Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Timu ya Wakimbizi yang'ara katika sherehe za Ufunguzi wa 'Paralympic' Paris 2024

Mchezaji wa  taekwondo aliye na ulemavu Zakia Khudadadi, kutoka Afghanistan anashiriki Michezo ya watu wenye ulemavu ya ya Olimpiki 2024 huko Paris.
© IPC Mchezaji wa taekwondo aliye na ulemavu Zakia Khudadadi, kutoka Afghanistan anashiriki Michezo ya watu wenye ulemavu ya ya Olimpiki 2024 huko Paris.

Timu ya Wakimbizi yang'ara katika sherehe za Ufunguzi wa 'Paralympic' Paris 2024

Wahamiaji na Wakimbizi

Baada ya kushinda changamoto kubwa ya kufikia Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu (Paralympic), timu ya wanariadha wakimbizi sasa inalenga kuwania medali, kushinda, na kuleta matumaini kwa wengine.

Wanamichezo wa Timu ya Wakimbizi ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu, ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kushiriki, wamepokelewa kwa shangwe kubwa walipojiunga na maandamano ya maelfu ya wanariadha wakipita mtaa wa Champs-Élysées na kuingia katika Uwanja maarufu wa Place de la Concorde jijini Paris, Ufaransa Jumatano tarehe 28 Agost, wakati wa Sherehe za Ufunguzi za kuashiria mwanzo wa Michezo ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2024.

Makumi ya maelfu ya watazamaji walijitokeza mitaani kuwashangilia wanariadha 4,400, akiwemo mbeba bendera wa Timu ya Wakimbizi ya Paralimpiki na mkimbiaji katika mbio za T11, Guillaume Junior Atangana.

"Timu hii ya Wakimbizi ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu ni mojawapo ya hadithi kubwa za Paralimpiki ya Paris 2024," amesema Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ya Walemavu, Andrew Parsons. "Kila mmoja wa wanariadha hawa amepambana na changamoto kubwa kufika hapa na ana ujumbe mzito kwa ulimwengu mzima. "Wote ni mabingwa wa michezo." Ameongeza.

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Filippo Grandi, amesema, "timu ya Wakimbizi ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu ni msukumo kwetu sote. Wanariadha hawa wa ajabu wamevuka vikwazo visivyoweza kufikirika ili kufikia kilele cha mafanikio ya michezo."

Wanariadha hao wanane wakimbizi wanatoka katika nchi sita na wanawakilisha zaidi ya watu milioni 120 waliolazimika kuhama makazi yao duniani kote kwa sababu ya vita, migogoro, vurugu na ukiukwaji wa haki za binadamu. Hii inajumuisha angalau watu milioni 18 wenye ulemavu, ambao wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi za vurugu, ubaguzi, utumikishwaji na unyanyasaji, pamoja na vikwazo vya kupata msaada muhimu, elimu, michezo na fursa za kujipatia riziki.

"Uwepo wa Timu ya Wakimbizi ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu katika jukwaa la kimataifa unatoa ujumbe wa matumaini kwa mamilioni ya wakimbizi duniani kote, na kwa hakika kwetu sote. Timu hii ya ajabu inatukumbusha umuhimu wa watu wenye ulemavu kupata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika jamii kwa usawa," amesema Grandi.

Hii ni mara ya tatu kwa Timu ya Wakimbizi ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu kushiriki kwenye Michezo hiyo. Timu ya kwanza, iliyojumuisha wanariadha wakimbizi wawili, ilishiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu ya Rio 2016. Timu hii iliongezeka hadi wanariadha sita walioshiriki huko Tokyo 2020. Mwaka 2024 wanariadha wanane wakimbizi na waongozaji wawili watashiriki katika michezo sita kati ya 22 ikiwa ni pamoja na riadha ya walemavu, kuinua uzito kwa walemavu, tenisi ya mezani ya watu wenye ulemavu, taekwondo ya watu wenye ulemavu, mashindano ya mbio tatu za watu wenye ulemavu , na mchzo uitwao fencing ya watu walemavu ambapo wanatumia kiti cha magurudumu kupambana kwa upanga.

