaguzi dhidi ya watu wenye asili ya Afrika - Guteress

Waandamanaji washiriki katika maandamano ya Black Lives Matter huko Paris, Ufaransa (Picha ya maktaba)
Unsplash/Thomas de Luze
Waandamanaji washiriki katika maandamano ya Black Lives Matter huko Paris, Ufaransa (Picha ya maktaba)

Hatua za kimataifa zinahitajika kumaliza ubaguzi dhidi ya watu wenye asili ya Afrika - Guteress

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa ili “kutokomeza ubaguzi na ubaguzi wa rangi  dhidi ya watu wenye asili ya Afrika.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Asili ya Afrika ambayo huadhimishwa kila Agosti 31, Guiteress amesema "watu wa asili ya Afrika wamechangia jamii kupitia uongozi na uharakati, lakini urithi wa utumwa na ukoloni unaendelea."

Mnamo Desemba 2013, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza Muongo wa Kimataifa kwa Watu Wenye Asili ya Kiafrika ili kushughulikia masuala ya utambuzi, haki, na maendeleo.

Muongo ulioanza mwaka 2015 ulilenga kukuza haki za watu wenye asili ya Afrika, kuongeza uelewa juu ya michango yao ya kitamaduni, na kuimarisha mifumo ya kisheria ili kupambana na ubaguzi wa rangi.

Mnamo mwaka 2021, tarehe 31 Agosti ilitambuliwa kama siku ya kimataifa.

Guterres amewataka Nchi Wanachama kutangaza muongo wa pili wa kimataifa “ili kusaidia kuharakisha juhudi za kimataifa za mabadiliko ya kweli.”

Kukabiliana na ubaguzi wa rangi

Guteress amesema, “ubaguzi wa rangi wa kimfumo umeenea na unaendelea kubadilika na kuwa wa aina mpya. Baadhi ya mabadiliko haya ni pamoja na teknolojia mpya, ambapo au 'algorithm' yaani mfumo wa kidijitali ambao unaamua jinsi ya kusambaza maudhui kwa mitandao ya kijamii kwa kufuatilia mitindo, umri au ajira ya mtu binafsi zinaweza kuongeza ubaguzi.”

Kwa mujibu wa Guteress, Umoja wa Mataifa unaweka kipaumbele katika kutokomeza "janga la ubaguzi na ubaguzi wa rangi" na imeanzisha Ofisi mpya ya Kupambana na Ubaguzi wa rangi ambayo itashughulikia ubaguzi wa rangi wa mahali pa kazi.

“Tunahitaji pia serikali zichukue uongozi kwa kusonga mbele na kutekeleza sera na sheria za kushughulikia ubaguzi wa kimfumo wa rangi wa na kuhakikisha ushirikishwaji,” ameongeza Guterres.

“Kuna haja ya kutoa haki ya urejesho ili kushughulikia uhalifu wa utumwa.” Ameongeza huku akitoa wito wa juhudi za kimataifa ili kujenga dunia ya usawa, fursa, na haki kwa wote.

Mfumo na muundo

Wataalamu walioteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la UN pia walitoa wito wa kukomesha ubaguzi kabla ya Siku ya Kimataifa huku wakitambua "kwamba mamilioni ya watu wenye asili ya Kiafrika kote ulimwenguni wanaendelea kuwa waathiriwa wa ubaguzi wa mfumo na muundo na ubaguzi wa rangi."

Kama ilivyo kwa Katibu Mkuu, wataalamu hao wanatoa wito wa Muongo wa Pili wa Kimataifa kwa Watu Wenye Asili ya Kiafrika kuanzia 2025-2034 kwani “bado tuko mbali na kuhakikisha kuheshimiwa kwa haki za binadamu na uhuru wa kimsingi wa watu wenye asili ya Kiafrika, ikiwa ni pamoja na kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi yao.”

Muongo ujao unahitaji mwelekeo thabiti zaidi juu ya utambuzi, haki, na maendeleo huku ukikabiliana na changamoto zinazowaathiri moja kwa moja watu wenye asili ya Kiafrika.

Wataalamu hao wamesema Nchi Wanachama zinapaswa kuunda na kutekeleza zana za haki za binadamu, mikakati, na mifumo ya ufuatiliaji ili kushughulikia ubaguzi wa rangi wa mfumo na kuhakikisha ulinzi kamili na kuheshimiwa kwa haki za watu wenye asili ya Kiafrika katika muongo ujao.

Mkutano wa zama zijazo au Summit of The Future, utafanyika mwezi Septemba na Mkutano wa 16 wa Nchi Wanachama kuhusu bayonuai utafanyika mwezi Oktoba, wataalamu wanawahimiza wanachama kutumia mikutano hii muhimu kama fursa ya kushughulikia masuala yanayohusu watu wenye asili ya Kiafrika.

“Wakati wa kuchukua hatua madhubuti ni sasa,” wamesema. “Tuchukue fursa hizi ambazo zinaweza kuleta mabadiliko ya maana kwa watu wenye asili ya Afrika na kwa ubinadamu wote.”