Mwanariadha mkimbizi wa kwanza kushindana siku ya kwanza atakuwa, Zakia Khudadadi, bingwa wa Ulaya mwaka 2023 wa taekwondo ya watu wenye ulemavu katika uzani wa 47kg. Khudadadi, ambaye sasa anaishi Ufaransa, ni mtetezi wa haki za wanawake duniani kote aliyegonga vichwa vya habari baada ya kukimbia kwa njia ya kijasiri kutoka nchi yake siku chache kabla ya Michezo ya Tokyo 2020.

"Timu hii inaundwa na wanariadha, kila mmoja akiwa na hadithi tofauti," amesema Khudadadi. "Kuwa sehemu ya timu hii ni heshima, na lengo langu ni kuonesha jinsi wanawake wanavyoweza kuwa na nguvu na kuhamasisha wasichana na wanawake wengine kufuata michezo na kulenga Michezo." Ameongeza.

Hadi Hassanzada, mkimbizi wa Afghanistan anayeishi Austria, anashindana katika para taekwondo kwenye Michezo ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu ya 2024 huko Paris.
© IPC Hadi Hassanzada, mkimbizi wa Afghanistan anayeishi Austria, anashindana katika para taekwondo kwenye Michezo ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu ya 2024 huko Paris.

Katika taekwondo ya watu wenye ulemavu, Hadi Hassanzada pia  anatarajia kuiga mafanikio ya kushangaza ya mkimbizi mwenzake Khudadadi atakaposhindana katika uzani wa wanaume wa 80kg katika michezo yake ya kwanza.

Mbeba bendera na mkimbiaji wa riadha ya walemavu, Atangana alimaliza katika nafasi ya nne katika mbio za mita 400 T11 kwenye Michezo ya Paralimpiki ya Tokyo 2020, akikosa tu medali. Katika Sherehe za Ufunguzi za Jumatano, Atangana amebeba bendera ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu akiwa na mwongozaji wake katika mbio za T11 mita 400 ambaye pia ni mkimbizi Donard Ndim Nyamjua. Atangana pia atashindana katika tukio la T11 mita 100 huko Paris.

Ibrahim Al Hussein anashindana katika michezo ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu kwa mara ya tatu mfululizo, lakini katika mbio tatu za walemavu kwa mara ya kwanza baada ya hapo awali kushindana katika mashindano ya kuogelea ya walemavu.

Salman Abbariki anashindana kwa mara ya kwanza katika timu ya wakimbizi wenye ulemavu  katika mashindano ya kurusha tufe, mchezo ambao alishindana awali kabla ya kuwa mkimbizi huko London 2012, na katika Michezo ya watu walio na  umavu ya Asia mwaka 2010 ambapo alishinda dhahabu na kuvunja rekodi ya Asia.

Hadi Darvish anashindana katika kuinua mizani kwa walemavu, kufuatia mafanikio yake ya kushinda medali ya shaba katika tukio la wanaume la hadi 80kg kwenye Kombe la Dunia la Tbilisi 2024 mwezi Juni, katika tenisi ya mezani ya walemavu, Sayed Amir Hossein Hosseini Pour anatarajia kuendeleza mafanikio yake baada ya kushinda medali mbili za dhahabu katika Michezo ya Vijana Walemavu ya Asia 2021 huko Bahrain.

Katika fencing ya watu wenye ulemavu wanotumia kiti chenye magurudumu, Amelio Castro Grueso pia anatarajia kurudia mafanikio ya awali baada ya kushinda shaba katika kundi la B la  ya wanaume kwenye Mashindano ya Amerika ya  fencing kwa walemavu wanaotumia  Kiti cha Magurudumu nchini Brazil mwezi Mei.

Timu ya Wakimbizi ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu inatumaini kufuata nyayo za Timu ya Wakimbizi ya Olimpiki ambayo ilifurahia mafanikio ya kihistoria huko Paris 2024, ikishinda medali yake ya kwanza kabisa. "Tumepitia mengi, lakini tuko hapa kushinda. Hatutakubali kushindwa," amesema Khudadadi.

UNHCR, inashirikiana na Kamati ya Kimataifa ya watu wenye ulemavu (IPC), Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, na Olympic Refuge Foundation ili kusaidia wakimbizi katika Michezo ya Olimpiki na ya Olimpiki ya Watu wenye Ulemavu huko Paris.